Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema kuwa, rushwa imeota mizizi ndio maana viongozi wanaochaguliwa badala ya kuwajibika kwa wananchi pindi wanapochaguliwa, wamekuwa wakiwatumikia waliowawezesha kifedha.
Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Dk. Helen Kijo-Bisimba, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa warsha iliyoambatana na mkutano mkuu wa 14 wa wanachama wa kituo. Sherehe hizo zilitanguliwa na mada isemayo, ‘miaka 20 ya kituo katika kupigania haki na usawa, nafasi ya wanachama’.
Akizungumza na wanachama hao, Dk. Kijo-Bisimba alisema kuwa nchi inakabiliwa na mambo matatu ambayo ni uchaguzi mkuu, Katiba Mpya na watu ambao wanaonyimwa haki zao.
“Haya mambo matatu sisi kama kituo, wakati tunasherehekea miaka 20 tunaweza kusema tumepiga hatua, lakini bado tunakazi mbichi inayotukabili mwaka huu nayo ni uchaguzi mkuu, katiba mpya na watu wenye kunyimwa haki,” alisema. Aliongeza kuwa nchi imefikia hatua rushwa imeota mizizi na watu wake wanaona hawawezi kufanya chochote bila kutoa rushwa.
Pia alisema tatizo kubwa kipindi cha uchaguzi ni kuwepo kwa nguvu kubwa ya fedha kutumiwa na wagombea ndio maana baada ya kushinda hujikuta wakirudisha fadhila kwa wale waliowawezesha.
Aidha alitoa wito kwa wananchi waungane kwa pamoja kukataa vitendo hivyo vya matumizi ya fedha ili kuweza kupata kiongozi bora.
Alisema wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya kituo mambo mengine wanayoyaangalia ni jinsi ya kukabiliana na changamoto za usoni.
Alisema hadi sasa kituo kimeweza kusaidia wananchi takribani 200,000 waliofika moja kwa moja LHRC. Aliongeza kuwa wameweza kusimamia kesi mbalimbali ambazo miongoni mwake zipo zilizotolewa maamuzi na wao kushinda.
“Changamoto tunazokutana nazo wakati tunapoamua kusimamia kesi zenye maslahi ya Umma, huwa tunatozwa faini kubwa ambazo kituo kinashindwa kuzilipa,” alisema. Pia alisema tatizo lingine ni ucheleweshwaji wa utoaji maamuzi wa baadhi ya kesi ambazo wanazisimamia.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga, ametoa wito kwa LHRC pindi kesi za wananchi zinapowafikia na wakashindwa kuzitatua, wazifikishe kwenye tume hiyo kwa hatua zaidi. “Iwapo ikabainika kabla ya kupelekwa mahakamani na ikawa nyinyi mmeshindwa basi tuleteeni sisi tushughulike nalo,” alisema.
Kadhalika, amekitaka kituo hicho wakati kikiadhimisha miaka 20 kikumbuke maneno haya,’ kila mtu atamani kuona jamii yenye usawa’.
NIPASHE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment