ZAIDI ya Watanzania 1,200 wanatarajiwa kuajiriwa kwenye Kampuni ya Kuchezesha Bahati Nasibu ya Afrika Kusini Murharndziwa itakayoanza kufanya shughuli zake nchini kuanzia Julai, Mwaka huu.
Akizungumza jana kabla ya kukabidhi leseni kwa Kampuni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Bahati Nasibu Taifa Abbas Tarimba alisema kutokana na Kampuni hiyo kuwa na vifaa vya kisasa inategemea kuajiri Watanzania 200 kwa ajira za moja kwa moja na 1,000 ambao ni mawakala.
Alisema pia, Serikali itanufaika na fedha za uwekezaji katika mwaka wa kwanza ambapo itapata Sh bilioni 56 na itakuwa ikitoa kodi Sh bilioni kwa mwaka wa kwanza Sh bilioni 40.
“Kampuni hii kabla ya kuipa leseni tuliichunguza kwa kushirikiana na Mtandao wa Polisi wa Kimataifa (Interpol) kujua imepata wapi fedha za kuendesha mchezo huo, tukajiridhisha na kuipa nafasi kwa mujibu wa sheria namba 41 ya bahati nasibu, tunategemea Watanzania wengi watanufaika,” alisema.
Tarimba alisema kampuni hiyo inatarajiwa kufanya kazi kwa kipindi cha miaka mitano ambapo kwa sasa imepewa muda wa miezi mitano kwa ajili ya kufunga mitambo yake na kuendelea na mchakato wa ajira kuwapata wale wanaowahitaji.
Alisema mchezo huo utaendeshwa nchi nzima ambapo tiketi ya kwanza itauzwa rasmi kuanzia Julai 4, ambayo itakuwa ni siku ya uzinduzi na kwamba zawadi ya kwanza itakuwa ni Sh bilioni moja.
Alisema michezo ambayo watakuwa wanaendesha ni Loto, kutabiri michezo ya kimataifa na mingine mipya itakayotambulishwa siku ya uzinduzi rasmi.
Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya Kimataifa ya Gidani na Murhandziwa Professa Bongani Khumalo alisema ujio wa kampuni hiyo ya pili kwa ukubwa barani Africa unategemewa kuleta manufaa kwa nchi na Watanzania kwa ujumla waliopo katika sekta rasmi na waliopo katika sekta zisizo rasmi yaani wafanyabiashara binafsi.
No comments:
Post a Comment