Tuesday, 10 February 2015

JINSI YA KUJIWEKEA MAZINGIRA BORA YA MAFANIKIO KIMAISHA

Baada ya kujua namna ya kuishi na kuongozwa na malengo, leo tunajifunza juu ya faida ya kuweka malengo na hata namna ya kutumia muda wako kikamilifu.

Moja ya faida ya malengo ni kwamba hutulazimisha katika kuufikia mpango tulioupanga kwa muda muafaka.
Pili, hutuwezesha kutambua uwezo na jitihada zetu na hii hutupa ujasiri katika kulifikia lengo na tatu, hutuwezesha kuweka mtazamo wetu kwenye matokeo, na sio tu kuwa wenye bidii hewa.
Tujifunze ni jinsi gani ya kuutumia muda kiufanisi ili kufikia malengo ambayo tayari tumejipangia.
Jitambue kama wewe ni mtu wa asubuhi, mchana au usiku. Kuna watu ambao wanaweza kufanya kazi kiufanisi wakati wa asubuhi, wengine mchana na wengine usiku.
Jitahidi kuweka zile kazi bora na za muhimu katika muda ambao wewe unakuwa makini zaidi. Hii itakusaidia kuukomboa muda na kuutumia kiufanisi zaidi.
Fahamu jinsi unavyoutumia muda wako na ni mazingira gani yanayokupotezea muda wako kwa kujua au kwa kutokujua.
Panga ni muda gani unafaa kufanya kazi zenye ubora na ni upi wa kufanya kazi laini. Mfano kusoma, kuhesabu fedha, kupasi, kufua, kupanga vitu na kadhalika.
Kula chakula bora ili kuongeza ubora na uwezo wa kufikiri na hivyo kusaidia kuzalisha vilivyo bora zaidi.
Ruhusu mwili na akili yako kupumzika baada ya kiwango fulani cha kazi. Wengi wetu hatuna muda wa kupumzika na hata zinapokuja nyakati za likizo, wengine huziuza likizo zao kwenye ofisi au kampuni zao. Tusidhani waliogundua kuwepo kwa likizo walikuwa wajinga. Mwanadamu wa kawaida anahitajika kupata mapumziko baada ya kiwango fulani cha kazi.
Wenzetu wa nchi za magharibi wanaamini katika usemi usemao “rest is not a west of time”, wakiwa na maana; kupumzika siyo kupoteza muda bali ni maandalizi ya muda bora zaidi wa baadaye.
Angalizo. Hapa sizungumzii wale wanaopenda kutumia muda mrefu kupumzika tu pasipo kufanya kazi. Hilo ni tatizo.
Epuka kulundika kazi au majukumu hadi yawe ya lazima kufanywa. Panga au jiwekee muda wa kumaliza kazi hizo. Jipangie za muda mfupi na mrefu ili kukuwezesha kumaliza kazi zako mapema.
Usipende kufanya kazi katika shinikizo “pressure” kwasababu hata kama utaimaliza hiyo kazi lakini ubora au ufanisi wake hautakuwa wa kuridhisha. Jitengenezee muda mrefu zaidi kwa ajili yako mwenyewe, kwa kugawanya majukumu kwa wengine.
Ningumu sana na haishauriwi kufanya kila kitu mwenyewe. Katika kugawa majukumu, ni vema tukijifunza kugawa kazi sahihi kwa mtu sahihi kwa maana yawezekana kabisa kazi sahihi ikapewa mtu asiye sahihi au kazi isiyo sahihi ikapewa mtu sahihi na kwa hali zote hizi matokeo lazima yatakuwa mabaya.
Namna nyingine ya kujitengenezea muda wa ziada katika maisha yako ya kila siku ni kwa kujaribu kuamka mapema zaidi kuliko kawaida.
Mfano, umezoea kuamka saa moja na kufika ofisini saa mbili kila siku na wakati huo unalalamika muda hautoshi na majukumu ni mengi, ni vema ukijitahidi kuamka mapema zaidi ili ikiwezekana uwepo ofisini saa moja.
Saa moja ya ziada itakayoongezeka itakusaidia sana kupunguza baadhi ya kazi na mzigo utapungua taratibu.
Wakati wowote na katika mazingira yeyote tunatakiwa kukumbuka kuwa, mtu asiyekuwa na lengo basi ana lengo la kufeli na kutofanikiwa “Not having a plan is a proper plan to fail”
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!