Tuesday 7 April 2015

MALASUSA: WAUMINI WENGI NI WASHIRIKINA



Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Alex Malasusa akiongoza ibada ya Pasaka katika Kanisa la Azania Front, Dar es Salaam jana.(Picha na Fadhili Akida).



MATUKIO ya ukatili dhidi ya walemavu wa ngozi, vikongwe na watu wa makundi mengine ya kijamii nchini, yametajwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na hofu na kutojiamini kwa baadhi ya watu, hivyo kujikuta wakitumia nguvu za ziada kutaka kufanikisha mambo yao, badala ya kumtegemea Mungu.
Hayo yamebainishwa kwenye Ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Azania Front na Mkuu wa kanisa hilo, Askofu Dk Alex Malasusa.
Alisema hofu na kukosa uhakika ni chanzo kikubwa cha dhambi jambo ambalo linawafanya watu kuingia katika matendo ya ushirikina na mauaji ya binadamu wenzao.
“Watu wengi wamekuwa wakishiriki ushirikina na si kwamba wanapenda ushirikina, hawapendi, lakini wamejawa na hofu na hawana uhakika na ndio chanzo cha dhambi. Kumekuwapo na matukio mengi ya ushirikina ambayo si kawaida kwa binadamu aliyeumbwa na akili akayatenda."
Malasusa aliongeza: “Haijalishi umesoma kiasi gani, leo hii imethibitika wasomi wengi wameingia kwenye ushirikina, haijalishi una hali gani ya kiuchumi, wafanyabiashara wengi wamejiingiza kwenye ushirikina, haijalishi unapenda ibada kiasi gani, imethibitika tunaoingia na kutoka ibadani bado tunashiriki ushirikina.
“Ndio maana tunasikia matendo ya kusikitisha ya binadamu kwenda kuua binadamu wenzao kama albino, vikongwe kutokana na kujawa na hofu, eti wanaamini kwa kuua albino watapata fedha au mafanikio kwenye uchaguzi, huo ni uovu na akili za kishetani. Yesu aliyefufuka ndio atakayekupa mafanikio.”
Pengo na majuto ya dhambi
Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akisoma Misa ya Pasaka ambayo kitaifa imefanyika katika Kanisa la Mtakatifu Maurus Kurasini, amewataka Wakristo na jamii kwa ujumla kutokana tamaa kutokana na makosa na dhambi walizofanya na badala yake wanatakiwa kujutia makosa ili wawe huru.
“Tunaweza kuanguka hata machoni pa Yesu Kristo, au tukamkosea Mwenyezi Mungu katika jambo kubwa au dogo, isiwe sababu ya sisi kukata tamaa. Tusikate tamaa maana tutaishia mahali pabaya na badala yake tufanye kama Petro kwa kujutia makosa yetu na tusibaki ndani ya makosa. Mungu ni mwema na mwenye huruma na rehema anayeweza kutufanya kusimama bila woga, bila wasiwasi.”
Aidha, Pengo aliwataka Wakristo wakiwa wanaadhimisha sherehe za Pasaka, kuwa tayari kujutia makosa yao na kuanza upya kwa ari kubwa na kutenda matendo ya kumpendeza Mungu.
Balozi wa Papa
Katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi, Sinza, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla aliitaka jamii kuhakikisha inadumisha amani, upendo na maelewano ndani ya jamii, Bara la Afrika na dunia kwa ujumla.
Alisema kwa sasa dunia imekuwa na changamoto kadhaa ikiwamo ya baadhi ya watu kuwa tayari kupoteza uhai wao kwa kuua wenzao kwa kuamini kwa kufanya hivyo ndio wanafanya mambo sahihi.
Naye Paroko wa Parokia ya Kristo Mfalme Tabata, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Peter Shao aliwataka Wakristo kumlilia Mungu ili aweze kulisaidia taifa la Tanzania na Kanisa kwa ujumla kutokana na changamoto ambazo wanapitia sasa ikiwa ni pamoja na mchakato wa Katiba Mpya na uchaguzi mkuu.
Alisema Wakristo wanapaswa kumlilia Mungu ili kuweza kupata Katiba ambayo itatetea haki za Watanzania na pia kumpata rais atakayeendesha taifa kwa hekima, kuleta umoja na maendeleo kwa wananchi wake.
Alisema pia Wakristo wanatakiwa kumlilia Mungu kutokana familia kuwa katika hatari kutokana na mambo ambayo yanahatarisha familia kama vile dawa za kulevya, ndoa za jinsia moja na mauaji ya albino.
“ Kuna mambo ambayo yanaharibu familia…, mambo kama ya ndoa za jinsia moja ambazo ni hatari kwa kanisa na jamii, watu wenye ulemavu wa ngozi wanashambuliwa, haki zao zinachukuliwa na hatujaweza kusimama na kutetea haki zao. “Kuwakata albino viganja vya mikono kwa imani za kishirikina ni matokeo ya dhambi za mwanadamu, hivyo tunahitaji kumlilia Mungu ili afanye jambo kwa nchi na kanisa.”

HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!