Filamu ya kusisimua inayohusu ukatili wa watu wenye ulemavu wa ngozi(Albino) inatarajia kuzinduliwa mwezi April Mwaka huu.Filamu hiyo iliyopewa jina la “FIRIGISI” imefanywa na wasanii kutoka mkoa wa Shinyanga( Bongo Movie Shinyanga) na msanii Denice Sweya maarufu Dino kutoka Bongo Movie Dar es salaam.
Dino ameigiza na kuongoza Filamu hiyo ambayo imebeba maudhui kuhusu Ukatili wanaofanyiwa watu wenye Albinism nchini Tanzania huku watu mbalimbali wakitajwa kuhusika katika ukatili huo wakiwemo wafanyabiashara,wachimbaji wa madini na wanasiasa.
Akizungumza na Malunde1 blog mjini Shinyanga Mwongozaji wa Filamu hiyo Denice Sweya( Dino) amesema filamu hiyo ina maudhui mazuri kwani hata mazingira yake ni ya Kanda ya Ziwa ambako ndiko vitendo hivyo vya ukatili vimekuwa vikifanyika.
“Ni filamu ya kiwango cha juu sana inasisimua,imeandaliwa na wasanii kutoka mkoa wa Shinyanga,msanii pekee kutoka Dar es salaam ni mimi ambaye nimeigiza na Kuongoza Filamu hii,production yake pia imefanyika Dar es saalam kwani wapiga picha wanatoka Dar es salaam ambao ni Amani Masuka akishirikiana na Benny Luoga”,ameeleza Dino.
“Filamu hii ina maudhui yanayogusa Kanda ya Ziwa kwani ndiyo inaonekana kuwa ina matatizo makubwa ya ukatili wa watu wenye albinism,tumejitahidi kuielimisha jamii,tumeonesha,chanzo cha vitendo hivyo, kipi wanapaswa wajue,nini kifanyike,nini kinawaponza na mambo kadha wa kadha”,ameongeza Dino.
Dino amesema washiriki katika filamu hiyo ni watu wanayoyajua vyema mazingira ya Kanda ya ziwa na kwamba miongoni mwa wahusika wakuu yumo kijana mwenye Albinism hali ambayo imefanya filamu hiyo iwe katika kiwango cha juu na wanategemea filamu hiyo itakuwa katika kiwango cha Kimataifa kwani haijawahi kutokea.
Amesema mdhamini mkuu aliyetoa mamilioni ya fedha kufanikisha kutengenezwa kwa katika filamu hiyo ni ndugu Wille Mzava wa mjini Shinyanga na kwamba filamu hiyo inatarajia kuzinduliwa mjini Shinyanga kati ya Mwezi Aprili na Mei mwaka huu huku wageni wakiwemo wafanyabiashara wakitarajiwa kuhudhuria uzinduzi huo ambapo mgeni rasmi atakuwa mtu mkubwa sana hapa nchini ingawa hakutaka kutaja jina lake.
Aidha Dino amesema kauli mbiu waliyotumia katika filamu hiyo ni “Albino ni Mimi na Wewe,Tuwalinde,Tuwapende na Tuwathamini(TTT)” ikiwa ina maanisha kuwa kibaiolojia mwanamme na mwanamke mweusi wanaweza kukutana na kuzaa mtoto mwenye Albinism,na kwamba ni ndugu zetu Tunazaa wenyewe kwani huwezi jua kesho kitatokea nini,mtu yeyote anaweza kuzaa mtoto mwenye albinism.
Mwenyekiti wa Bongo Movie Shinyanga Juma Ibrahim Songoro (Songoro Gaddafi) amewaomba wakazi wa Shinyanga,kanda ya ziwa na nchi kwa ujumla kuunga mkono kazi yao ya kwanza na kuahidi filamu hiyo kuzinduliwa haraka iwezekavyo.
“Hii ni filamu ya aina yake,haijawahi kufanywa popote duniani,hatujaiga mahali popote kama wanavyofanya baadhi ya wasanii,na filamu hii inamvuto,inasikitisha,inasisimua,inafunza,inaonya,inaelimisha kwa kila mtu atakayeiangalia hivyo tunaamini itapokelewa siyo tu kitaifa bali kimataifa”amesema Songoro
Na Kadama Malunde-Shinyanga
No comments:
Post a Comment