Saturday, 14 March 2015

MAMA, MWANAYE JELA MIAKA 30 KWA UBAKAJI


MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma, imewahukumu kifungo cha miaka 30 jela Bw. Sagimembe Mroso na mama yake Bi. Regena Kigelulye wote wakazi wa Mtaa wa Hazina, mjini humo kwa kosa la ubakaji.



Washtakiwa hao wanadaiwa kufanya tukio hilo Machi 6, mwaka huu, katika mtaa huo ambapo Bi. Kigelulye anadaiwa kumsaidia mwanaye Bw. Mroso ili kufanikisha ubakaji.

Hukumu hiyo imetolewa jana ambapo Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Paskal Mayumba baada ya kusikiliza maelezo ya Mwendesha Mashtaka, Bw. Godwin Ikema alisema Mroso alitenda kosa hilo kinyume na kanuni ya adhabu.

Alisema mahakama imejiridhisha kuwa, mshtakiwa wa pili, Bi. Kigelulwe, alimsaidia mwanaye Mroso kufunga mlango kwa nje ili mbakwaji (jina linahifadhiwa), asiweze kutoka.

Aliongeza kuwa, siku ya tukio Bi. Kigelulye ambaye ni nesi katika Hospitali ya Benjamini Mkapa, alimchukua mbakwaji aliyekuwa akimuuguza baba yake hospitalini hapo kwenda kulala naye nyumbani kwake.

Wakiwa ndani ya nyumba hiyo, Bi. Kigelulye alifunga mlango kwa nje ili mwanaye aweze kumbaka akimsihi kuwa yeye ni mtu mzima hivyo hapaswi kupiga kelele.

Akiendelea kusoma maelezo ya kesi hiyo, Hakimu Mayumba alisema baada ya majirani kusikia kelele za mbakwaji, mshtakiwa wa pili Bi. Kigelulye aliwaambia kuwa mama huyo alitoka kijijini hivyo alikuwa anaogopa alipowaona katika televisheni.

Hata hivyo, mlango huo ulifunguliwa kwa nje ambapo Bi.Kigelulye alimtaka mwanaye amsindikize hospitalini lakini walipofika eneo la Korongoni, alianza kumbaka tena.

"Kumbukumbu zinaonesha mshtakiwa Mroso anaishi na virusi vya UKIMWI na alifanya kosa hilo bila kutumia kinga, uongozi wa hospitali ulimpa kinga ambayo hadi mbakwaji amepimwa mara kadhaa lakini hana virusi hivyo.

"Baada ya tukio hilo, mbakwaji alifukuzwa nyumbani na mumewe ambapo mgonjwa wake (baba yake mzazi), naye alifariki dunia hivyo kwa sasa ameathirika kisaikolojia," alisema Hakimu Mayumba.

Aliongeza kuwa kutokana na tukio hilo, mahakama imemtia hatiani Bw. Mroso kwa kubaka na mama yake kwa kusaidia ufanikishaji wa tendo hilo.

Walipopewa nafasi ya kujitetea, Bw. Mroso aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwani ana watoto watatu ambao wanamtegemea pia ana virusi vya UKIMWI.

Mshtakiwa wa pili, Bi. Kigelulye aliiambia mahakama kuwa yeye ni mzee mwenye miaka 60, watoto 10 ambao miongoni mwao wapo yatima anaowalea pia ana tatizo la shinikizo la damu hivyo apunguziwe adhabu.

Mwendesha mashtaka, Bw. Ikema aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa iwe fundisho kwa wengine kwani wanawake wengi wanafanyiwa ukatili wa aina hiyo.

Hakimu Mayumba alisema, mahakama inawahukumu washtakiwa hao kifungo cha miaka 30 jela ambapo mshtakiwa wa kwanza Bw. Mroso atachapwa viboko 12 na mali zao zote zitauzwa kwa mnada ili kulipa fidia ya sh. milioni 5.

Fedha hizo ni sehemu ya fidia kwa ajili ya mbakwaji kudhalilishwa na ndoa yake kuingia katika mgogoro.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!