Tanzania haiko tena kwenye kundi la nchi 10 maskini duniani, kwa mujibu wa Ripoti ya Benki ya Dunia (WB), iliyotolewa wiki iliyopita.
Ripoti hiyo imenukuliwa na jarida la uchumi la kwenye mtandao la Business Sheet la Februari 14, mwaka huu.
Imeangalia pato la taifa, ambalo kimsingi huwa ni jumla ya thamani ya bidhaa zilizozalishwa kwa kipindi fulani, mara nyingi kwa mwaka, kikigawanywa kwa idadi ya watu ndani ya nchi husika.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi 10 maskini zaidi duniani ni Malawi, ambayo pato la kila mwananchi wa taifa hilo kwa mwaka, ni Dola za Kimarekani 226.50.
Malawi inafuatiwa na Burundi, Dola 267.10, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Dola 333.20, Niger, Dola 415.40, Liberia, Dola 454. 30 na Madagascar, Dola 463.
Aidha mataifa mengine na pato la kila mwananchi, ni ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Dola 484.20, Gambia, Dola 488.60, Ethiopia, Dola 505, na nchi ya 10 kwa umaskini ni Guinea, ambako pato la mwananchi ni Dola 523.10.
Ripoti hii huenda ikawa ni habari njema kwa Tanzania, kwani kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Aprili, mwaka 2005, Tanzania ilikuwa ni ya tano kati ya nchi 10 maskini duniani.
Kwa mujibu wa Ripoti hiyo, Tanzania ilitanguliwa na Timor ambalo mwananchi wake alikuwa na pato la Dola 400 kisha Malawi, Dola 596, Somalia Dola 600, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Dola 675.
Pia, Tanzania iliyafuatia Yemen Dola 745, Burundi Dola 753, Afghanistan Dola 800, Guinea Bissau Dola 856 na Ethiopia Dola 859.
PROFESA SEMBOJA
Akizungumzia sababu zilizochangia Tanzania kuondoka kwenye kundi hilo la nchi 10 maskini zaidi duniani, Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Profesa Haji Semboja (pichani), alisema:
“Hilo linaonyesha kuwa tumeweza kujenga uwezo wa kuzimiliki, kuzisimamia, na kuziendesha rasilimali lukuki tulizojaliwa kuwa nazo, ili kuboresha ustawi wetu na taifa kwa ujumla, tofauti na wenzetu tuliokuwa nao kwenye kundi hilo.”
Prof. Semboja alisema vile vile kuwa hata ule wigo unaotumika kupata takwimu za jumla za pato la taifa, pia umepanuliwa zaidi, tofauti ilivyokuwa siku za nyuma.
Alisema kuna maeneo ambayo yameongezwa kwenye kupima jumla ya thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini, ambazo mwisho wa siku, ndio hutoa pato la taifa.
Profesa Semboja alisema, kama taifa limepiga hatua kwenye maeneo yanayoonyesha ishara ya kukua kwa uchumi, hasa upande wa sekta ya ujenzi, kama ile ya miundo mbinu, na majengo, maeneo yanayosaidia kuongeza tija katika pato la taifa.
“Tuna mabenki mengi hivi sasa, yaliyopanua fursa ya upatikanaji mikopo kwa wananchi, mikopo inayotumiwa kuwekezwa kwenye sekta za kiuchumi zilizo na tija moja kwa moja kama, ujenzi wa majengo yaliyo na uhakika wa mapato kwa watoa mikopo, wenye mali, na kwa wananchi wengine,” alisema.
Akijibu swali lililohusu takwimu nyingi za mashirika na taasisi mbalimbali za kimataifa kuonyesha uchumi wa Tanzania kukua bila ya kunufaisha wananchi walio wengi, alisema, hilo linatokana na mfumo wa kibepari uliopo.
Alisema wakati ni kweli kuwa uchumi unakua, lakini ni kweli vile vile kuwa ukuaji wake unagusa wachache, kwa sababu za kimfumo.
“Mfumo wa kijamaa ulijikita kwenye ustawi wa wote na ndiyo maana kwa mfano tulikuwa na shule nzuri za serikali zilizowahudumia wananchi wote, tofauti na mfumo wetu wa sasa ambapo shule nzuri zilizopo ni za binafsi zinazofikiwa na wenye nacho tu,” alisema.
WAZIRI WA FEDHA
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema kuondoka kwa Tanzania kwenye kundi la nchi 10 maskini zaidi duniani, kumetokana na jitihada za serikali za kuboresha maisha ya wananchi wake.
“Tumefanya vizuri katika kuboresha uchumi wa nchi na maisha ya wananchi na ushahidi wa hili tunaweza tukaupata kwenye viashiria vya maendeleo,” alisema.
Alisema viashiria hivyo ni kama vile vya kuongezeka kwa umri wa kuishi kutoka miaka 41 mwaka 1967 hadi miaka 61, mwaka 2012, ikiwa na maana kuwa huduma za afya zimeimarika.
Alisema hata vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 115 kati ya kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai, mwaka 1988 hadi kufikia vifo 21, mwaka 2013.
Aidha, alisema, hata idadi ya vifo vitokanazo na uzazi vimepungua kutoka vifo 578 kwa kila mama 1,000 wanaojifungua mwaka 2005, hadi 432 mwaka 2012.
“Tumepunguza mfumuko wa bei na tumepanga ufike kiwango cha asilimia 4 kufikia Juni mwaka huu, lakini vile vile tuna maeneo ambayo yalikuwa yanaachwa wakati wa kuchukua takwimu za pato la taifa, ambavyo sasa yameiingizwa,” alisema.
Alisema maeneo hayo ni kama mapato yatokanayo na matumizi ya sayansi na teknolojia kwa ujumla, kama vile mapato ya kazi za sanaa, matumizi ya mawasiliano ya kielektroniki, kama uhamishaji na utumaji wa fedha.
“Tumepiga hatua kubwa kwenda mbele kimsingi, na ndiyo maana hatupo tena kwenye nchi 10 maskini duniani, ingawaje bado tuna changamoto kama ilivyo kwenye nchi zingine,” alisema.
Salum alitaja mojawapo ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na tatizo la ukosefu wa ajira nchini, na kuwa serikali inachukua hatua za kupambana na tatizo hilo, kwa kuwekeza kwenye kilimo, eneo ambalo linaajiri wananchi wengi nchini.
Alisema katika kuonyesha namna serikali ilivyojipanga kuboresha kilimo ili kitoe ajira kwa wananchi, kilimo ni moja ya vipaumbele vilivyoko kwenye mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Kwa upande mwingine, ripoti hiyo ya WB imezitaja pia nchi tajiri zaidi duniani, zikiongozwa na Luxembourg, ambayo mwananchi wa taifa hilo ana pato la Dola 110,697 na inafuatiwa na mataifa ya Norway, Qatar, Macao, Switzerland na Australia.
Nchi zingine ni Australia, Sweden, Denmark, Singapore na Marekani inayoshika nafasi ya 10 kati ya mataifa tajiri, ambako mwananchi wa taifa hilo ana pato la Dola 53,042.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment