Rais Jakaya Kikwete, amesema siku chache zijazo mizigo inayosafirishwa kwenda nchi za Afrika Mashariki na Kati kutoka Bandari ya Dar es Salaam, itabebwa kwa treni na kusafirishwa kwa reli na kuachana na usafirishaji mizigo kwa malori.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa treni za mizigo kwenda nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Uganda, Burundi na Rwanda, alisema kwa sasa mizigo itasafirishwa kuanzia makao makuu ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kwenda nchi husika.
Alisema kwa sasa wataalamu wa TRL wamebuni utaratibu mzuri wa mabehewa yanayotoka nchi moja kwenda nyingine moja kwa moja tofauti na utaratibu wa awali wa kukata bogi ili kushusha mizigo.
"Pamoja na treni za nje ya nchi, lakini kutakuwa na treni za kubeba mizigo ya ndani...utaratibu huu utapunguza ucheleweshaji wa mizigo uliokuwapo, hivyo nchi zenye bandari kuona kama adhabu kusafirisha mizigo kupitia Tanzania," alisema.
Rais Kikwete alisema mkutano uliowaleta pamoja marais wa nchi za Afrika Mashariki na Kati una lengo la kuimarisha miundombinu ya barabara, reli na bandari ili Tanzania itimize wajibu wake wa kuzisaidia nchi zisizo na bahari.
Mathalani, Rais alieleza kuwa alikwenda Burundi na kuzungumza na wafanyabiashara ambao kilio chao kikubwa kilikuwa ni ucheleweshaji wa mizigo unaoanzia bandarini na vikwazo vingine zikiwamo barabarani kiasi cha nchi hiyo kujilaumu kupakana na Tanzania.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, alisema kwa sasa inachukua siku mbili kwa mizigo kufika Kigoma kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Burundi, DRC na Rwanda na kwamba kwa sasa kutakuwa na mabehewa kati ya 15 na 20 kwa kila safari.
Alisema mizigo ya kwenda Rwanda itashushwa Bandari Kavu ya Isaka na ya Uganda itashushwa feri ya Mwanza na kuvushwa kwa meli kwa haraka.
"Utaratibu huu ni endelevu, utakuwa kila mfanyabiashara atafuatilia mzigo wake ulipo na atapata kwa muda mfupi...tunawashukuru mafundi wa Tanzania na Malaysia ambao wamezifufua Injini za miaka 40 iliyopita kufanya kazi upya," alisema.
Rais wa Burundi, Pierre Nkrunzinza, aliishukuru Tanzania kwa jitihada za kuisaidia nchi hiyo katika masuala ya kupata Uhuru, kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe na sasa kuwa na amani ya kudumu.
Alisema wakati wa vita Warundi milioni moja walipata hifadhi ya muda Tanzania na kwamba kwa sasa wanazisaidia nchi zenye vita zikiwamo Afrika ya Kati na Sudan Kusini.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment