Sunday 15 March 2015

UCHAKAVU WA MABASI CHANZO CHA AJALI NYINGI BARABARANI


ILI huduma ya usafirishaji wa abiria iweze kufanikiwa ni lazima wadau wa usafirishaji wafuate haki za watumiaji wa huduma za usafiri wa nchikavu na majini kwa mujibu wa kanuni za usafirishaji za mwaka 2007. 


Pia wawe na ajenda moja ambayo kwa namna moja ama nyingine itaweza kupanua wigo na kutoa tija kwa abiria sanjari na kukuza soko la ushindani ndani na nje ya nchi.
Huduma ya usafirishaji ambayo ndiyo huduma mama na endapo busara haitotumika kwa umakini kila siku itakuwa ni shida na lawama na kutoweza kupatikana kwa ufumbuzi wa kudumu.
Tatizo linalochangia kuendelea kuwepo kwa huduma isiyoridhisha ya usafiri ni wengi kuishi katika mfumo wa kimazoea yaani kutofuata sheria za usafirishaji nchini kama kuingiza gari barabarani likiwa bovu.
Pamoja na kuwepo kwa hali hiyo pia suala la rushwa ndogo ndogo ni kati ya sababu inayochangia huduma ya usafirishaji abiria kutofuata sheria.
Ingawa sheria na taratibu zipo wazi katika sekta hiyo lakini kwa kuwa hakuna mtu anayehoji au kuzifuatilia sheria wala taratibu hizo imechangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa uvunjwaji wa sheria za barabarani kutokana na kila mmoja kufanya vile anavyojua.
Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri Majini na Nchikavu (SUMATRA), kanda ya Mashariki Konrad Shio anasema kuwa licha ya changamoto ambazo zimekuwa zikionekana moja kwa moja kwa wamiliki wa mabasi hapa nchini lakini bado abiria nao wamekuwa na udhaifu katika sekta hiyo.
Anasema kuwa abiria wanatakiwa kufahamu haki zao kama basi analopanda ikiwemo kudai tiketi ya fedha halali anazolipa ikiwa ni nauli ya sehemu husika na ni jukumu la mmiliki kuhakikisha tiketi inapatikana kulingana na nauli iliyotolewa.
"Tatizo kuna mfumo kwa baadhi ya abiria kuishi na kufanya safari kimazoea pindi wanaposafiri jambo ambalo bado linatuletea changamoto kubwa katika utendaji kazi wetu wa kila siku sisi kama mamlaka kwani utakuta abiria hawana tiketi ya basi husika bado wengine wakishabikia mwendokasi wa basi," anasema Shio.
Anasema kuwa ili ajali za barabarani ziweze kupungua hapa nchini ni pamoja na abiria kuacha ushabiki katika mabasi ambayo wamekuwa wakipanda kwani jambo hilo humchochea dereva kuendesha mithili yupo kwenye mashindano.
Anasema kuwa asilimia 85 ya ajali ambazo zimekuwa zikitokea barabarani kila mara ni pamoja na mapungufu mbalimbali huku asilimia inayobaki ni kutokana na matatizo mbalimbali ya kiufundi.
Kwa upande wake mmoja wa wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani, Joyce Camiliius anasema kuwa sekta ya usafirishaji inatakiwa kuangalia upya pamoja na kuboreshwa zaidi ili kuwa na ufanisi zaidi.
Anasema kuwa kama inawezekana serikali iwe wabia katika sekta hiyo ili kuweza kuiboresha na kuleta tija kwa taifa na kutoonekana ya mtu mmoja mmoja.
"Serikali iseme kuwa wamiliki wajiunge kwa pamoja na kufahamika na Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) ili tuweze kutambulika na kuweza kutukopesha na mwishowe tuwe na mabasi ya kisasa zaidi ambayo yataweza kutoa huduma nzuri hapa nchini," anasema.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani Mohammed Abdullah (TABOA), anasema kuwa biashara ya usafirishaji ni muhimu kuliko mambo mengine hivyo umakini mkubwa unatakiwa ili kuweza kuboresha sekta hii.
"Nieleweke kuwa kila jambo linahitaji uangalifu wa aina yake na ushindani upo kila siku hivyo jambo hili litazamwe upya kadri siku zinavyokwenda ili liweze kuonekana lina mafanikio makubwa kwa taifa na hata kwa nchi kwa ujumla," anasema Abdullah.
Abdullah anafafanua kwa kina kuwa miongoni mwa sababu ya kufanya sekta hii ianze kurudi nyuma ni kutokana na sera ya usafirishaji kutotiliwa mkazo na kusaidia wamiliki kupata fursa ya kuongeza mabasi yanayokidhi mahitaji ya wateja wao.
Anasema kuwa endapo Serikali itaandaa mkakati wa sera ya sekta ya usafiri ina uwezo wa kuleta tija na kuwafanya wamiliki wa mabasi kununua mabasi mapya yasiyokaa kwa miaka mingi.
Abdullah anasema kuwa kama serikali endapo itafikiria hatua ya kuondoa Ongezeko la Thamani (VAT) ingewawezesha wamiliki walio wengi kununua mabasi ambayo ni mapya na yanayoendana na wakati.
Anasema kuwa mabasi mengi yasiyokidhi kiwango nchini yanatokana na kitendo cha serikali kuweka ushuru huo sanjari na ongezeko la thamani linalofanya wamiliki kuendelea kuwa na magari yasiyokidhi viwango.
"Sheria za nchi zipo wazi kuwa basi ambalo lina umri zaidi ya miaka 10 haliruhusiwi kufanya kazi ya usafirishaji wa abiria lakini kutokana na uwepo wa ushuru kumesababisha walio wengi kushindwa kumudu gharama hizo za uendeshaji," anasema.
Anasema kuwa nchi jirani kama Kenya ilifikiria kwa undani zoezi hilo la uondoaji wa ushuru katika mabasi na kwa maana nyingine wameweza kupiga hatua katika nyanja ya usafirishaji kwa kuwepo kwa mabasi yenye kukidhi viwango na yenye kutoa huduma bora.
"Kwa maana nyingine ni kuwa kama ushuru huo ungeondolewa kama ilivyo kwa nchi jirani ya Kenya umri wa mabasi ya kusafirisha abiria ungepungua hadi kufikia miaka saba au nane tofauti ilivyo hivi sasa ambapo kuna baadhi ya mabasi yana umri hadi miaka 18, ambapo wamiliki wanafanya kuyakarabati kwa kupaka rangi na kuonekana mapya," anasema Abdullah.
Anasema kuwa serikali inatakiwa iangalie upya sera ya usafirishaji ili iweze kuwa na tija kwa pande zote mbili yaani kwa mmiliki na abiria ili kuifanya biashara hiyo kuwa ya kiushindani zaidi kwa ndani na nje ya nchi.
Pia mwenyekiti huyo anapendekeza mabasi kutopita katika mizani pindi yawapo safarini kwa sababu kuwa uzito wa abiria na wa basi unajulikana hivyo hakuna haja ya kupima kama magari ya mizigo.
Anasema kuwa endapo kama kuna mabasi yanayokiuka sheria adhabu kali ziwe zinatozwa ili iwe fundisho kwa wasafirishaji wengine wenye mchezo huo wa kuharibu miundombinu ya nchi.
Sera ya usafirishaji ni miongoni mwa jambo lingine ambalo linatakiwa iruhusu mabasi kufanya safari zake saa 24 ili kupunguza ajali msongamano na vurugu nyinginezo ambazo hazina msingi.
"Mabasi yanatembea saa 12 tu sasa likitokea Dar es Salaam kwenda Kagera na kama likitoka kwa kuchelewa ni lazima dereva akimbize basi ili ahakikishe kuwa usiku haumkuti barabarani lakini vipi kwa watakaosafiri masaa 3,4 hadi 5? alihoji Abdullah.
Enea Mrutu ni Katibu wa chama cha wamiliki wa mabasi nchini TABOA, anasema kinachotakiwa hivi sasa katika sera ya usafirishaji ni kuhakikisha siasa haziingilii sekta ya usafirishaji na kuacha inajitegemea yenyewe.
Anasema kuwa TABOA imekuwa ikikubaliana mambo mbalimbali lakini siasa zimekuwa zikipenyezwa ndani yake na kusababisha kushindwa kufikia malengo husika katika usafirishaji.
"Kama chama tunakubaliana mambo mbalimbali lakini tatizo kuna harufu ya siasa ndani yake na ndiyo maana malengo yanaweza kuchelewa au kutimia kwa kusuasua katika kuboresha sekta hii," anasema Mrutu.
Hata hivyo anapendekeza kwa wasafirishaji kufuata taratibu zote za usafirishaji ili kufanya biashara ya ushindani ambayo inaendana na uhalisia wa soko hivi sasa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!