Serikali imewasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za kulevya ambao unawabana wauza ‘unga’ ukipendekeza kuwa watakaobainika kufanya biashara hiyo haramu watozwe faini ya Sh. bilioni moja au kifungo kisichopungua miaka 30, huku wabunge wakitaka watakaobainika wapigwe risasi hadharani au wanyongwe.
Aidha, atakayekutwa analima, kusambaza mbegu, kusafirisha, kuzalisha au kuingiza mimea inayozalisha dawa za kulevya kama bangi, mirungi na cocaine atatozwa faini isiyopungua Sh. milioni 20, kifungo kisichozidi miaka 30 au vyote kwa pamoja.
Wakichangia muswada huo ambao uliwasilishwa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri MKuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenister Mhagama (pichani), wabunge walipendekeza kufutwa kwa kipengele cha faini kwa kuwa kinatengeneza mazingira ya rushwa kwa watendaji wa serikali wanaohusika na kazi ya udhibiti wa dawa za kulevya, kwa kuwa wanaofanyabiashara hiyo ni watu wenye mabilioni ya fedha.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, alisema vita dhidi ya dawa za kulevya inakuwa ngumu kutokana na tabia ya serikali kulinda watuhumiwa hata pale ushahidi unapokuwa wazi.
Alisema ili kukomesha tabia hiyo, sheria hiyo inapaswa kutamka kwamba watakaobainika kujihusisha na biashara hiyo adhabu ndogo iwe kifungo cha maisha, kunyongwa hadi kufa au kupigwa risasi hadharani na kwamba adhabu ya faini iondolewe.
“Bila hivyo, tutakuwa tunabadilisha chupa, lakini mvinyo ni ule ule. Tatizo tulilonalo ni kulindana siyo vyombo vya usimamizi. Polisi wakikamata
mfanyabiashara wa dawa hizi, simu za wakubwa zinapigwa wanawaachia, kwa hiyo mimi sikubaliani na hili la kuanzisha mamlaka kama hatutaondoa tatizo la kulindana,” alisema.
Alisema wafanyabishara wa dawa za kulevya wanajulikana kwa majina hadi nyumba wanazoishi lakini hawachukuliwi hatua badala yake vyombo vya dola vinahangaika kukamata wasafirishaji wadogo wadogo.
Aidha, alikiri kuwa na orodha ya majina na namba za nyumba wanakoishi wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini, lakini hawezi kuwataja bungeni
hapo kutokana na hali ya sasa kuonyesha kuwa mfumo mzima unawalinda wafanyabiashara hao.
Naye mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, pamoja na kutaka watakaokutwa na dawa za kulevya kunyongwa au kupigwa risasi hadharani wiki mbili baada ya kuhukumiwa, pia aliitaka Serikali itafute mbinu ya kuondoa dhana kuwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo wanalindwa.
Mbunge wa Chambani (CUF), Yusuph Salim Hussein, aliungana na wenzake na kutaka adhabu ya kifo cha kunyongwa au kupigwa risasi hadharani kwa watakaojishughulisha na dawa za kulevya huku akisisitiza adhabu hiyo ni stahiki kutokana na madhara makubwa ya dawa hizo kwa jamii.
“Lakini pia naomba niulize inakuaje mtu anakutwa amemeza kete tumboni za dawa za kulevya, anazitoa tumboni lakini hachukuliwi hatua eti kwa
sababu ya uchunguzi, uchunguzi gani? Watu kama hawa wahukumiwe palepale,” alisisitiza.
Mbunge huyo alimtaja kijana mitano sasa, kwa kosa la kukutwa akisafirisha dawa za kulevya, akisema tajiri aliyemtuma ambaye alimtaja kwa jina moja la Dewji yuko nje na wala hajawahi kuhojiwa.
Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde, alisema ni wakati sasa Serikali ianze kufanyia kazi hukumu za kunyongwa zinazotolewa na majaji kwa watuhumiwa wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi au kukutwa na kuuza dawa za kulevya ili kukomesha vitendo hivi.
“Sasa hivi kuna kesi za wauaji wa albino zimetolewa hukumu ya kunyongwa, lakini mpaka leo hawa watu hawajanyongwa, kwa sababu Rais hajasaini, sasa tunapendeza kunyongwa pia hawa dawa za kulevya, Rais kabla hajaondoka madarakani, asaini wanyongwe,” alisisitiza.
Alisema serikali inapata kigugumizi cha kuwabana wafanyabiashara wa kubwa wa biashara hiyo kwa kuwa ni matajiri wenye nguvu ya kufanya jambo lolote kujilinda.
Awali, akiwasilisha muswada huo, Mhagama alisema katika kuiongezea ukali sheria hiyo, adhabu za watu wote watakaoukutwa, kutumia, kufadhili au kufanya dawa za kulevya zimeongezwa na kuwa kali zaidi.
Serikali inakusudia kuanzisha Chombo kinachojitegemea chenye mamlaka ya kiutendaji ya kuchunguza, kupekua na kukamata watuhumiwa tofauti na ilivyo Tume.
Nayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, imeungana na wabunge kwa kutaka adhabu ya faini iondolewe kwenye sheria hiyo badala yake ibakie kifungo cha maisha au kunyongwa, pindi mtuhumiwa atakapothibitika kuhusika na biashara hiyo.
Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, mbunge wa Viti Maalum (CCM), Neema Himd, alisema wakulima wa mimea ya dawa za kulevya kama bangi, kamati hiyo imependekeza kuwa watakaobainika waongezewe kifungo na kusiwepo na faini.
Alisema Kamati pia imependekeza kuwa baadhi ya wadau wameeleza kuwa hivi sasa wauza ‘unga’ wameanza kutengeneza wateja kwa kuweka dawa hizo kwenye vyakula na vinywaji kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, hivyo akapendekeza kuwa adhabu iwe kali ili kukomesha uharamia huo.
Naye msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika Wizara hiyo, Rajab Mohamed Mbarouk, alisema ili sheria hiyo iwe kali, lazima adhabu iwe ni kifungo cha maisha au kunyongwa hadi kufa badala ya kuweka adhabu ya faini au kifungo.
“Kambi rasmi inapendekeza kufuta masharti yote yanayotoa nafasi ya kulipa faini kwa mtu atakayepatikana na biashara ya dawa za kulevya na badala yake kuacha masharti ya kifungo pekee, hii itasaidia kukomesha biashara hii haramu ambayo inaangamiza nguvu kazi ya Taifa,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment