Tuesday 2 June 2015

LUKUVI AFANYA MAREKEBISHO MRADI WA MJI WA KIGAMBONI


Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imefanya marekebisho ya matangazo mawili Gazeti la Serikali, kwa kupunguza  kata za mradi wa uendelezaji wa mji wa Kigamboni, Dar es Salaam kutoka tisa hadi sita na eneo la mradi kutoka hekta 50,934 hadi 6,494.


 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (pichani), aliyasema hayo wakati  akizungumza kwenye mkutano wa pamoja baina ya wananchi wa Kigamboni, kamati ya ufuatiliaji malalamiko ya wananchi wa eneo hilo, Mbunge, Waziri wa Tamisemi, Mkuu wa wilaya na wadau wengine.
 
Alisema ili kuondoa malalamiko ya wananchi wa eneo hilo kwa muda mrefu, amerekebisha Tangazo la Serikali Na. 229 la mwaka 2008 lililotaja maeneo ya mpango kuwa ni Kigamboni, Vijibweni, Mjimwema na Kibada kwa kuongeza Kata ya Tungi na sehemu ya Kata ya Somangila katika mitaa miwili ya Kizani na Mbwamaji ambazo hazikuwamo kwenye tangazo la awali. 
 
Alisema pia amerekebisha Tangazo la Serikali Na. 6 la mwaka 2013 lililotaja eneo la Mpango kuwa na kata tisa kwa kupunguza ukubwa wa eneo la Mpango kutoka hekta 50,934 hadi 6,494 na kupunguza idadi ya kata kutoka tisa hadi sita kwa kuondoa Kata za Kisarawe II, Kimbiji na Pembamnazi kwenye eneo la mpango.
 
Lukuvi alisema pia amerekebisha Tangazo la Serikali Na. 7 la mwaka 2013, lililoanzisha Mamlaka ya Uendelezaji mji Mpya wa Kigamboni (KDA) na kutaja majukumu yake kwa  kuondoa jukumu la KDA la kuwa mwendelezaji Mkuu wa eneo la Kigamboni. 
 
Waziri Lukuvu alifafanua kuwa katika marekebisho hayo, pia ameridhia marekebisho ya vipengele mbalimbali, lengo likiwa ni kukamilisha mpango wa uendelezaji Mji mpya wa Kigamboni kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine na kuondoa dhana iliyokuwa imejengeka awali kuwa Serikali ingetwaa maeneo ya wananchi, kuwahamishia mahali na kuuza maeneo yao kwa wawekezaji kwa gharama kubwa na bila ridhaa ya wananchi.
 
“Kwa mujibu wa dhana mpya, wananchi wa Kigamboni wana fursa ya kushiriki katika uendelezaji kwa mwananchi mwenyewe kuwa mwendelezaji katika eneo lake kwa kuzingatia mpango; mwananchi kulipwa fidia au kuuza eneo lake kwa mwekezaji kwa hiari yake kwa kuzingatia bei ya soko na kuingia ubia na mwekezaji kwa kutumia ardhi yake kama mtaji,” alifafanua.
 
Alibainisha kuwa katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huo, jukumu la Serikali litakuwa ni kuandaa mazingira wezeshi katika kila hatua ya utekelezaji, na kwamba KDA itakuwa na jukumu la kuratibu wadau mbalimbali na kusimamia utekelezaji wa mpango kwa ujumla. 
 
Waziri huyo alisema kwa sasa serikali itaanza kutengeneza barabara za mji huo, na kwamba kila mwananchi atakayekutwa katikati ya barabara atalipwa fidia kwa wakati kwa kuwa zaidi ya Sh. bilioni tatu zimetegwa kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hiyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!