Monday, 23 March 2015
WASIOLIPA ADA ZA ARDHI KUKIONA!
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi, ameagiza halmashauri zote nchini kutoa notisi ya kufuta hati za wamiliki wote wasiolipa ada za ardhi kwenye maeneo yenye migogoro ya ardhi ambayo haiendelezwi kisheria.
Amesema hayo mjini Babati jana katika ziara yake ya kutembelea mkoa huo, ambapo aliagiza uongozi wa mkoa huo kuhakikisha unatenga maeneo ya akiba na kuchukua hatua kwa watu wanaochukua ardhi ya kijiji kwa madai ya kulima na kufuga na hatimaye kuishia kupata hati za kupata mikopo katika taasisi za fedha pasipo kuyaendeleza.
Alisema malalamiko yote ya mashamba ambayo hayatumiki na kuendelezwa yanapaswa halmashauri husika kuyatathmini na kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuyagawa kwa wananchi ili waweze kuyatumia na wao kuwa wasimamizi wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yao.
“Nimeelekeza maeneo yote yenye migogoro ya ardhi ambayo hayaendelezwi wala kulipiwa ada za ardhi na kufanywa kama biashara halmashauri zitoe notisi za kufuta hati zao na kuchukua ardhi hiyo na kuweka akiba, hii ni kazi ya halmashauri, kwani kuwa na shamba sio kosa bali kutoendeleza ni kosa,” alisema.
Alisema mkoa wa Manyara umekithiri kwa migogoro ya ardhi ambapo baadhi ya migogoro hiyo imekuwa ikisababishwa na baadhi ya wataalamu wa ardhi na kuutaka uongozi wa mkoa chini ya Mkuu wa Mkoa huo Dk Joel Bendera kuishughulikia na kutoa taarifa wizarani ifikapo Mei mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment