Saturday, 21 March 2015
JIHADHARI NA UGONJWA WA FIGO UNAOONGEZEKA NCHINI
FIGO ni kiungo kimojawapo kati ya viungo muhimu ndani ya mwili wa binadamu ambacho kinapatikana maeneo ya ubavuni ndani ya tumbo la mtu.
Mtoto anapozaliwa figo huonesha dalili ya kuwa zinafanya kazi kwa mtoto mchanga kupata haja ndogo ndani ya saa 48 baada ya kuzaliwa na endapo hatokojoa katika kipindi hicho, basi huonesha kwamba mtoto ana tatizo kwenye kiungo hicho. Dalili ya ugonjwa wa figo kwa mtoto mdogo ni pamoja na kuzaliwa na uvimbe tumboni.
Wengine hujikamua wakati wa haja ndogo na mkojo unaotoka ukiwa mchache. Daktari Bingwa wa magonjwa ya figo na magonjwa ya watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Jacqueline Shoo, anasema kuwa kazi kubwa ya figo ni kuchuja sumu zinazotengenezwa mwilini kutokana na vyakula na vinywaji mbalimbali.
Pia kazi nyingine ni urekebishaji wa maji mwilini, urekebishaji wa shinikizo la damu, utengenezaji wa vimeng’enyo vinavyotumika kutengeneza damu na kuimarisha mifupa. Dk Shoo anasema takwimu zinaonesha kwamba asilimia 8-16 ya watu duniani wanasumbuliwa na matatizo kwenye figo.
Pia inakadiriwa kwamba ifikapo 2023 asilimia 70 ya watu wanaoishi nchi za jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania wataathirika na ugonjwa huo. “Katika utafiti uliofanyika 2011, Tanzania inashika nafasi ya 54 katika nchi zinazoongoza kuwa na vifo vinavyotokana na magonjwa ya figo ambapo asilimia 1.03 hufariki kwa ugonjwa huo kila mwaka,” anasema Dk Shoo.
Anasema kitaalamu ugonjwa wa figo unatafsiriwa kama kupungua kwa uwezo wa kazi ya figo. “Ugonjwa huu husababishwa na magonjwa mengine kama vile ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, ugonjwa wa chujio la figo na magonjwa mengine kama vile maambukizi ya Ukimwi, saratani za aina mbalimbali na magonjwa ya njia za mkojo kama vile tezi dume,” anasema Dk Shoo.
Mengine yanayochangia ugonjwa wa figo ni pamoja na unywaji pombe, uvutaji sigara, maambukizi ya mkojo mara kwa mara, matumizi holela ya dawa mbalimbali za binadamu, dawa za mitishamba zisizo na viwango na utoaji wa mimba.
Pia anasema kuwa kwa wasichana na akina mama wanaotoa mimba pia wapo katika hatari ya kuugua ugonjwa wa figo kwani huharibu mfumo wa damu au mara nyingine kuzidiwa katika kuchuja sumu mwilini kwa sababu ya dawa watumiazo katika tendo hilo.
Akizungumzia dalili za ugonjwa huo, Dk Shoo anasema kuwa figo inaposhindwa kufanya kazi, inaweza kusababisha kutokwa kwa damu katika fizi au sehemu yoyote iliyo wazi. Pia dalili nyingine ni kutapika na kukosa nguvu mwilini na kuvimba uso na miguu. Kwa mujibu wa Dk Shoo, ugonjwa wa figo unaweza kutibika kulingana na hatua iliyofikia.
Anasema kuwa matibabu maalumu ni ya aina mbili, moja ni usafishaji wa damu kwa figo bandia (dialysis) na nyingine ni upandikizaji wa figo. Kwa sehemu kubwa usafishaji wa damu hutumika kama daraja ambalo baadaye mgonjwa hupandikizwa figo kama tiba kuu ya ugonjwa wa figo.
Usafishaji wa damu kwa mashine hujulikana kama hemodialysis na ule wa kuwekewa maji tumboni hujulikana kama peritoneal dialysis.
“Usafishaji wa damu kwa mashine humwezesha mgonjwa kuweza kuchuja taka sumu za mwilini kwa kutumia kifaa maalumu kinachofanya kazi kama figo. Damu ya mgonjwa hupitishwa kwenye kifaa hicho kwa kutumia vifaa maalumu na baada ya kusafishwa hurudishwa tena mwilini,” anafafanua daktari huyo bingwa.
Dokta anasema anayepandikizwa figo hupaswa kuwa na mchangia figo ambaye ni ndugu wake wa damu na aliye tayari kuchangia figo yake. Anasema mtu anayetaka kumchangia figo ndugu yake ni lazima apatiwe elimu ya kina kuhusu masuala ya figo kuondoa imani kwamba figo moja pekee ndiyo inafanya kazi.
Anasema pamoja na elimu hiyo, anatakiwa kuchunguzwa kwa kina kabla ya upandikizwaji huo kufanyika. Pia anasema baada ya matibabu hayo, mpandikizwaji huendelea kuwa kwenye matibabu maalumu na kisha hurejea katika mfumo wake wa maisha ya kawaida.
Akizungumzia kinga, Dk Shoo anasema kuwa wenye ugonjwa wa figo wanatakiwa kufuata maelekezo ya wataalamu, ikiwamo lishe na matumizi ya kunywa maji na dawa. Daktari huyo wa magonjwa ya figo na ya watoto anasema kuwa zipo changamoto nyingi zinazoikabili taaluma hiyo ikiwamo uhaba wa wataalamu Pia anasema changamoto nyingine ni ughali wa dawa maalumu za figo ambazo hugharimu Sh milioni mbili kwa kila mwezi.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wataalamu wa Figo (NESOT), Dk Onesmo Kisanga anasema kuwa ni rahisi sana kuzuia ugonjwa wa figo endapo mtu atakuwa na mazoea ya kupima afya kwa mwaka mara mbili.
Anasema miaka sita iliyopita hakukuwepo na wataalamu wa figo nchini lakini kwa sasa Serikali imetoa nafasi kwa wanafunzi mbalimbali au madaktari kuweza kusomea taaluma hiyo, licha ya kwamba bado wapo wachache. Mmoja wa mgonjwa aliyelazwa katika hospitali hiyo, Simbano Msangi anashauri serikali kutoa huduma kwa wagonjwa wa figo kupitia bima katika hospitali za mikoani ambazo ni za binafsi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment