Saturday, 21 March 2015
MAZUNGUMZO YA MAGARI YA KENYA NA TANZANIA YAVUNJIKA
MAZUNGUMZO ya Watendaji na Mawaziri wa Tanzania na Kenya kuhusu kuzuiwa kwa magari ya kitalii ya Tanzania kuingia katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, yamevunjika.
Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amewataka watalii wanaoingia Tanzania kutumia ndege zinazotua moja kwa moja Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) mpaka hapo maelewano baina ya nchi hizo mbili, yatakapofikiwa.
Nyalandu alisema hayo jana jijini Arusha, baada ya kuvunjika kwa kikao cha mazungumzo hayo, ambacho kilishirikisha wataalamu wa wizara za utalii, Afrika Mashariki na viwanda na biashara za nchi hizo.
“Sisi mawaziri wa nchi hizi tuliagiza yajadiliwe mambo yote yaliyosababisha zuio hilo, kabla hayajafika kwetu, lakini kikao kikawa kigumu kukubaliana ajenda moja tu kuhusu kwa nini Jamhuri ya Kenya, walizuia magari ya Tanzania wakati hawajawahi kubadilisha makubaliano hayo,” alisema.
Moja ya makubaliano ya Mkataba wa mwaka 1985 kwa mujibu wa Nyalandu, nchi hizo zilikubaliana kudumisha ushirikiano katika biashara ya utalii na waliweka bayana kuwa magari yote ya Kenya, yataruhusiwa katika mipaka iliyo wazi Tanzania na kupeleka watalii Arusha, Musoma, Moshi na Tanga.
Pia Nyalandu alisema, walikubaliana magari ya Tanzania yanayopeleka wageni Kenya, yataruhusiwa kuingia katika miji yote ya Jamhuri ya Kenya na makubaliano hayo hayajawahi kubatilishwa.
Baada ya kutokea tatizo hilo, Nyalandu alisema mawaziri waliagizwa kikao kifanyike Tanzania Machi 19 na kushirikisha wataalamu wa wizara hizo, ili wajadiliane sababu ya zuio hilo na ajenda ilikuwa hiyo tu, wakati hawajawahi kubadilisha mkataba huo na matokeo yake kikao kilivunjika.
Nyalandu alisema kikao kilivunjika kwa sababu kila upande ulivutia kwake; Tanzania ikitaka kuelezwa sababu ya zuio hilo, huku Kenya wakisema hilo siyo la muhimu kwao, bali la muhimu ni kufanya marekebisho ya mkataba uliopo wa masuala ya utalii wa mwaka 1985.
“Makatibu wangu (kutoka Tanzania) walitaka ajenda kuu katika kikao hicho iwe zuio la magari ya Tanzania kuingia uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na wao hawakutaka, wakataka ajenda ya kuongelea marekebisho au maboresho ya mkataba aambao haujawahi kuvunjwa wala kurekebishwa tangu mwaka 1985,” alisema.
Alisema baada ya sintofahamu hiyo kikao kilivunjika na kesho yake (Jana) ilitakiwa kikao cha mawaziri kifanyike nacho hakikufanyika kwa ajili ya sintofahamu hiyo.
Mgogoro huo ulitokea Desemba 22 mwaka jana, mara baada ya Kenya kuzuia magari ya utalii ya Tanzania kuingia uwanja huo wa Kenyatta na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watalii wa Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment