Wednesday, 25 March 2015

MBARONI WAKIDAIWA KUUZA MIFUPA YA ALBINO MIL 3



Jeshi la Polisi mkoani Kagera,  limewatia mbaroni watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na mifupa ya viungo vya mwanamke mwenye ulemavu wa ngozi 
(albino), Zeulia Justus, aliyefariki dunia mwaka 2006 baada ya kujifungua mtoto katika kijiji cha Rushwa Kata Mshabago Tarafa ya Nshamba Wilaya ya 
Muleba, mkoani Kagera.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni James Lutozi (66) na Emmanuel Karoli (50), wakazi wa 
Kijiji cha Kyota Tarafa Kimwani wilayani humo.
Mwaibambe alisema kuwa  watuhumiwa hao walikamatwa na mifupa mitatu ya mwanamke huyo   baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kijijini 
humo kuwa kuna watu wanauza viungo vya  albino kwa Sh. milioni tatu.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Machi 20, mwaka huu, wakiwa na mfupa mmoja na walipopekuliwa kwenye makazi yao, walikutwa na mifupa 
mingine miwili. 
“Katika mahojiano, watuhumiwa hawa walikiri kwamba, mifupa hiyo ni ya albino aliyefariki mwaka 2006 katika Kijiji cha Rushwa, Kata Mshabago, 
Tarafa Nshamba, wilayani Muleba,” alisema Kamanda Mwaibambe.
Alisema watuhumiwa hao walidai kuwa mifupa hiyo waliipata baada ya kufukua kaburi alimozikwa albino huyo mwaka 2008 kwa maelekezo ya mganga 
wa jadi, Mutalemwa Revocatus.
Mwaibambe alisema polisi waliiomba mahakama mkoani hapa kibali cha kufukua kaburi na kupewa.
Alisema polisi walikwenda kwenye kaburi hilo Machi 23, mwaka huu na kulifukua na kujiridhisha kuwa mifupa hiyo ilikuwa ni ya viungo vya albino 
huyo.
Mwaibambe alisema polisi wanamsaka mganga huyo kwa tuhuma za kuwashawishi watuhumiwa kufukua kaburi la albino huyo na kuchukua mifupa ya 
viungo vyake.
Aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa atakayemuona kwa kutoa taarifa polisi ili mganga huyo akamatwe na kufikishwa mahakamani kujibu 
mashtaka.
Alisema atakayetoa taarifa na kuwezesha kukamatwa kwa mganga huyo, jeshi hilo litampa zawadi nono.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!