Thursday 19 March 2015

BUNGE LAPITISHA MUSWADA WA SHERIA YA KURATIBU AJIRA ZA WAGENI NCHINI

    111            
WAZIRI wa Kazi na Ajira Mhe. Gaudensia Kabaka amesoma Muswada wa Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini wa mwaka 2014 kwa mara ya pili ikiwa muswada huu umelenga masuala mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya kiuchumi pamoja na mahitaji ya kiteknolojia ambayo ni kichocheo kikubwa  cha uhamiaji wa nguvu kazi kutoka nchi moja kwenda nyingine.


 Mhe.Kabaka alisema kwa sasa zipo mamlaka nyingi zinzotoa vibali vya ajira kwa wageni kwa kuzingatia sheria zinazosimamia maswala ya Uhamiaji, Uwekezaji, Elimu, Biashara na Wakimbizi, hivyo hali hii ya kuwepo na mamlaka nyingi zinachangia  kusababisha usumbufu kwa wawekezaji na kokosekana kwa uwajibikaji pamoja na kuwepo na udanganyifu.

“Kutungwa kwa sheria hii kunalenga kutelekeza kwa manufaa ya nchi yetu mikataba ya kikanda inayoruhusu uhamiaji huru wa nguvu kazi hususani inayohusu itifaki ya soko la pamoja la Jumuiya ya Afika Mashariki na Ushirikiano wa Jumuiya ya nchi za kusini mwa Afrika SADC” alisema Mhe. Kabaka.

Katika kutekeleza mikataba ya kikanda na kimataifa kuhusu uhamiaji na nguvu kazi, utaratibu wa kutoa vibali vya ajira kwa wageni umekuwa ukitumika ili kuhakikisha nguvu kazi ya wageni hao inaleta manufaa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na pia katika kulinda ajira za wananchi.
Kwa upande wa Msemaji Mkuu wa kambi rasmi ya upinzani Mhe.Celina Paresso Mbuge wa Viti Maalum-CHADEMA aliishauri Wizara ya Kazi na Ajira kushirikiana na wizara mtambuka kama Wizara ya Viwanda na Biashara na Idara ya Uhamiaji, kufanya ukaguzi wa vibali vya ajira hasa katika maeneo ambayo raia wa kigeni wanafanya shughuri zao bila kuzingatia sheria za nchi.

“Tanzania tuna maliasili nyingi, lakini dunia ya leo na ijayo itatawaliwa na wenye maarifa, kwa maana ya sayansi, teknolojia, elimu na ujuzi” alisema Mhe. Paresso
“kuwa na maliasili peke yake haitoshi, hatuna budi tujinoe kwa elimu na ujuzi, na hasa elimu inayomuwezesha mtu aajirike au ajiajiri” aliongezea Mhe. Paresso
Endapo Mhe. Rais ataridhia, Sheria hii itaanza kutumika tarehe 1 Julai, 2015. Kutungwa na kuanza kutumika kwa Sheria ya Ajira ya Wageni Nchini kutakuwa na matokea chanya ikiwema uratibu mzuri wa ajira za wageni nchini, kuongezeka kwa ajira za watanzania na kuongezeka kwa ujuzi kwa wafanyakazi wa Tanzania

Na. Anitha Jonas na Johary Kachwamba -MAELEZO, DODOMA

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!