Monday, 9 February 2015
WATANZANIA WAONYWA URAIS WA FEDHA NA UDINI
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amewataka Watanzania kuwapuuza wanasiasa wenye kutaka kutumia fedha, dini, ukabila na aina yoyote ya ubaguzi kujijengea uhalali na kuombea kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Akifunga Mkutano wa Kimataifa wa Utume wa Kanisa la Waadventista Wasabato, Dar es Salaam juzi, Membe ameliomba kanisa hilo kuzungumza na vijana wao na kuwakumbusha wajibu wao wa kulinda amani na kufanya uchaguzi sahihi na kutokubali kutumika.
“Nawasihi muwapuuze wanasiasa wenye mwelekeo huo... hawa ni hatari kwa umoja na upendo wetu. Tuwachague wale wenye ulimi wa upendo, unyenyekevu, utu na amani. Tumwepuke shetani na kazi zake za ufisadi, rushwa na maovu mengine,” alisema Membe.
Mkutano huo wa kimataifa wa utume maarufu kama ‘Mission Extravaganza’ ulianza Jumatano wiki iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na uliwahusisha waumini wa kanisa hilo kutoka nchi 11 zilizoko katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, lengo lake likiwa ni kuwaandaa watu kiakili, kijamii na kiroho ili waweze kuishi maisha yenye uadilifu.
Zaidi ya watu 2,400 walibatizwa katika mkutano huo. Membe alisema mwaka huu, licha ya nchi kufanya uchaguzi mkuu lakini pia ina tukio lingine la kura ya maoni ya katiba, hivyo akasisitiza waumini wa kanisa hilo kuliweka taifa kwenye maombi.
“Nasisitiza hilo kwa kutambua kuwa kipindi kama hiki huja na migongano na mivutano katika nchi zenye demokrasia changa.”
Membe pia alitoa rai kwa waumini wa Kanisa hilo la Waadventista Wasabato kushiriki kikamilifu katika kutengeneza viongozi bora wa Serikali wanaozingatia misingi ya uadilifu, upendo na unyenyekevu.
Membe alisema kuwa dini na madhehebu yanayo nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye maadili na hofu ya Mungu, wakiwemo viongozi na hivyo kusababisha taifa kuwa na amani, upendo na mshikamano.
Alieleza kuwa kama Waziri wa Mambo ya Nje, amejifunza kuwa diplomasia na hofu ya Mungu vikifanya kazi pamoja hakuna changamoto yoyote isiyoweza kukabiliwa.
“Dini na Diplomasia vinahusiana pale masuala ya amani, ulinzi na usalama yanapoguswa. Hivyo nawaomba mshiriki katika kutengeneza viongozi bora katika jamii zetu kwa misingi ya uadilifu ambao watasimamia amani na kujiepusha na vitendo viovu ikiwemo rushwa,” alisema Membe.
Aidha, alilipongeza kanisa hilo kwa kuwa mfano mzuri wa ustahimilivu na uvumilivu wa kidini hapa nchini. Alieleza kwamba kamwe hajawahi kusikia Kanisa la Waadiventista Wasabato limeingia katika mgogoro na Serikali, dhehebu au dini nyingine.
Alisema hilo ni funzo kubwa kwa Watanzania, kwamba kutofautiana kiitikadi, kidini, kikabila au rangi si sababu tosha ya kuwagombanisha na kuvuruga amani ya nchi.
“Nalipongeza kanisa lenu kwa kuwa mfano mzuri wa uvumilivu wa kidini na imani, mnaendesha mambo yenu kwa uvumilivu mkubwa na kushirikiana na dini zote na hili linatufundisha kuwa kutofautiana kwetu sio sababu tosha ya kugombana,” alisisitiza Membe.
Membe alilihakikishia kanisa hilo dhamira ya Serikali ya kuendelea kushirikiana nalo kwa ajili ya ustawi wa nchi na kufafanua kuwa Serikali itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu kwa dini zote kama inavyoelezwa kwenye Katiba ya nchi.
“Serikali inao wajibu wa kusaidia dini na madhehebu kufanya kazi kwa uhuru. Bahati nzuri Katiba inayopendekezwa imezingatia kulinda uhuru huo hivyo tuiunge mkono,” alifafanua Waziri Membe.
Aidha, amelisifu kanisa hilo kwa kuanzisha miradi ya huduma zikiwemo Shule 15 za Sekondari na Msingi, Chuo Kikuu na Hospitali mbili ambavyo vinatoa mchango mkubwa kwa serikali na wananchi kwa ujumla.
Awali akimkaribisha Waziri Membe kufunga kongamano hilo, Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo duniani, Askofu Dk Ted Wilson alisema kuwa anawaombea viongozi wa Tanzania waendelee kuwa na maono kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kwamba wakimtumaini Mungu atawawezesha kupata maono mapya kwa ajili ya kulitumikia Taifa hili.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Kanisa hilo Kanda ya Afrika Mashariki na Kati, Askofu Blasius Luguri aliipongeza Tanzania kwa kudumisha amani ambayo imechangia kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo lililoshirikisha Mataifa zaidi ya 20.
Aidha, alimwomba Waziri Membe kufikisha ujumbe kwa Rais Jakaya Kikwete kuwa wana imani na Tanzania kuwa ni nchi ya amani, usalama na utulivu.
Kanisa la Sabato ni kanisa linalokua duniani likiwa na waumini milioni 307 huku waumini milioni 30 wakiwa Afrika na takriban milioni 5 wakiwa Tanzania.
VIA-HABARI LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment