Sunday, 22 March 2015

WAPINZANI WAMUONE KINANA KAMA OKWI ANAYEPIGA MASHUTI"

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Abdulrahman Kinana ameishika nafasi hiyo tangu Novemba 2012. Kuanzia hapo hajapumzika wala kulala usingizi.

Anatembelea mikoa yote na kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Ni nadra kukosa habari za Kinana kwenye vyombo vya habari nchini, mara leo yuko Mbeya, yuko Dodoma, yuko Tanga, yuko….
Yupo kila siku na yupo katika kila eneo, anapokwenda haachi kufukua mawe yaliyoota mizizi na kisha kuyapindua na kuyageuza, anasema, anaelekeza, anakemea na anapongeza.
Amejielekeza kama ni mtu huru, yuko kote kote, kwa wananchi na kwa chama, anauma na kupuliza. Hasiti kuikosoa Serikali pale anapoona imekwenda mrama, analia kilio cha wananchi bila kujali kama yeye ni mtendaji mkuu wa chama kinachoongoza Serikali.
Anachofanya ni kukisafisha chama mbele ya macho ya wananchi, kazi hiyo amekuwa akiifanya kwa takriban miaka mitatu sasa.
Utamkuta vijijini akishirikiana na wananchi kujenga, kulima na hata kuhamasisha. Hivi sasa anawahamasisha wananchi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura na kisha kushiriki katika kupiga Kura ya Maoni.
Yuko ‘bize’, hashughulishwi na yasemwayo dhidi yake wala dhidi ya chama chake, ilimradi yeye anajua akitendacho.
Mchambuzi mmoja wa masuala ya kisiasa alimfananisha Kinana na Karl Rove, gwiji la mikakati ya siasa wa Marekani. Kama Rove, Kinana ni bingwa wa stratejia na ni zaidi ya meneja wa kampeni.
Mwaka 2005 alikuwa meneja wa kampeni wa Jakaya Kikwete na alifanikiwa kumuingiza madarakani. Mwaka 2010 alihakikisha kuwa Rais Kikwete anaendelea kubaki madarakani.
Kuanzia mwaka 2012, Kinana amekuwa akifanya kazi ya kukiimarisha chama na kufufua matumaini ya wanachama. Ndiyo maana anazunguka nchi nzima kuwa karibu na wananchi. Wananchi wanamuona yeye na wanamsikia yeye, huyu ni mwenzao, anayezungumza lugha yao, lakini anacho anachokiwakilisha na kukiwasilisha.
Wakati vyama vingine (vya siasa nchini) vinafanya kampeni za kushtukiza na za zimamoto, Kinana ana stratejia makini kwa chama chake, hajawahi kupumzika, anapita kila penye pori na nyika, anatifua. Vyama hivi vitakapojikita katika kampeni za uchaguzi katikati ya mwaka huu, CCM zamani imemaliza kupiga kampeni, sasa itakachofanya ni kumnadi mgombea wake tu, kwani tayari Kinana ameshafanya kazi ya awali.
Mengine anayoyazungumza dhidi ya Serikali yake, yanatia shaka, hee, anaibomoa Serikali inayoongozwa na chama chake? Watu wanaulizana, lakini wasichokijua ni kuwa Kinana anaijenga Serikali ijayo.
Anakemea rushwa na viongozi wabovu, anashangazwa na ubovu wa huduma vijijini, anajifanya haelewi kwanini mpaka sasa maji safi na salama hayapatikani. Hatambui kwanini huduma za afya vijijini bado duni, anataka kuonyesha kwamba wananchi kupata huduma bora ndiyo kipaumbele cha CCM, lakini tatizo ni ubinafsi wa baadhi ya viongozi waliopo serikalini.
Anachofanya ni kuwaonyesha wananchi kama kwamba kinachofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali, CCM haijakibariki wala haikipendi, hivyo CCM haihusiki kwa sababu haijawatuma.
Anaendelea kuikita mizizi ya CCM mashinani, yeye hana habari na kilele kwa sababu anajua kuwa akiimarisha mizizi kwa kuimwagilia maji, kuiwekea mbolea na kuipalilia, bila shaka kilele kitanawiri. Wakati vyama vya upinzani vikijikita mijini na katika baadhi ya mikoa, CCM haichagui, iko kila pembe ya Tanzania, hawa kweli wanakusudia kufanya biashara.
Pamoja na ukweli kwamba vyama vya upinzani viliongeza ushawishi wake wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, lakini bado CCM imefika ambako vyama vya upinzani havijafika bado.
Katika baadhi ya vijiji nchini, wananchi wanawaona wapinzani kama ‘wahuni’ tu, na ukiwauliza kama upinzani upo watakwambia kuwa ‘wapo wahuni wachache’ wanaotukorofisha kidogo.’
Si ajabu pia kama utafanya utafiti kwa kuuliza swali kama uchaguzi utafanyika leo, wewe utachagua chama gani, wakakujibu: “Chama cha Mwalimu Nyerere.”
Wakati wa kampeni za uchaguzi uliomuingiza George W. Bush madarakani mwaka 2001, Karl Rove alitumia ‘Grassroots Political Strategy.’ Kwa tafsiri si-si-si, grass ni majani na roots ni mizizi. Hivyo huo ni mkakati wa chini kabisa kuanzia kwenye mizizi inayootesha majani.
Kamusi ya Tuki, imeitafsiri roots kama umma. Hivyo anachofanya Katibu Mkuu wa CCM ni kwenda kwenye mizizi ya umma, mwanzo kabisa na kutengeneza msingi kwa kuuwekea zege ili uwe madhubuti.
Kwa kweli Kinana hata akipigwa madongo hayamfiki kwa sababu ametengeneza staili ya kuyakwepa, yeye hajibu mapigo kwa mdomo, bali anafanya mambo kwa vitendo.
Huyo ndiye mwana-stratejia Kinana anayeyaendea majimbo yote ya uchaguzi, hata kabla ya uchaguzi, anaeleza dhamira, mipango na mikakati ya chama chake, anakipeleka chama kwa wananchi, je, wale wanaopiga kelele juu, wanayo nafasi?
Operesheni Sangara, Operesheni Vuguvugu la Mabadiliko (Movement For Change - M4C), Operesheni Pamoja Daima, Operesheni Zinduka, Operesheni Mchakamchaka na nyingine nyingi, ni operesheni za maji moto, zinaunguza kwa muda lakini hii operesheni ya kuijenga CCM kuanzia mashinani ni maandalizi ya muda mrefu na mazuri ya kushinda Uchaguzi Mkuu. Wapinzani wanapaswa wamuone Kinana kama Okwi anapiga mashuti na kufunga goli.
NA HAWRA SHAMTE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!