Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe jana aliwaaga wafanyakazi wa wizara hiyo akisema hatafanya kazi tena wizarani hapo katika uongozi wa awamu ya tano.
Membe anayetajwa kuwa miongoni mwa wanaCCM wanaowania urais alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo, ambao hufanyika kila mwaka kujadili masuala ya usalama kazini, utawala bora na mambo mengine yanayohusu wizara hiyo.
Mbunge huyo wa Mtama mkoani Lindi ameshatangaza kwamba hatagombea tena ubunge ifikapo Oktoba.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa baraza hilo, Membe alisema mkutano huo ni wa mwisho kwake kuhudhuria katika wizara hiyo kwa kuwa hafikirii tena kuongoza wizara hiyo.
Hata hivyo, Membe ambaye yumo kwenye kundi la wabunge sita waliopewa onyo na CCM baada ya kutiwa hatiani na Kamati Kuu ya chama hicho kwa kuanza kampeni kabla ya wakati na kufanya mambo yanayokiuka maadili ya chama hicho, alifafanua kuwa uamuzi huo si tafsiri ya yeye kugombea urais au vinginevyo, bali yote ni mipango aliyokuwa nayo awali.
“Kabla ya kumaliza mazungumzo yangu, naomba nitumie nafasi hii kuwaaga rasmi katika baraza hili kwani sitegemei kurejea tena kuongoza wizara hii baada ya Uchaguzi Mkuu, lakini niseme tu kwamba, sifanyi hivyo kwa ajili ya urais, lakini kama ikiwa hivyo pengine ni mapenzi ya Mungu.
“Tuombeane uzima tu kwa kipindi kijacho, ninaamini hazina niliyoiacha hapa ni kubwa na muhimu sana kwa Taifa. Kuna hazina kubwa ya viongozi ambao wanaweza kutumika kwa Taifa hili, wizara hii ni chombo cha kupika viongozi na mimi kama nikipata nafasi yoyote itabidi niangalie viongozi wa kufanya nao kazi katika wizara hii.”
Membe alipongeza juhudi na ushirikiano ulioonyeshwa na wafanyakazi wa wizara hiyo huku akielezea hatua zinazoendelea kwa sasa ikiwamo bajeti ya Sh3.3 bilioni iliyotengwa kuwarudisha nyumbani watumishi 45 waliomaliza muda wao wa kufanya kazi nje ya nchi.
“Miongoni mwao kuna wachumi, wahasibu na mabalozi. Watarejea nyumbani na kuwapeleka wengine kujaza nafasi, utaratibu huo tayari umeshaanza miezi mitatu iliyopita,” alisema Membe.
Kuhusu madai ya nyongeza za mishahara kwa wafanyakazi hao, Membe aliwataka kuwa na uvumilivu kwa kuwa suala hilo linafanyiwa kazi na Rais Jakaya Kikwete.
Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje, Rose Jairo alitoa shukrani kwa Membe huku akimwahidi: “Tunashukuru sana na bado tuna imani na wewe... tutakuwa pamoja kwa kuunga mkono katika harakati zako.”
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment