Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Aishael Sumari, ameshtushwa na idadi ya watoto wanaoshikiliwa kwa muda mrefu katika mahabusu kuu ya Mkoa wa Kilimanjaro, wakisubiri kesi zinazowakabili kumalizika ili kuwapa fursa ya kuendelea na masomo waliyokatisha katika Shule za Msingi na Sekondari.
Sumari alipigwa ‘butwaa’, jana asubuhi baada ya kuitembelea mahabusi hiyo, akiwa ameongozana na majaji Amaisairio Munisi, Benedict Mwingwa na Mahakakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi-Moshi.
Baada ya kujionea hali halisi ya mahabusu hiyo, iliyopo chini ya Idara ya Ustawi wa Jamii, Mkoa wa Kilimanjaro, Jaji Mfawidhi, aliwaambia mahabusu hao kwamba, mahakama imeguswa na mahitaji yao na kwamba ameuelekeza uongozi kuwasilisha mara moja kwa Msajili, majina ya watoto wanaosota mahabusu muda mrefu wakisubiri haki.
“Hapa siyo mahali mnapostahili kuwapo; tumejifunza ni kwa sababu gani mmewekwa hapa kwa muda mrefu, ingawa tunajua ni balaa limewapata tu…tunaamini baada ya haki, mtakuwa waadilifu kwa wazazi na hata jamii inayowazunguka,” alisema Jaji Sumari.
Aliongeza: “Nimeuelekeza uongozi wa mahabusu, uniletee majina yenu na kesi zinazowakabili ili tuone namna ya kuwatendea haki na msiendelee kuitwa wahalifu kwani sio jambo la furaha kwenu.”
Majaji hao, Mahakimu na watendaji wengine wa mahakama za mkoa wa Kilimanjaro, walikwenda kuadhimisha siku ya sheria nchini katika mahabusu hiyo pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi kwa kujionea hali halisi na kisha kugawa zawadi mbalimbali zikiwamo viatu, sukari, ndoo, dawa za meno, juisi na vifaa vya usafi.
Awali, akitoa ufafanuzi kuhusu mahabusu hao, Afisa Ustawi wa Jamii (Mfawidhi) wa kituo cha Moshi, Wolfgang Kimaro, alisema idadi kubwa ya mahabusu wanaoshikiliwa ni wanafunzi wa Shule za Msingi ambao bila ya msukumo wa mahakama, wataendelea kusotea haki na kupoteza mwelekeo wa kupata elimu kama taa ya maisha pamoja na makuzi ya walezi au wazazi wao
No comments:
Post a Comment