Afisa mawasiliano mwandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bw. Andrew Singu akimpima uzito na urefu mmoja wa wahudhuriaji wa mkutano wa mwaka wa wahasibu waandamizi unaofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere,jijini Dar es salaam.
………………………………………………………
Na Mwandishi wetu- Dar es Salaam
WADAU wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wameuomba Mfuko huo kuendeleza programu za upimaji wa afya bure ili kuwasaidia wanachama wake na wananchi kwa ujumla kujua hali za afya zao lakini pia kuepekana na maradhi yasiyoambukiza.
Hayo wameyasema Dar es Salaam jana katika mkutano wa Wahasibu Waandamizi wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, unaofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu J.K.Nyerere ambapo NHIF ilishiriki kwa kuwa na banda la elimu kwa umma na upimaji wa afya bure uliokwenda sambamba na utoaji wa elimu ya namna ya kujikinga na maradhi yasiyoambukiza kama moyo na mengine.
Pamoja na ombi hilo, NHIF imekuwa ikiendesha upimaji katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa lengo la kuwasaidia wananchi kufahamu afya zao lakini pia kuwapa ushauri wa namna ya kujikinga na maradhi hayo ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi na matibabu yake ni ya ghari.
Katika mkutano huo ambao ulikuwa na jumla ya washiriki 800 ambapo jumla ya washiriki 600 walipima afya zao , idadi ya wanawake ikiwa ni 350 na wanaume 250.
Katika dawati la elimu kwa umma ililitolewa elimu ya umuhimu wa kujiunga na NHIF, haki na wajibu kwa mwanachama wa NHIF wakati wa kupata huduma.
Wakizungumza katika banda la Mfuko washiriki wa mkutano huo walisema huduma zinazotolewa na Mfuko ni nzuri na ni za kuigwa kwa kuwa zimelenga kuelimisha jamii umuhimu wa kupima afya kabla ya kuugua hasa katika kipindi hiki ambapo gharama za matibabu zimekuwa ni kubwa.
Akitoa ushauri wa jumla kwa washiriki hao, Ofisa Udhibiti Ubora wa NHIF, Dk. Raphael Mallaba, alisema kuwa ni vyema wakawa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara hali itakayowasaidia kujitambua kutokana na ukweli kwamba magonjwa haya kwa sasa yanaongezeka na matibabu yake ni ya ghari.
Alisema kuwa magonjwa haya yanasababishwa na hali halisi ya maisha iliyopo sasa hivyo ni vyema mkakati wa kufuatilia afya ukawa kwa kila mtu kwa kuwa bila kuwa na afya njema hata maendeleo ya jamii zetu zitayumba
No comments:
Post a Comment