Tuesday, 10 February 2015

MUNGU ALISHAIACHA AFRIKA- BRUCE WILLIS



Muigizaji  wa filamu wa Marekani, Bruce Willis, katika filamu yake kuhusu Afrika, hasa Nigeria ilikofanyiwa uigizaji, ‘Tears of the Sun’, kuna wakati alikuwa akiagwa na mchungaji mmoja mzungu aliyekataa kuondoka eneo la mapigano, akiambiwa, “God be With you” (Bwana awe nanyi); Willis alisita kidogo na baadaye kusema, “God left Africa long time ago.” (Mungu Alisha iacha Afrika kitambo.” Na msaidizi wake, Red, aliunga mkono kwa kusema “Yeah” (ni kweli).


“Tears of the sun” ni kama ilitabiri kinachotokea sasa kati ya wananchi na Boko Haram. Ingawa mrengo na muktadha ni tofauti lakini ukweli ni kwamba kama kuna Mungu basi Boko Haram wanathibitisha kuwa Alisha iacha kitambo. Afrika ni nchi ambapo viongozi, na siyo Boko Haram, Lord Resistance Army, Seleka, au Antibalaka, au Al-Shabaab peke yako, wanaonyesha kuwa Mungu amewakasirikia. Hayupo nao. Na kuwa kuongezeka au makundi yanayoakisi kutokuwapo kwa (neema za) Mungu inatokana na uongozi ambao haumjali Muumba.
Huko Nigeria, wakati wananchi wanaendelea kuuwawa kwa idadi kubwa na Boko Haram wakindelea kuonyesha kutishika, serikali inaendelea na uchaguzi kama vile hakuna kitu kinachotokea, na wanasema huko wanakouawa uchaguzi hautafanyika. Wanauawa kunyimwa haki yao ya kuishi, na wanaambiwa kura nayo siyo haki yao. Viongozi wamepandisha mashetani ya kuwa viongozi, na wanaona kuuawa kwa wananchi wengine sio kigezo cha kutosheleza kuahirisha uchaguzi. Kuwa tatizo hilo ni la watu wa kasikazini, na sie wengine hatumo.
Afrika ilimwasi Mungu, kwani tabia ya kutojali haki za wananchi wenzao ni ishara mojawapo. Familia za viongozi, viongozi wenyewe, maswahiba wao, hawaoni haya kuwalinda waovu wanaoiba mali za umma. Matajri wengi wa Afrika na hasa viongozi,   wanatokana na kuiba fedha za umma ama kudhulumu haki za raia. Grace Mugabe anadaiwa kuua wananchi wenzake kwa kuwaachia wanyama maeneo ambayo wananchi walikuwa wakiishi, ili waondoke na yeye aweze kuanzisha bustani yake ya wanyama kwa ajili ya utalii. Kuna Mungu hapo? Na sidhani kama Grace Mugabe anawaona wananchi hao wanaofukuzwa kikatili kwenye ardhi yao kama nao ni watoto wa Mungu.
Afrika imejawa na viongozi wengi ambao kila uchao wanawaza namna gani watatumia fursa zao za uongozi kujimilikisha utajiri. Kwa sasa hatuioni Afrika ambayo viongozi ni wale wa miaka kabla ya kipindi hiki cha mageuzi ya kiuchumi, ambapo wakati huo (viongozi) walikuwa wakipanga namna ya kuwakomboa Waafrika wenzao kiuchumi. 
Nyakati zile za Jaramogi Odinga Oginga, Nyerere, Kwameh Nkrumah, Murtala Mohamed na Thomas Sankara. Huu ni wa wakati ambapo viongozi wengi huwa wanapanga namna gani watashirikiana wao kwa wao kuitafuna nchi; wanapanga kushirikiana na mafisadi wenzao wa ndani (baadhi ya wafanyabiashara), kuihujumu nchi; wakishirikiana na mashirika ya nje na nchi za nje kutafuta utajiri wetu.
Inanishangaza sana kuona viongozi wakienda kanisani au misikitini, huku jana yake tu wamekuwa wakifanya mikutano ya siri na wanaouza dawa za kulevya, wakijua kuwa taifa lile walilioapa kulilinda dhidi ya uovu ndilo wanaloliangamiza kwa dawa za kulevya. Kwa mfano, unakuwaje waziri unayeahidi ajira 100 halafu jioni unakuwa na kikao na wauza unga? Hizo ajira 100 zitafanywa na nani? Hao vijana hawana kazi, bado unataka kuwadhulumu kidogo wanachokipata kwa kuwauzia dawa za kulevya wasijimudu kabisa. Mungu anaweza kuwa yupo hapo? Kiongozi anaapa kuwa atalinda nchi na watu wake, na vyote vilivyomo. 
Lakini mara baada ya igizo la kiapo, kiongozi anataka kujua wapi atapata soko la siri la dhahabu, meno ya tembo, vipusa, na kadhalika, ili aweze kujitajirisha na kuwalinda walio nje au ndani ya serikali yake. Afrika ilishamuudhi Mungu na yeye ameshaitelekez, na Bruce Willis hajakosea kabisa. Afrika hii ambayo ina utajiri lakini haitaki kuwa tajiri isipokuwa inataka tu viongozi wake pekee wawe tajiri hawana sababu ya kusema Mungu atatujalia! Mungu hawezi kuijaalia nchi ambayo kila uchao viongozi wao wanafikiria namna gani wataifilisi nchi yao. Mungu alishaliacha bara hili.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!