Monday 6 April 2015

TUMEDHARAU MICHEZO WENZETU WANAVUNA FEDHA"



Miezi michache imebaki kabla ya Tanzania kuungana na mataifa mengine zaidi ya 50 ya Afrika kwenye michezo ya bara hili iliyopangwa kufanyika Septemba huko Kongo-Brazaville.

Pamoja na muda mfupi uliobaki kabla ya kufanyika kwa michezo hiyo ambayo huko nyuma iliwahi kuibeba nchi yetu kimataifa, tuna wasiwasi na maandalizi ambayo yamekuwa yakiendelea na kuhusisha michezo ambayo nchi yetu itawakilishwa.
Wasiwasi wetu umeongezeka zaidi baada ya wanariadha kadhaa wa Tanzania kushiriki mashindano ya mbio za nyika nchini China ambako hawakufanya vizuri. Kutofanya vizuri kwa wanariadha wetu, hata kama walikuwa wachache kiasi gani ni dalili kwamba nchi yetu lazima isubiri matokeo mabovu kwenye Michezo ya Afrika ya Kongo.
Mbali ya riadha, tunaingiwa na wasiwasi na maandalizi ya mchezo wa ndondi ambao siku za nyuma ulikuwa ukisaidia nchi yetu kupata walau medali kwenye mashindano ya kimataifa.
Kwa bahati mbaya, mara zote tumeelezwa sababu ya kufanya vibaya kwa wanamichezo wetu kuwa ni ukosefu wa maandalizi ya kutosha kabla ya michezo yenyewe au wakati mwingine kukosekana kwa mechi za majaribio.
Hata hivyo, majaribio ya wanariadha wetu kule China pamoja na kauli kama ya Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui kwamba wanamichezo wetu wanakosa lishe inayostahili, ni ushahidi mwingine wa kufanya kwetu vibaya kimataifa.
Tunajiuliza, kama hao RT ambao ndiyo wasimamizi na walezi wa riadha, bosi wake anazungumzia au kulalamikia suala la ukosefu wa lishe bora kwa wanamichezo wake je, tunategemea nini kwa wanamichezo wetu katika michezo huko Kongo?
Bila shaka, ni aibu nyingine kwa nchi yenye wakazi zaidi ya milioni 48,  ambayo inashiriki katika michezo mikubwa kama hiyo Afrika, ikirejea na medali moja au mikono mitupu.
Lakini mbali na tatizo la lishe kama alivyoeleza Nyambui, umefika wakati sasa kuangalia mipango mingine mingi ikiwamo maandalizi ya wanamichezo wetu kabla ya kujitosa kwenye michezo ya kimataifa na ikiwezekana tujitoe.
Tunadhani, kasoro ipo kwenye mipango ya muda mfupi, muda wa kati na mrefu ya michezo ambayo kwa Tanzania imekuwa tatizo sugu, tena la kudumu. Tunaelewa,  miongoni mwa sababu au visingizio vinjgi ambavyo vimekuwa vikitolewa na viongozi wetu wa shughuli za michezo ni ukosefu wa fedha au bajeti kwa ajili ya shughuli hizo.
Tunajiuliza, kama tatizo ni ufinyu wa bajeti, wizara inayosimamia masuala ya michezo inafanya kazi gani? Kwa nini iiache sekta hii iwe haina mwenyewe? Tunaamini, wizara hii kama zilivyo za mataifa mengine duniani chini ya kurugenzi au idara zake inao wajibu wa kutimiza katika kufanikisha majumu yake vinginevyo ni kuongeza ukubwa wa Serikali bila sababu.
Haiwezekani shughuli za michezo zionekane kwamba si kipaumbele wakati tunaelewa fika kwamba ikitiliwa mkazo, itaongeza ajira kitaifa na kimataifa lakini pia uwekezaji mkubwa. Tunayo mifano ya mataifa kama Nigeria.
Nchi kama Kenya, Ethiopia au hata nchi ndogo ya Eritrea, michezo, ikiwamo riadha inao uwekezaji,   inawalipa wanariadha na kuingizia nchi mapato. Tanzania inapaswa ibadilike, iige kwa wenzetu waliofanikiwa. Michezo ni fedha!

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!