'Nabembelezwa” ulikuwa ni moja ya nyimbo za Barnaba ambazo nilitokea kuzipenda sana. Lakini wimbo huo ilinikera pale video yake ilipotoka ikiwa na ‘Scene’ ambayo inawaonyesha watoto wa umri mdogo chini ya miaka saba wakipigana busu.
Mambo hayakukomea hapo, Bob Junior naye alikuja na kibao chake cha “Nichumu” ambacho video yake pia ilikuwa ikionyesha yaleyale yaliyofanyika kwenye wimbo wa Barnaba.
Shida inakuja pale nyimbo hizo zinapopigwa mchana muda ambao watoto wetu wanakuwa nyumbani na wanaona yale yanayofanywa na watoto wenzao kwenye runinga.
Kipi kizuri wanajifunza kutoka katika hizo kazi zenu mnazoziita za sanaa? Bila shaka hakuna zaidi ya uharibifu mkubwa wa maadili kwa jamii yetu hasa kwa watoto.
Sanaa imekuwa na mchango mkubwa katika suala zima la ajira kwa vijana lakini pia imechangia mmomonyoko mkubwa wa maadili na kama unapingana na hilo tazama video nyingi za miziki na hata filamu.
Kwenye sinema zetu, wanawake wanavalia nusu uchi kana kwamba wote wanacheza uhusika wa kahaba; yaani namaanisha wanavaa hivyo hata pasipostahiki.
Kwa uchunguzi usio rasmi nimegundua kwamba wengi wenu mnaiga yanayofanywa na wasanii kutoka nchi za Magharibi huku wangi wakisahau kwamba wao wana utamaduni wao na sisi tuna wetu.
Kama kuna mtu aliwadokeza kwamba mashabiki tunapenda ujinga wa namna hiyo amewadanganya. Sisi (Mashabiki) tunapenda tutazame filamu na nyimbo zenu tukiwa tumejumuika na familia zetu hapa namaanisha mama zetu, baba na hata watoto wetu. Lakini naanzaia wapi kuthubutu kutazama filamu ya Kibongo mbele ya mtu ninayemuheshimu? Siwezi kwani naogopa kufedheheka.
Usitegemee kwamba utatengeneza video ya muziki yenye kuhamasisha vitendo vya ngono na ikafanikiwa. Ili kujifunza hilo tazama baadhi ya video za hapa Tanzania zilizowahi kushinda tuzo za nje.
Tazama video ya wimbo wa “walk alone” ya AY, ilishinda tuzo za Channel O ingawa haikuwa na sehemu hata moja inayoonesha mwanamke aliyevalia nguo za ndani pekee na anakatika katika bila mpango ufukweni.
Rudi kwa Diamond na nyimbo yake ya ‘My Number one’ imempa tuzo zaidi ya tatu za Channel O pia na nyingine nyingi za nje lakini haina huo upuuzi ambao mmeukazania nyinyi.
Au hamfahamu kwamba sanaa kazi yake ni kuelimisha na kuburudisha pia? Labda mnaposikia kuburudisha mnadhani ni wanawake kudhalilishwa na kujidhalilisha kwa kuvaa nusu uchi na kuchezacheza hovyo ufukweni?. Huo ni udhalilishaji tena wa hali juu.
Je, mamlaka husika hamlioni hili? mara kwa mara tumesiki video kadhaa zikifungiwa lakini tatizo bado lipo pale pale jambo linalozidi kuniweka njia panda kwa kutoelewa ni kipi hasa kinastahili kufungiwa na kipi hakistahili kutokana ukweli kwamba hata hizo zilifungiwa hazina tofauti sana na ambazo zipo sokoni.
Bila shaka si mimi pekee mwenye shaka juu ya kipi kinastahili kufungiwa na kipi hakistahili kufungiwa.
Basi mamlaka zinapofungia kazi hizo zitueleze kinagaubaga kuhusu vigezo wanavyoangalia kabla ya kuizuia kazi na si kuishia kutuambia kuwa “Tumefungia kazi fulani kwasababu inahamasisha ngono” wakati hizi tulizobaki nazo mtaani zinalingana na hizo zilizofungiwa.
Jambo la kukumbuka hapa ni kwamba sanaa ina mchango mkubwa katika kuitengeneza sura ya jamii yetu ndio maana tunawatumia wasanii katika maeneo mbalimbali kutokana na ushawishi walio nao hivyo wanapovunja maadili kupitia kazi zao za sanaa ni wazi kwamba hata jamii yetu itafanana hivyo.
Ni muda sasa wa kudilika na tumieni sanaa yenu kujiingizia kipato na kulinda maadili yetu
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment