Friday, 15 May 2015

BURUNDI BADO HALI SI SHWARI

Dar/Mashirika. Hali bado si shwari Burundi. Vituo vitano vya redio ikiwamo ya Taifa na ile ya African Public Radio (RPA) kilichokuwa kimefungwa na Serikali ya Burundi vilishambuliwa jana huku kukiwa kukiwa hakuna taarifa za uhakika za nani anayeitawala nchi hiyo kwa sasa.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Meja Jenerali Godefroid Niyombare kutangaza kumpindua Rais Pierre Nkurunziza wakati akiwa Tanzania katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa kikatiba wa Burundi.
RPA ilipigwa kombora la roketi ikielezwa kuwa askari wanaomtii Rais Nkurunziza ndiyo waliotekeleza shambulizi hilo.
Kituo hicho cha RPA kilifungwa na Serikali baada ya kuanza harakati za kumpinga Nkurunziza lakini kilianza kurusha matangazo yake juzi na usiku wa kuamkia jana kikapigwa kombora hilo.
Mbali na kituo hicho, vituo vya redio vilivyolipuliwa vinaelezwa kufanya harakati za kuipinga Serikali.
Vituo hivyo vilishambuliwa usiku wa kuamkia jana muda mfupi baada ya waandamanaji kuvamia kituo cha redio na televisheni ya Rema, vinavyohusishwa na chama tawala.
“Tunalaani mashambulizi kwa vyombo vya habari inatakiwa waandishi waachwe wafanye kazi zao,” alisema Mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Habari Burundi, Alexandre Niyungeko.
Alisema hakufahamu hasa ni nani aliyeshambulia vituo hivyo na kwamba yamefanyika wakati jeshi liliahidi ulinzi katika maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, taarifa zilizochapishwa na Gazeti la Jeune Afrique zilisema vituo vya redio vilivyolipuliwa ni vitano, viwili vikilipuliwa na polisi, kimoja na waasi wanaomuunga mkono Jenerali Niyomare na viwili vikichomwa na waandamaji.
Nkurunziza atuma ujumbe
Rais Nkurunziza alituma ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akiwataka wananchi wake kutulia kwa kuwa jeshi limezima majaribio yote ya mapinduzi.
Hata hivyo, Rais Nkurunziza ameendelea kubaki Dar es Salaam hasa baada ya kutangazwa kufungwa kwa mipaka ukiwamo Uwanja wa Ndege wa Bujumbura.
Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Burundi, Leontine Nzeyimana alithibitisha kuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza yupo Tanzania.
Nzeyimana aliyasema hayo jana akiwa katika Hoteli ya Serena ambako wakuu wa nchi za Afrika Mashariki walikutana kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa Burundi.
“Bado yupo, lakini baadaye anaweza kuondoka,” alisema kwa kifupi waziri huyo bila kubainisha eneo alipo Rais huyo.
Baadaye Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Laurent Kavakure alisema jijini Dar es Salaam kwamba Rais Nkurunziza alitarajiwa kuondoka jana kurudi nyumbani na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salvatory Rweyemamu alisema jana kwamba kiongozi huyo alishaondoka nchini.
Vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa vikiwamo vya Burundi, vimekuwa vikihoji aliko Rais Nkurunziza ambaye alielezwa kuondoka baada ya mkutano wa usuluhishi juzi na kurejea Dar es Salaam baada kushindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bujumbura.
Juzi, Meja Jenerali Niyombare alitangaza kuwa jeshi limemtimua Nkurunziza na kuunda Serikali ya mpito kuongoza nchi hiyo.
