Ona kioja cha nchi hii; mwalimu wa Kiswahili anafanyiwa usaili kwa lugha ya Kiingereza ili apate kazi. Dereva mzoefu na fundi hodari wa magari anakosa kazi katika mashirika ya umma au yale binafsi kwa sababu hajui Kiingereza.
Katika ujenzi wa ghorofa, mhandisi anayejua Kiingereza anawatumia mafundi wa Kiswahili wasiojua Kiingereza, lakini wana maarifa mapana kuhusu ujenzi.
Kuna wakati anapogundua kafanya kosa anaomba ushauri kwa mafundi haohao na kazi inaendelea kwa ubora stahiki.
Namalizia kioja kingine. Siku moja jirani yangu alijisifu kuwa tangu amhamishe mwanawe shule, sasa anazungumza kimombo si mchezo! Akatumia fursa hiyo kunishawishi na mimi kumhamisha mwanangu.
Nilfikiri angenambia mwanawe huyo ameongeza uwezo wa kusoma, kuandika, kuhesabu au kufikiri, la hasha, anafurahia mwanawe wa miaka minne kujua Kiingereza!
Si yeye, hata mimi mtoto wangu alipoanza chekechea siku ya kwanza alipokutana na mimi usiku na kunambia ‘Good morning madam’, japo alikosea salamu hiyo nilifurahi kuona anazungumza Kiingereza.
Ukweli ni kwamba fikra kuwa Kiingereza ndiyo kila kitu zimetuzonga Watanzania. Wengi hatuamini kama elimu na maendeleo vinaweza kupatikana bila kutumia lugha hiyo.
Ni kasumba tu tuliyonayo Watanzania, ndiyo maana ni kawaida hata kwenye mikusanyiko ya Waswahili watupu, washiriki wanaulizana watumie Kiingereza au Kiswahili.
Walipo Waswahili 200 na mzungu mmoja, watu watajiumauma na Kiingereza. Kisa, wamridhishe mgeni mmoja.
Eti msomi aliyezaliwa na kukulia Kariakoo anadai hawezi kuandika mada kwa Kiswahili!
Wanaowasilisha mada kwa Kiswahili nao wanajiona wana kasoro, hawajaiva kimaarifa kama wenzao ‘wanaotiririka’ kwa Kiingereza.
Nimeshawahi kuhudhuria mkutano fulani, mgeni mzungu ilibidi atoe ruhusa watu wazungumze Kiswahili kwa kuwa washiriki tungekuwa wazi na huru kuzungumza kilichokuwa kikijadiliwa. Ikumbukwe mada iliyokuwa ikijadiliwa ilihusu maendeleo yetu sisi Waswahili na siyo maendeleo ya mzungu huyo mgeni.
Wataalamu wa sayansi ya lugha wanatufahamisha kuwa matumizi ya lugha kwa watu wasio na umahiri nayo, yanaweza kukwaza ujumbe kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Hiki ndicho kinachojiri katika mikusanyiko mingi ambayo washiriki wanang’ang’ania kutumia Kiingereza bila ya kujali kuwa kwa kufanya hivyo wanafifisha uelewa kwa wengine.
Kibaya zaidi, leo kujua Kiingereza kunatumika kama hoja ya kumkuza mtu. Mjuzi wa Kiingereza hata kama kichwani hana kitu anaonekana msomi.
Tusiojua Kiingereza au tunaokitumia kwa kutafuta maneno tunasimangwa, tunaonekana ni kichekesho au hatujasoma. Mhitimu wa uhandisi wa chuo kikuu ‘anapondwa’ kwa kuwa hajui Kiingereza.
Pamoja na kuwa na maarifa na ujuzi, mhandisi huyu anaweza kukosa kazi kwa kushindwa usaili wa Kiingereza. Wengi utawasikia wakiwananga wahitimu wa vyuo vikuu vyetu kuwa wanashindwa japo kuandika barua kwa Kiingereza.
Tunawahukumu wahitimu wetu sio kwa kuwa hawana maarifa, bali kwa kutojua kuandika barua ya Kiingereza! Ndiyo maana vijana wanakosa ajira sio kwa sababu hawajui walichosomea bali hawana mbwembwe za ‘is and was’.
Nakiri na ndivyo ukweli ulivyo kuwa Kiingereza ni ‘Kiswahili cha dunia’, lakini siamini kama bila lugha hiyo maisha na maendeleo haviwezi kupatikana.
Ingekuwa hivyo Wafaransa, Warusi, Wachina, Wajapan wangekuwa tegemezi kwa mataifa yanayozungumza Kiingereza.
Sawa tujihimu kukifahamu Kiingereza kitusaidie katika biashara za kimataifa na mengineyo lakini hatuna budi kuimarisha lugha yetu.
Hakuna nchi iliyoendelea duniani kwa kuiga utamaduni wa mwenzake. Ubunifu, ugunduzi na uvumbuzi ambavyo ndiyo chachu ya maendeleo haviji kwa kutumia lugha ya kukopa.
Hata hivyo, utashi wa kukithamini Kiswahili uanzie kwa viongozi wetu. Wiki iliyopita niliandika nikasema ni aibu ilioje wageni wazungumze kwa lugha zao wakiwa katika ardhi ya Tanzania ilhali wenyeji tung’ang’anie kuzungumza lugha za kigeni nyumbani.
Fahari ilioje kwa mtu kuzungumza lugha yake ndani ya ardhi yake? Kiswahili kikipendwa na viongozi kitapendwa na wananchi na matokeo ya kupendwa ni kuendelezwa na hatimaye kuwa nguzo ya maendeleo ya nchi. Hivi ndivyo ilivyo kwa Kichina kwa Wachina, Kirusi kwa Warusi, Kifaransa kwa Wafaransa. Mifano ni mingi, nikomee hapa.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment