Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amewataka Watanzania kulaani na kukemea mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kwa kuwa vitendo hivyo vinaitia aibu nchi na kuipotezea sifa yake ya amani.
Pia amekitaka Chama cha Watu wenye Ulemavu wa Ngozi Tanzania (TAS), kushawishi ili majina ya watu 16 waliohukumiwa kifo baada ya kutiwa hatiani na mahakama kwa kuhusika na mauaji ya albino, yamfikie mapema Rais Jakaya Kikwete, ili wapate
adhabu hiyo.
Lowassa aliyasema hayo wakati akihutubia mamia ya vijana walioshiriki matembezi ya hiari ya kulaani na kupinga mauaji, ukataji wa viungo pamoja na ufukuaji wa makaburi ya albino, jijini Dar es Salaam jana.
Alionekana mwenye afya njema akiwa na wabunge, madiwani pamoja na albino, walitembea umbali wa kilomita tano kuanzia Uwanja wa Taifa hadi viwanja vya TCC Club kwa miguu.
Walipita Hospitali ya Temeke, Chang’ombe Polisi na Shule ya Sekondari Kibasila kabla ya kuhitimisha matembezi hayo katika viwanja hivyo.
Akihutubia mamia vya vijana hao, Lowassa alimpongeza Rais Kikwete kwa kulivalia njuga suala hilo na uamuzi wake wa kuhakikisha inaundwa tume ya kuchunguza mauaji dhidi ya albino, akisema nao pia wana haki ya kuishi kama watu wengine.
Alisema ni wajibu wa kila Mtanzania kuliona suala hilo kama lake na kushirikiana na serikali kuwafichua wahalifu wa vitendo hivyo kwani wanatoka katikati ya jamii zao.
“Suala hili linaitia aibu nchi yetu. Hivyo, tume iliyoundwa na Rais Kikwete inapaswa kuanza kazi mara moja ili ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi waishi maisha ya furaha na amani kama watu wengine,” alisema Lowassa.
Aprili 12, mwaka huu, Rais Kikwete alinukuliwa akisema hajapelekewa majina ya watu 16 waliohukumiwa kifo kutokana na mauaji ya albino nchini kwa sababu safari ya kisheria ya majina hayo kufikishwa kwake ni ndefu.
Alisema alipozungumza katika ibada maalumu ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Liberatus Sangu kuwa Mhashamu Baba Askofu wa Jimbo la Kanisa Katoliki la Shinyanga.
Akizungumza katika ibada hiyo iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma, Ngokolo, mjini Shinyanga na mbele ya viongozi wengi wa kanisa hilo, wakiwamo maaskofu wakuu, maaskofu na maaskofu wasaidizi 38, Rais Kikwete alitumia nafasi hiyo kujibu madai kuwa serikali yake haichukui hatua za kutosha kukabiliana na mauaji ya albino na pia kufafanua juu ya shinikizo ambalo linatolewa na baadhi ya mashirika yasiyokuwa ya serikali (ngo’s) yakimtaka kutia saini ya kuruhusu watu hao wanyongwe.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, alipotafutwa jana kueleza kama majina ya watu hao 16 yamekwishapelekwa kwa Rais au la, hakupatikana na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Aidha, Lowassa aliipongeza kamati iliyoundwa na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) ya kuchunguza vyanzo vya ajali za barabarani zinazotokea kila siku.
Aliitaka serikali kuingilia kati kusaidiana nao ili kuongeza wigo wa kupata chanzo na kuokoa maisha ya Watanzania wanaofariki dunia kwa ajali.
No comments:
Post a Comment