Friday 3 April 2015

WATOTO WENGINE 147 WAKUTWA MAFICHONI


WATOTO wengine 147 wamekutwa wakiwa wamehifadhiwa katika misikiti mitatu, tofauti, wilayani Hai ikiwa ni siku chache tangu watoto wengine 29 wakutwe wamefichwa mafichoni jirani na  Manispaa ya Moshi na Lyamungo Wilaya ya Hai.



Watoto hao wa kiume  wenye umri kati ya miaka 10-21 waligundulika kufichwa kwenye misikiti hiyo baada ya taarifa kutolewa za siri kwenye kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Hai.



Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika watoto hao walipatikana kutokana  operesheni iliyoendeshwa na kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo  Machi 25 hadi 27  baada ya kupata taarifa.

Watoto hao wanadaiwa kutoka mikoa mbalimbali ambapo wanadaiwa kwamba walikuwa  wakipatiwa mafunzo ya dini ya Kiislamu.

Misikiti ambayo watoto hao walikutwa ni  Masjid Bilal uliopo Mtaa wa Kibaoni,ambako walikutwa  vijana 70, Masjid Othman uliopo Mtaa wa Uzunguni  walikutwa Vijana 50 na Msikiti wa kwa Kiriwe ambako walikutwa  vijana
27.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro zinasema watoto hao walibainika kuishi na kulala ndani ya misikiti hiyo kwa madai ya kupewa mafunzo ya imani ya dini ya Kiislamu. Taarifa hizo zilieleza kuwa vituo hivyo havitambuliki kisheria.

Baadhi ya watoto waliohojiwa na makachero alikiri kukatishwa masomo katika shule walizokuwa wanasoma.  Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo imeagizwa kufungwa kwa vituo hivyo ili watoto hao warejeshwe kwao.

“Hatua ya kwanza iliyochukuliwa baada ya kupatikana kwa watoto hao  ni kufungwa kwa vituo kwa maana ya mafunzo kusitishwa hadi watakapofuata taratibu,” alisema.

Akizungumzia sakata hilo,Mkuu wa Wilaya ya Hai, Anthony Mtaka, alikiri kukutwa  kwa vijana katika misikiti hiyo,ambao walikuwa wanajifunza mafunzo ya dini na kwamba  baadhi yao walikatisha masomo.

Mtaka ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na usalama katika Wilaya hiyo,alisema vijana hao baada ya kuhojiwa walieleza kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro, Singida, Tanga, Pwani na Dar es
Salaam.

Mach 8, mwaka huu  watoto 18, wa jinsia tofauti wenye umri katika ya miaka miwili hadi 16, walikutwa wamehifadhiwa katika nyumba moja kata ya Pasua mkoani hapa na kuibua tafrani kubwa kwa wananchi wa Manispaa ya Moshi.

Mbali na watoto hao pia watoto wengine 11 wa kike wenye umri kati ya miaka 14 hadi 17, walikutwa wamehifadhiwa katika nyumba moja eneo la Lyamungo Wilaya ya Hai,Machi 11, hali ambayo imeanza kuibua wasiwasi mkubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!