Jeshi
la polisi mkoani Simiyu linawashikilia askari wawili wa jeshi la
magereza na polisi kwa kukutwa na noti bandia ikiwa ni pamoja na sare za
jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ).
Akitoa
taarifa za kukamatwa kwa askari hao Naibu Kamishna wa jeshi la polisi
Mkoani Simiyu Charles Mkumbo alisema kuwa askari hao walikamatwa juzi
majira ya saa 9 mchana katika mtaa wa Old Maswa kata ya Nyakabindi
Wilayani Bariadi.
Alisema
askari hao walifika kwenye kibanda cha M-pesa kinachomilikiwa na
Mwalimu wa Shule ya sekondari Old Maswa Kassian Luhende (29), wakiwa na
pikipiki yenye namba za usajili T-403 CXW aina ya Sunlg kwa lengo la
kuweka fedha hizo kweye simu.
Alisema
baada ya Mwalimu huyo kupokea fedha kiasi cha noti 10 zenye thamani ya
Shilingi 10,000 alizitilia shaka ambapo alipoendelea kuzikagua zaidi
alizigundua kuwa siyo fedha halali.
Mkumbo
alieleza kuwa Mwalimu huyo baada ya kugundua fedha hizo kuwa ni feki,
alichukua jukumu la kuwajulisha majirani zake ili kuomba Msaada wa
kuweza kuwakamata askari hao baada ya kugundua siyo watu wema.
Aidha
alieleza kuwa baada ya mwalimu kutoa taarifa kwa majirani, wananchi
walikusanyika na kuanza kuwahoji askari hao, ndipo askari mmoja alipotoa
kitambulisho kuwa yeye ni askari na mwingine kujitambulisha kuwa ni
dereva bodaboda.
Alibainsiha
kuwa wananchi baada ya kuambiwa hivyo waliwatilia shaka zaidi ambapo
walitoa taarifa Kituo cha polisi Bariadi, na askari kwenda kuwakamata.
Mkumbo
aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni askari mwenye namba H 2420 PC Seleman
Juma (25) ambaye ni askari wa kikosi cha kutuliza gasia FFU Mkoani
Simiyu, na askari namba B.6499 WDR Edmund Masaga (28) ambaye ni askari
Magereza wilayani Bariadi.
Kamanda
Mkubo alieleza kuwa baada ya askari hao kukamatwa mmoja wao PC Selemani
Juma alipopekuliwa katika mfuko wa suruali yake alikutwa na noti
zingine za Bandia za elfu kumi kumi na jumla yake kama zingelikuwa
halali zingelikuwa na thamani ya Shilingi 1,920,000.
Mbali
na hilo Mkumbo alieleza kuwa Askari huyo alipokwenda kupekuliwa
nyumbani kwake alikutwa na sare za JWTZ ambazo ni Pensi 4, T-shirt 2,
Kombati 1 pamoja na Kitambaa.
Hata
hivyo Mkuu huyo wa polisi alieleza kuwa uchunguzi zaidi unaendelea ili
kubaini mtandao mzima wa usambazaji wa noti bandia ndani ya mkoa huo,
huku akieleza kuwa mara baada ya uchunguzi kukamilika askari hao
watachuliwa hatua za kinidhamu pamoja na kisheria.
Alitoa
onyo kwa askari Mkoani Simiyu kuacha tamaa ya pesa na badala yake
waridhike na ajira zao zinazowapatia pesa halali, huku akieleza kuwa kwa
atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheraia na nidhamu.
No comments:
Post a Comment