Wakimbizi 720 kati ya 800 wanaoingia nchini kutoka Burundi wamewekwa kwenye Kambi ya Nyarugusi, Kasulu – Kigoma wengine wakiendelea na taratibu za kujiandikisha.
Raia hao wa Burundi wanakimbia ghasia zinazoikumba nchi yao baada ya Rais Pierre Nkurunziza (pichani) kuteuliwa na chama chake cha CNDD – FDD kugombea urais kwa muhula wa tatu kinyume na Katiba katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Juni 26, mwaka huu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Isack Nantanga alisema jana kuwa, Serikali haina mpango wa kufungua kambi mpya, badala yake wakimbizi wote watahifadhiwa kwa muda katika kambi hiyo wakati wakisubiri hali ya utulivu kurejea nchini mwao.
Nantanga alisema, wakimbizi 51 waliojaribu kuingia nchini kupitia mpaka wa Kagera walirudishwa kwao kwa sababu walikiuka sheria ya Umoja wa Mataifa. Alisema watendaji wa Serikali wanafuata taratibu zote za kuwapokea wakimbizi.
“Sheria za UN haziruhusu mkimbizi kuvuka nchi mbili kuingia nchi nyingine. Hawa 51 waliingia Rwanda ndipo wakaja Tanzania kupitia Mkoa wa Kagera. Hii siyo sahihi,” alisema ofisa huyo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani.
Baadhi ya raia wa Burundi wamekimbilia nchi jirani za Rwanda, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Rwanda ndiyo imepokea wakimbizi wengi ambao ni zaidi ya 20,000.
Nantanga alisema Serikali za Vijiji, wilaya na halmashauri za Mkoa wa Kigoma zinaratibu utaratibu wa kuwapokea huku Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR) likitoa msaada wa chakula na malazi.
“Takwimu kamili za wakimbizi walioingia nchini mwishoni mwa wiki hii tutazitoa kesho (leo). Jeshi la Wananchi linafanya kazi yake kuhakikisha kuna amani na usalama, pia serikali za mitaa zinaratibu shughuli ya kuwapokea wakimbizi hao,” alisema.
Akizungumzia hali ya viongozi kujiongezea muda na kusababisha vurugu, Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Profesa Abdallah Safari alisema changamoto kubwa anayoiona ni viongozi wengi wa Kiafrika kutumika kama vibaraka wa mataifa ya nje.
Alisema wawekezaji wengi wanaoingia mikataba na nchi za Afrika, wamekuwa wakinufaika zaidi na nchi hizo hivyo kushinikiza viongozi wengi kubaki madarakani ili kuendelea kulinda masilahi yao kiuzalishaji.
“Kuna nguvu ya nje na nguvu ya ndani, ile ya nje inasukumwa na wawekezaji. Kwa mfano nchini hakuna mwekezaji anayependa upinzani uingie madarakani endapo kuna dalili kama hizo, lakini atashinikiza ili kulinda masilahi yake, kwani mikataba mingi walioingia ni ya unyonyaji tu,” alisema.
No comments:
Post a Comment