Stephen Masato Wasira ni mwanasiasiasa nguli wa CCM; kada madhubuti ambaye chama kinajivunia kuwa naye. Amekuwapo katika awamu zote nne za uongozi akishika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama na serikali.
Katika umri wa miaka 70 na hata baada ya kutumika awamu zote nne, Wasira hajafikiria kung’atuka katika siasa na sasa ameamua kujitosa kuwania urais akiomba ridhaa kupitia CCM.
Mwanasiasa huyu mwenye historia ndefu, sasa kama Mbunge wa Bunda, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika amewakuna watu mbalimbali wilayani kwake alipotangaza kuwania urais. Baadhi ya watu mbalimbali wakiwamo baadhi aliosoma nao katika ngazi tofauti za elimu wamesema ni “chuma cha pua”.
Mmoja wa wakazi hao wa Bunda, John Mkaka anasema anamfahamu vyema Wasira tangu alipokuwa akigombea ubunge wa Jimbo la Mwibara miaka ya 1970, kabla ya jimbo hilo kugawanywa na yeye kuamua kugombea jimbo la Bunda mwaka 1985.
“Namfahamu vizuri, aligombea ubunge akiwa kijana mdogo, nafikiri alikuwa na miaka 23 wakati huo. Yule ni chuma cha pua amesaidia sana katika mambo mbalimbali ya maendeleo katika jimbo letu, kila nafasi aliyopewa aliimudu vyema,” anasema Mkaka.
Anasema ingawa kuna baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakimhukumu kwamba ameshindwa, anachotambua yeye ni kwamba kuna mambo mengine yamemshinda kutekeleza kwa sababu yapo juu ya uwezo wake, likiwamo suala la maji.
“Wapo wanaodai kwamba hajaleta maji, kwani yeye ndiye anayepaswa kuyaleta? Najua ametetea sana tupate maji hadi kuna wakati alipewa mkandarasi ili mradi uanze, lakini kuna mambo sijui ni ufisadi yakakwamisha tena,” anasema.
Mzee Mkaka anasema hali ya nchi kwa sasa imeharibika hasa kwenye nyanja ya uongozi ambapo ufisadi unazidi kustawi tangu ulipoanzia wakati wa uongozi wa awamu ya pili, kisha ya tatu na sasa ya nne. Anasema kumekuwa na tofauti kubwa ukilinganisha na uongozi wa awamu ya kwanza.
Anavyofahamu, Wasira amewasaidia wazee kuwa na umoja wao wa kusaidiana ambapo wanajiendeleza, tofauti na vijana ambao waliunganishwa lakini wakasambaratika. Anaamini kwamba akipata nafasi ya kuchaguliwa kuwa rais anaweza kufanya vizuri.
Jacob Iparapara, mkazi wa Kabasa anasema anamfahamu Wasira kwa jina la Mataluma alilokuwa akiitwa utotoni. Alisema alionekana kuwa kama mtu dhaifu, mpole na asiyependa mambo ya ukorofi.
“Maana ya Mataluma ni watu waliokuwa wanashurutishwa kuweka matuta ya kuzuia maji kwenye mashamba. Hilo ni jina lililokuwa limezoeleka sana, alikuwa anachokozwa, mara kwa mara, lakini hakuwa mwepesi katika ugomvi, hivyo alikuwa hapendi kucheza hata muda wa mapumziko,” anasema,
Iparapara anasema walipokuwa wanasoma Shule ya Msingi ya Nyambitirwa baada ya kumaliza darasa la nane, Wasira alionekana kujihusisha zaidi na masuala ya kisiasa.
“Akawa mzungumzaji mzuri tofauti na alivyokuwa mwanzoni. Mwalimu Julius Nyerere akampenda na kumpa cheo cha Ofisa Maendeleo kabla ya kuwa Katibu wa Tanu wa mkoa. Asingehamishwa labda angekuwa amefanya mambo makubwa ya maendeleo zaidi,” anasema Iparapara.
Mwenyekiti wa Kata ya Bunda, Chacha Gikalo anasema alimfahamu Wasira wakati yeye alipokuwa mwandishi wa ushirika wa Kyakabari, lakini baada ya muda aliondoka akagombea udiwani akashindwa akaenda kuishi Ukerewe baada ya kupata kazi ya afisa maendeleo.
“Baadaye nikasikia kaomba nafasi ya kuwa Katibu wa Tanu wa Geita ambayo hata mimi niliiomba lakini akapata yeye kabla ya kuja kugombea ubunge mwaka 1970. Ni mtu ambaye anaweza siasa kwa sababu amekuwa akifanya kazi ya siasa kwa kipindi kirefu katika maisha yake na mara kwa mara amekuwa akipewa nafasi ya uwaziri,” anasema Gikalo.
