Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani, imezindua program ya uimarishaji ulinzi katika Bandari ya Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kwa kutumia mbwa maalum kubaini dawa za kulevya na pembe za ndovu.
Wizara za Uchukuzi, Mambo ya Ndani na Maliasili na Utalii, ndizo zitakazohusika na program hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema jijini Dar es Salaam juzi kuwa program hiyo inalenga kuimarisha ulinzi katika maeneo hayo kwa kuanzia ili kupambana na wasafirishaji wa dawa za kulevya na pembe za ndovu.
Chini ya mpango huo, Polisi wa Tanzania watapatiwa mafunzo nchini Marekani ya kutumia mbwa maalum katika maeneo hayo ifikapo Septemba, mwaka huu.
Waziri Nyalandu alisema dhamira ya serikali ni kuwa na ulinzi wa namna hiyo katika mipaka yote ya nchi kuhakikisha taifa linakuwa salama kutokana na uharibifu unaofanywa na watu wasio na mapenzi mema na taifa lao.
Kamishina wa Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani, Gil Kerlikowske, kwa upande wake alisema baada ya kupatiwa mafunzo katika vyuo vya idara hiyo, Polisi wa Tanzania watarejea nchini wakiwa na mbwa hao tayari kwa kuanza kazi ya kupambana na wasafirishaji haramu wa dawa za kulevya na bidhaa zitokanazo na wanyamapori. “Program za kutumia mbwa hawa maalum, huongeza kwa kiwango kikubwa uwezo wa bandari na viwanja vya ndege kubaini bidhaa haramu zinazoingizwa au kutolewa nchini,” alifafanua.
Ni mara ya kwanza katika historia ya idara hiyo kuwezesha matumizi ya mbwa katika kubaini pembe za ndovu.
Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia Miundombinu katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Aloyce Matei, alisema suala la ulinzi na usalama, ni kati ya vipaumbele vikubwa vya mamlaka hiyo.
“Tunakaribisha sana program hii katika bandari yetu,” alisema Matei aliyemwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu TPA, Awadh Massawe.
Baada ya mafunzo hayo, wataletwa mbwa maalum wanne nchini; wawili Bandari ya Dar es Salaam na wengine idadi kama hiyo Uwanja wa Ndege.
Matei aliishukuru Serikali ya Marekani kwa msaada huo wa kutoa utaalam kwa askari wa Tanzania ili kudhibiti uhalifu hapa nchini.
Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Virginia Blaser, alisema uzinduzi huo ni matunda ya ushirikiano wa nchi hizo mbili wa muda mrefu katika masuala mbalimbali yakiwamo ya kiuchumi.
“Program hii tunayoizindua leo (jana), ni mfano mzuri wa mafanikio tunayoyapata pale ambapo wahusika wote tunashirikiana,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment