Monday, 23 March 2015

BARABARA ZETU NI AJALI TOSHA MADEREVA NI CHAMBO TU-JULIUS MTATIRO


Unaweza kuwa umekaa mahali fulani, lakini kichwani ukiogopa kusafiri kutokana na mfululizo wa ajali za barabarani zilizotokea hivi karibuni.

Dada yangu aitwaye Judith ni mwoga hata kuendesha gari yake kwa kuhofia kugongwa au kugonga. Ajali zimepamba moto tangu mwaka huu uanze, na zimeongezeka mwezi wa Machi.
Zamani niliwahi kusikia tetesi ambazo ziliaminiwa na watu wengi kuwa katika mwaka kuna miezi ya ajali, ukisafiri wakati huo kuna uwezekano mkubwa wa kupata ajali. Tulitajiwa kuwa miezi ya karibu na pasaka (Machi na Aprili) na ile ya mwisho wa mwaka (Novemba, Desemba na Januari) huwa na ajali nyingi.
Pia, hata wakati naandika makala hii bado natatizwa na uwepo wa ajali kwa kuhusianisha na wakati fulani wa mwaka.
Ukweli unabakia kuwa ajali ni ajali tu na inaweza kutokea muda wowote, wakati wowote, siku yoyote, saa yoyote na sekunde yoyote.
Wataalamu wanasema ajali hutokea na kukamilika ndani ya sekunde chache na mara nyingi humnyima dereva au abiria kufikiri cha kufanya na ndiyo maana husababisha maafa makubwa bila dereva na abiria kujitetea.
Mathalan gari inakwenda kwa mwendo kasi wa kilomita 120 kwa saa. Hii ni sawa na kasi ya mshale. Katika mwendo huu, gari moja ikikutana na nyingine, kitakachojiri ni kukusanya miili ya makumi ya wananchi wenzetu ambao dakika chache zilizopita walikuwa wakicheka, kufurahi, kupiga simu na kutambiana. Matarajio yao yalikuwa kufika salama. Lakini ghafla watu wote hawa wanakuwa marehemu!
Pamoja na madereva wetu kulaumiwa sana kwa kusababisha ajali, mtazamo wangu ni kuwa serikali ilipaswa kulaumiwa kwanza ndipo madereva wafuate.
Kila ajali inapotokea nimekuwa nawaona makamanda wa polisi wa mikoa na wilaya wakieleza sababu ya ajali hiyo kuwa ni mwendokasi wa madereva au kukosa umakini. Sijawahi kumsikia kamanda akisimama na kusisitiza kuwa ajali imetokea kwa sababu serikali imeshindwa kujenga barabara fulani kwa viwango stahiki.
Nasema hivi kwa sababu ajali nyingi zinasababishwa ama na ubovu wa barabara zetu au miundo mibovu ya ujenzi. Ajali kama iliyotokea hivi karibuni eneo la Mafinga kati ya lori na basi na kuua watu 52 ilisababishwa na magari yote kuwa katika mwendo w akasi huku yakikabiliwa na jukumu la kukwepa mashimo makubwa barabarani. Katika harakati hizo ndipo lori likaangukia basi na kusababisha mauti kuu.
Nilimwona kamanda wa polisi wa Iringa akisisitiza kuwa ajali hiyo ilisababishwa na madereva.
Tunamdanganya nani? Ni kweli kwamba madereva wote wawili walipaswa kuwa wanajua barabara wanayopita kwamba ina mashimo, lakini je kwa nini tuwape kazi hii madaereva wetu? Kwamba dereva anaendesha gari kila mara akiwaza wapi kuna mashimo? Kwa nini tusiyazibe kwa uimara wa kipekee yasiwepo kwa muda mrefu? Tunafurahia nini wato wanapokufa halafu tueleza kuwa walikuwa kwenye mwendo mkali?
Hivi tunataka gari itembee kutoka Iringa hadi Dar kwa mwendokasi wa kilomita 20 kwa saa? Na mbona tukaruhusu magari yenye mwendokasi wa kilomita 180 hadi 240 yaingizwe nchini? Tunataka yaendeshewe wapi? Najaribu kujiuliza ikiwa tumeacha kufikiria! Yaani tunaingiza magari yenye mwendokasi mkubwa, halafu hatutengenezi barabara zetu na baadaye watu wakishakufa tunatupa lawama kwa dereva, ambaye kwa kiasi kikubwa naye huwa marehemu, kisha sisi tunaendelea na mambo yetu kama kawaida? Hakika serikali yetu bado haiwajibiki katika jambo hili muhimu.
Tunajenga barabara kwa mfumo wa njia moja na hiyo hiyo ndiyo inatumiwa na magari yanayokwenda na kurudi.
Hivi tunategemea nini? Magari haya yanapishana kwa sentimita chache sana kutoka gari moja hadi jingine, tena yakiwa katika mwendo wa kasi. Tunataraji nini kitokee gari moja linapoyumba? Ni dhahirini kuangukia au kugonga gari jingine na kuua watu.
Njia zetu kuu kama Dar es Salaam hadi Namanga, Dar es Salaam hadi Mtwara, Dar es Salaam hadi Mbeya, Dar hadi Bukoba na Dar es Salaam hadi Sirari, zilipaswa kujengwa kwa mfumo wa njia mbili tofauti. Kwamba magari yanayotoka Dar es Salaam kwenda Mwanza yawe na njia yake na iwe na ukubwa wa kupitisha walau magari mawili au matatu kwa wakati mmoja na yale yanayotoka Mwanza kuja Dar es Salaam yawe na njia yake. Lengo ni kuhakikisha kuwa magari yanayokwenda na kurudi hayapishani kwenye njia moja. Barabara hizi zisingekuwa tishio kwa maisha ya watu, maana hakutakuwa na gari kwa mbele tofauti na sasa ambapo ili gari moja lilipite gari la mbele ni lazima kuchungulia kuhakikisha hakuna gari linalokwenda mwelekeo hasi.
Hatuhitaji kutuma mawaziri wetu Ulaya kujifunza haya kwa sababu hata hapa Afrika nchi nyingi tu zimeshaweka miradi ya barabara za aina hiyo.
Kwamba wizara zinapofikiria kujenga barabara mpya, zinamaanisha kujenga barabara mbili tofauti zenye njia zaidi ya mojamoja na kufanya magari yanayokwenda na kurudi yasikutane? Hivi tutazuiaje ajali ikiwa barabara zetu zote muhimu zinakutanisha magari safari nzima?
Nawasifu sana madereva wetu! Ni kazi nzito kuendesha gari kwenye hizi nchi zetu!
Ikiwa serikali itatumia kodi zetu kutengeneza barabara za namna hii (jambo linalowezekana kabisa!) tutakuwa na mwanya na nguvu kubwa kuwashupalia madereva wanaovunja sheria.
.za barabarani, kutokuwa makini na kusababisha ajali.
Kwa mtizamo wangu, ni ajali chache sana ambazo husababishwa na umakini mdogo wa madereva lakini ajali nyingi husababishwa na ubovu wa barabara na tatizo la kutumia barabara moja yenye njia mbili zinazopishanisha magari hapo hapo.
Wakati serikali inaandaa mpango wa muda mrefu wa kujenga barabara mbili tofauti zenye njia tofauti za kwenda na kurudi, inapaswa kufanya marekebisho makubwa kwenye maeneo yote korofi. Ukiendesha gari kutoka Dar kwenda Mtwara utakutana na maene korofi zaidi ya 100, utakuta barabara imechimbika katikati, kuna mchanga umejaa barabarani, kuna mashimo ya kila aina n.k. Hivi ni vikwazo vikuu kwa madereva wengi jambo linalofanya watumie umakini mkubwa kupita kiasi wanapokuwa safarini.
Naamini kuwa, utafiti ukifanyika itagundulika dereva wa Tanzania anatumia akili nyingi kuendesha gari barabarani zaidi ya mara 10 ya dereva anayeendesha gari nchini Afrika ya Kusini.
Nasisitiza kuwa serikali ina wajibu wa kutumia kodi zetu kututengenezea barabara bora na zenye usalama ili ipate sababu ya kupambana na madereva wakorofi bila aibu. Lakini kuendelea na barabara hizi mbovumbovu miaka nenda rudi inaleta ile dhana ya “kujibaraguza” katika jambo ambalo lilipaswa kutatuliwa kwa uwazi.
Ni masikitiko yangu kuwa watanzania wataendelea kufa kila siku huku serikali ikitupa lawama kwa madereva peke yao bila kugusa upande wake ambao kwa mtizamo wangu ni kisababishi cha ajali kwa kiasi kikubwa kuliko uzembe wa madereva.
Tukumbuke ule msemo maarufu “kama elimu ni ghali, jaribu ujinga”.
Msemo huu utukumbushe jambo kwamba “kama kujenga barabara zisizopishanisha magari ni gharama kubwa, tujaribu kuendelea na ajali zisizokwisha!” Hakika, ujenzi wa barabara imara, za muda mrefu na za kudumu zenye upana wa kutosha (kwa maana ya njia zinazokwenda na kurudi bila kukutana), ni suluhisho pekee litakalotuondoa kwenye aibu ya kuzika ndugu zetu kila siku huku lawama tukiwatupia madereva.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!