Serikali imewasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi ya mwaka 2014 huku Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ikiponda watendaji wa serikali kutumia fedha za Ukimwi katika makongamano badala ya fedha hizo kuelekezwa katika kuwapatia lishe watu walioathirika na Virusi vya Ukimwi (VVU).
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), Rajab Mohamed Mbarouk, alisema kumekuwa na kilio cha muda mrefu kwa watendaji wa serikali kutumia fedha za Ukimwi kulipana posho kwenye vikao badala ya kuzitumia katika malengo yaliyokusudiwa.
Alisema maambukizi ya Ukimwi yamepungua kutoka asilimia saba mwaka 2003/2004 hadi asilimia 5.3 kwa Mwaka 2011/2012 ingawa kupungua huko siyo kwa kiwango kilichotakiwa kutokana na serikali kutoonyesha umakini kikabiliana na tatizo hilo.
Mbarouk alisema katika miaka yote wanawake wamekuwa na maambukizi zaidi kuliko wanaume na asilimia 85 ya wajawazito wanaopimwa na kugundulika na maambukizi hupatiwa dawa za kinga kwa watoto na wao hutumia dawa ya kupunguza makali ya maambukizi ya Ukimwi (ARVs).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenister Mhagama (pichani), akiwasilisha muswada huo alisema serikali itaanzisha mfuko wa Ukimwi kwa lengo la kuwajengea uwezo wananchi wazalendo kuanza kuchangia masuala yanayohusu afya zao.
Mhagama alisema gharama ya kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2013 hadi 2018 ni Sh. bilioni 5,119.6 na kuna upungufu wa Sh. bilioni 300 kila mwaka.
Alisema ili kuhakikisha mfuko unaopendekezwa unanufaisha wananchi, serikali itazingatia mifano ya Zimbabwe na Afrika kusini ambazo zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza suala hilo.
Naye Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, alisema serikali imeridhia kuanzishwa kwa mfuko huko japo bado kuna mazungumzo na wataalamu ili kuainisha vyanzo vya mapato ya mfuko huo.
Malima alisema Canada na Denmark zimekuwa zikichangia takribani Sh. bilioni 17 kwa mwaka, lakini hivi sasa Canada imejitoa kuchangia huku Denmark ikitarajia kujitoa mwakani.
Hata hivyo, Glob Fund wamekubali kutoa Dola za Marekani milioni 280 kwa miezi 18 ambazo mfuko umetoa masharti kuwa kati ya hizo asilimia 80 zitatumika kununulia dawa.
Mbunge wa Viti Maalum, Diana Chilolo, alisema hakuna umakini wa serikali katika kupambana na Ukimwi kutokana na kuchangia kiasi kidogo cha asilimia tatu tu huku asilimia 97 zikitolewa na wahisani.
Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Mchungaji Luckison Mwanjale, alisema serikali ianzishe mfumo wa ukimwi kwani kuendelea kuwategemea wahisani ni hatari kwani siku wakisitisha misaada hali itakuwa mbaya.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Maria Hewa, alisema ili kuweza kukabiliana na tatizo la Ukimwi na kuwa uundwaji wa mfumo wa Ukimwi yasiwe maneno tu bila utekelezaji kutokana na wahisani kujitoa
No comments:
Post a Comment