Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk Seif Rashidi, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Donan Mmbando alisema takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa mwaka 2013 wagonjwa wa Kifua Kikuu 65,000 waligunduliwa.
Alizitaja aina mbili za Kifua kikuu ikiwamo cha mapafu ambacho hushambulia mapafu pekee na cha nje ya mapafu, huku akibainisha kuwa cha mapafu ndiyo kinaongoza hapa nchini.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za kawaida zinazopatikana kutoka katika vituo vya kutolewa huduma za afya , zinaonyesha kuwa maambukizi mapya yanatokea miongoni mwa rika la vijana wenye umri kati ya miaka 25 na 44, kama ilivyo Virusi Vya Ukimwi.
“Kifua Kikuu ni tatizo na kinashambulia zaidi vijana ambao ndiyo tegemeo la taifa hili, hivyo kudhoofisha uchumi wa nchi, hivyo wizara ili kunusuru kizazi hicho inaongeza juhudi za kuhakikisha inatokomeza kama siyo kukimaliza kabisa, alisema Mmbando.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), kati ya watu milioni tisa wanaougua ugonjwa huo duniani kwa mwaka, theluthi moja ya hao hawatambuliki katika mifumo ya sekta ya afya, huku sehemu ya hao milioni tatu wanaishi katika nchi masikini ikiwamo Tanzania.
Alisema kwa Tanzania watu wanaoshambuliwa zaidi na ugonjwa huo ni katika makundi maalumu kama vile watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi, watoto, wazee, wafungwa na watu wenye magonjwa ya muda mrefu kama saratani na kisukari.
Meneja Mipango wa Wizara hiyo Dk. Beatrice Mutayoba alisema kuwa pamoja na juhudi zinazofanywa kudhibiti ugonjwa huo bado ni tatizo kwa jamii na kila mwaka wagonjwa wapatao 63, 000 hugundulika. Huku Mikoa kama Dar es Salaam, Mwanza, Shinyanga, Mbeya, Morogoro, Mara, Arusha na Tanga ikiongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi.
“Hadi sasa kuna changamoto wa kuwabaini wagonjwa wa kifua kikuu, kwani kati ya wagonjwa 65,732 waliobainika katika takwimu za Kitaifa za kubaini wagonjwa zilizofanyika mwaka 2012, sawa na asilimia 54 pekee huku wagonjwa 56,000 hukosa kugundulika na kupata matibabu hivyo kuendelea kuwaambukiza wengine, ”alisema Dk. Mutayoba.
Dk Mutayoba pia aliwataka wananchi kutodharau kifua cha aina yoyote kwa sababu hakuna kifua cha kawaida, hivyo kila anayekohoa anahitaji kupata ushauri wa daktari na vipimo.
“Kifua siyo ugonjwa wa kurithi, kinaambukizwa, kina tiba na kinapona kabisa, hivyo kila anayekohoa anahitaji kupata tiba na vipimo sahihi badala ya kuona ni cha kawaida, ”alisema Mutayoba.
HABARI LEO.
No comments:
Post a Comment