Monday, 9 February 2015

KAULI YA OBAMA KUHUSU UKRISTO YAZUA KIZAAZAA!

Kauli ya Rais Barack Obama ya kuwataka Wakristo kujua kuwa Uislamu si dini pekee inayohusishwa na vurugu na mauaji, imezua kizaazaa duniani na baadhi wameanza kuhoji kama kiongozi huyo wa kwanza mweusi wa Marekani ni Mkristo.

Obama alitoa kauli hiyo Jumatano wakati wa Siku ya Taifa ya Maombi (National Breakfast Prayer) alipofananisha Vita vya Msalaba na vitendo vya ugaidi vinavyofanywa na vikundi vya Kiislamu vyenye imani kali.
“Hadi tutakapokuwa juu ya farasi na kufikiri kuwa jambo hili ni la pekee kwa baadhi ya sehemu, kumbuka kwamba wakati wa Vita Vitakatifu (crusades) na Mahakama ya Kanisa Katoliki (Inquisition), watu walifanya vitendo vya kutisha kwa Jina la Kristo,” Obama alikaririwa na Shirika la Habari la AFP akizungumza kwenye hafla hiyo Jumatano.
 “Na katika nchi yetu, utumwa na sheria za kibaguzi (Jim Crow), zote pia zilihalalishwa kwa jina la Kristo.”
Obama alikuwa akitoa hotuba yake kuhusu dini kwenye hafla hiyo iliyofanyika Washington, D.C. Akitumia maandiko ya dini za Kiislamu, Kiyahudi na kikristo, Obama alisifu imani yake.
“Utamaduni wa maombi umetuweka pamoja, ukitupa nafasi ya kukusanyika kwa unyeyekevu mbele ya Mungu na kutukumbusha nini kinatakiwa kushirikiana kama watoto wa Mungu,” alisema.
Obama pia aliwageukia magaidi wa kijihadi aliosema “wanaasi Uislamu”. Alilinyooshea kidole kundi la Islamic State ambalo alisema “limefanya vitendo visivyoweza kutamkwa vya ukatili “ Mashariki ya Kati pamoja na wanamgambo ambao hivi karibuni waliua watu kadhaa kwenye ofisi za gazeti la vibonzo la Charlie Hebdo nchini Ufaransa.
Lakini kauli yake imekosolewa sehemu mbalimbali.
Katibu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Padri Saba Raymond alisema alichozungumzia Obama ni historian a hivyo dunia inatakiwa ijifunze.
“Kama kimetokea, kimetokea. Tunatakiwa kujifunza kutokana na kilichotokea. Katika ulimwengu wa sasa ni fursa ya kujifunza yale yaliyotokea na hayafai na wakati huu yasitokee tena... wale wanaoyataka, washindwe,” alisema Padri Raymond
Padri Raymond aliongeza kusema: “Utumwa ulikuwa haufai na Marekani walijihusisha kwa hili (kuuondoa) na hii ni historia ambayo wanapaswa kuiacha.”
Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho alisema:” Ni kauli ya kujihami na anaogopa kuwanyooshea kidole moja kwa moja... Wamarekani wasingependa yatokee kama yaliyowahi kutokea huko nyuma.
“Hili ni suala nyeti na gumu sana, matuko mengi yamekuwa yakitoke hivi karibuni ya kuchinja watu kama Nigeria, Misri na kwingineko... Obama anachukua tahadhari ili akiondoka madarakani Wamarekani wasianze kumtuhumu kwa kusababisha maafa.”
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisita kidogo kuzungumzia suala hilo moja kwa moja kutokana na kutojua mazingira ambayo rais huyo wa taifa kubwa duniani aliyotumia kutoa kauli hiyo.
“Sijajua kwa nini ametoa kauli hiyo na wakati huu kwani hata hao wanaotekeleza vitendo vya kigaidi ni watu ambao si wa kawaida... ni kauli ambayo bado sijajua ina maana gani.”
Nchini Marekani, mtangazaji wa kituo cha televisheni cha MSNBC, Joe Scarborough hakuamini kauli hiyo ya Obama.
“Ni kitu usichoweza kuamini,” alisema mtangazaji Scarborough. “Wakati mwingine unaweza kusema tu, ‘Hey, unajua? Kuna Waislamu wenye imani kali ambao ni wabaya, wabaya kweli.’”
Wahafidhina nao walieleza kuchukizwa na kauli ya Obama.
Gavana wa zamani wa Virginia nchini Marekani, Jim Gilmore alisema kauli ya Obama ni “ya uchochezi ambayo haijawahi kutokea” maishani mwake.
Na televisheni ya Fox News ilitoa kipande baada ya kipande cha hotuba hiyo na kujadili.
“Mtu huyu hana maana, mbinafsi na mweye mambo yaliyopita kiasi,” mtangazaji wa kipindi cha mazungumzo ambaye ni mhafidhina, Mark Levin aliiambia Fox.
Levin alieleza kuwa kama rais wa zamani wa Marekani, Abraham Lincoln angefuata msimamo wa Obama, angeachia utumwa uendelee.
“Lincoln angesema, kutokana na hoja ya Obama, Msishuke kwenye farasi wenu. Hili siyo tishio lililopo,’” aliongeza Levin. “Lincoln angeweza kusema, ‘Kwa nini natuma duniani maelfu ya watu waende kwenye vifo ili waondoe utumwa?’Anachosema Obama ni kibaya kuliko vyote.”
Akihojiwa na ABC News, mwanahistoria wa Chuo Kikuu cha St. Louis, Thomas Madden alisema: “Sidhani kama rais anaelewa vizuri vita vitakatifu,” alisema.
“Anaonekana anaelezea kama mfano wa upotoshaji wa Ukristo na kujaribu kulinganisha na upotoshaji wa Uislamu kutokana na vitendo vya ISIS,” alisema Madden. “Lengo la awali la vita vitakatifu lilikuwa ni kurejesha kwa Wakristo ardhi iliyokuwa imetekwa kutokana na ushindi wa Waislamu.”
Vita vitakatifu, ambavyo vilianza mwaka 1095 kwa wito wa Papa Urban ll wa kutaka kuirejesha Jerusalem kutoka kwa Waislamu, ilikuwa na matukio kadhaa yaliyodumu kwa karne mbili. Ingawa hakuna makadirio yanayoaminika yaliyosababishwa na vita hivyo, zaidi ya Waislamu 2,700 waliokuwa wafungwa waliuawa kwa pamoja na Richard the Lionheart nje ya Acre wakati wa vita ya tatu ya Crusaders na tukio hilo linakumbukwa Mashariki ya Kati hadi leo.
MWANANCHI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!