Mara baada ya taarifa hiyo, Nkurunziza hakuweza kuhudhuria mkutano Ikulu na baadaye ilielezwa kuwa anaondoka kurudi Burundi. Hata hivyo, taarifa nyingine zinaeleza kuwa alilazimika kurejea nchini kutokana na sababu za kiusalama.
Alipoulizwa jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Tanzania, Bernard Membe alisema hajui alipo kiongozi huyo akisema hataki kuzungumzia suala la alipo kiongozi huyo na kwamba viongozi wa Afrika Mashariki watakutana tena Jumatatu ya wiki ijayo kujadili hali halisi ya Burundi.
Mapigano makali Bujumbura
Kumekuwa na mapigano makali ya kurushiana risasi Bujumbura kati ya majeshi na vikundi vinavyopingana nalo na wanajeshi takriban watano wameelezwa kuuawa.
Mwandishi wa BBC, Maud Jullien alisema mapigano hayo yalikuwa yanalenga kuiteka Televisheni ya Taifa.
Wakazi wa Burundi wameamka huku wakiwa na sintofahamu kuhusu nini kinaendelea baada ya kuelezwa kuwepo kwa mapinduzi.
Usiku wa manane, Mnadhimu Mkuu wa Majeshi, Prime Niyongabo, alitangaza kwenye Redio ya Taifa kuwa mapinduzi yaliyotangazwa na Meja Jenerali Niyombare yameshindwa.
Hata hivyo, kambi ya Niyombare ilisisitiza kuwa mapinduzi yamefanyika na wanaendelea kushikilia mamlaka za Serikali ikiwamo Uwanja wa Ndege wa Bujumbura.
Majeshi yagawanyika
Mara baada ya matangazo ya mapinduzi juzi, viongozi wa Jeshi linalomtii Rais Nkurunziza walitangaza kupitia Redio ya Taifa kuwa hali iko shwari lakini mmoja wa wapinzani wa Nkurunziza aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), kwamba majeshi ya Serikali yanajaribu kupotosha.
Katika gazeti la Jeune Afrique imeripotiwa kwamba pande zinazopingana nchini Burundi juzi usiku zilisema; “Tumekubaliana kwamba usiwepo umwagaji damu ya Warundi. Sote tumeafikiana kuwa kisiwepo kipindi cha tatu – itabaki namna ya kuangalia utaratibu wa kufikia hayo.”
Wasomi wainyooshea kidole EAC
Akizungumzia hali ya machafuko hayo, Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Profesa Abdallah Safari alisema iwapo wananchi hawamtaki Nkurunziza hana budi kujitoa katika uongozi kama katiba inavyosema.
“Kisheria, haki si lazima itendeke, lakini ni lazima ionekane ikitendeka. Watu kama wanamtaka wasingeandamana, hali ingekuwa shwari,” alisema Profesa Safari.
Alionyesha wasiwasi wake kuhusu uamuzi uliotolewa na viongozi wa Afrika Mashariki na kusema wengi wanafanana na Nkurunziza na ni vigumu kuwa upande wa wananchi.
Naibu Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu wa Chuo cha Diplomasia, Dar es Salaam, Dk Kitojo Wetengere alisema mgogoro wa Burundi ni wa kujitakia kwa sababu Nkurunziza amekaidi katiba na makubaliano ya Arusha.
Alisema hata kama ana hoja zinazomwezesha kuendelea kuongoza lakini angepima joto la wananchi kuangalia hali ikoje... “Lakini katika hili, EAC ina nafasi kubwa ya kuumaliza mgogoro huu kwa sababu Burundi ni majirani zetu na pia Tanzania inaathirika kwa kupokea wakimbizi wengi.”

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Mwesiga Baregu alisema mgogoro wa Burundi umeonyesha umuhimu wa nguvu ya umma kwani jeshi lisingeweza kuipindua Serikali iwapo wananchi wasingeandamana... “Ujumbe ni kwamba, wananchi wakiamua jambo hakuna anayeweza kupinda kwa sababu hata hao wanajeshi wasingeweza kuchukua uamuzi huo bila wananchi.”

Imeandikwa na Ibrahim Bakari, Peter Elias, Florence Majani

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!