Kwa mujibu wa Gikalo, Wasira ni kiongozi mwadilifu ingawa alisema wakati mwingine ana kauli za ukali. Anaamini hayo ndiyo maumbile yake hivyo anaweza kuwa rais mzuri kwa namna nyingine.
“Lakini nimeshangazwa na hatua yake hiyo kwamba naye ni miongoni mwa wanaowania urais. Nasema hivyo kwa sababu mwaka jana Agosti alipotuita wenyeviti wote wa kata wa jimbo, tulimuuliza kuhusu kugombea nafasi hiyo lakini alikataa na akatuomba tuendelee kumuunga mkono kutetea ubunge,” anasema Gikalo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Bunda, Flavian Nyamageko anasema mbunge huyo amewahi kujaribu kuwasaidia vijana kwa kuwachangia Sh3 milioni kutoka kwenye mfuko wa jimbo.
“Fedha hizo vijana walizitumia kwa kuanzisha kikundi cha saccos iliyoitwa Uvishira ikiwa na maana umoja wa vijana wa shida na raha, lakini walikumbwa na mgogoro wakashindwa kuendelea,” anasema Nyamageko .
Hata hivyo, anasema kuna ahadi ambazo mbunge huyo ameshindwa kuzitimiza, ikiwamo aliyoitoa mwaka 2011 ya kuunda vikundi vya vijana ili waweze kupewa fedha za kuanzisha miradi chini ya Mfuko wa Maendeleo wa Tasaf.
Ibrahimu Mussa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa UVCCM, anasema kwamba amefurahi kusikia mbunge wao ni miongoni mwa wanaowania nafasi ya urais.
“Machi Mosi kwenye mkutano wa CCM wa mkoa alitueleza rasmi kwamba katika idadi ya majina yatakayojitokeza ya watia nia ya kugombea urais, basi tutambue jina lake litakuwa miongoni mwao. Tumefurahi kwa kuwa ametumia haki yake ya kikatiba, amejipima amejiona anazo sifa, akichaguliwa tutamuunga mkono,” anasema Mussa.
Alfred Malagila, aliyesoma na Wasira Shule ya Msingi ya Balili (SDA) mwaka 1955 iliyokuwa ikimilikiwa na Kanisa la Sabato, anamwelezea Wasira kuwa ni mtu mwenye msimamo.
“ Wasira anatoka kwenye kabila la Wasizaki na mimi ni Msukuma, hivyo ni mtani wangu. Ninamfahamu kwa kuwa tulisoma naye ingawa baadaye alihama. Alilelewa na wajomba zake maana baba yao alifariki yeye akiwa na umri mdogo,” anasema Malagila
Kuhusu misimamo, Malagila anasema Wasira hayumbi hasa katika mambo ambayo anaamini kuwa ni ya maendeleo, hali ambayo ilimfanya wakati fulani kumfuata Mwalimu Nyerere ili kudai makao makuu ya Wilaya ya Bunda.
“Alikwenda nyumbani kwa Mwalimu na kumwelezea umbali wa makao makuu ya Bunda kutoka Kisoja hadi Mugumu. Nyerere alichukua jembe na kwenda kulima, Wasira naye alichukua akamfuata akalima naye hadi saa 7:00 mchana Mwalimu alipomwambia waondoke na akakubali kujenga makao makuu,” alisema.
Pia, anasema Wasira alikorofishana na Joseph Sinde Warioba kwa sababu za kisiasa na akiwa mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Kuzugu waliitwa na Mwalimu Nyerere. Alituhumiwa kuwa anataka ubunge kwa kutumia fedha.
Wasira na Warioba walichuana mwaka 1990 ambao alishindwa, lakini matokeo hayo yalitenguliwa baada ya kubainika kwamba Warioba alifanya kampeni kwa kutumia gari la Waziri Mkuu.
“Baadaye Wasira aliamua kuhama CCM mwaka 1995 na kujiunga na NCCR- Mageuzi akagombea jimbo hilo akamshinda Warioba ambaye aliamua kukata rufaa ambayo ilimng’oa kabisa katika siasa za ubunge,” anasema Malagila.
Anasisitiza kuwa yeye ni miongoni mwa watu ambao walikuwa wakimshawishi Wasira kurudi CCM kila alipokutana naye na hatimaye walifanikiwa alirejea.
Suzana William, aliyesoma pia na Wasira, anasema alikuwa na uwezo wa wastani katika masomo.
“Ukweli Wasira hakuwa mkorofi hali ambayo iliwafanya wanafunzi watundu wapende kumchokoza,” alisema William
No comments:
Post a Comment