Monday, 9 February 2015

HITILAFU YA UMEME NDIO CHANZO CHA AJALI YA MOTO ILIYOTEKETEZA FAMILIA JIJINI DAR



Moto ulioteketeza nyumba na ndugu sita wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya, jijini Dar es Salaam umeelezwa kuwa ulisababishwa na hitilafu ya umeme.
 
Taarifa zilizopatika eneo la tukio jana, zinasema moto uliopelekea vifo hivyo umesababishwa na hitilafu ya umeme iliyoanzia kwenye mita, kisha kuenea kwa kasi nyumba nzima.
 
Msemaji wa familia, Godfrey Mwandosya, alisema kulitokea hitilafu ya umeme katika mita iliyokuwa ndani ya nyumba hiyo na kusababisha moto kusambaa kwa kasi jambo lililowazuia marehemu kujiokoa.
 
“Haikuwa rahisi kujiokoa kwa sababu moto ulipoanza kwenye mita, ulisambaa kwa kasi kutoka eneo moja hadi lingine,” alisema Mwandosya.
 
Alisema kama familia wamepata pigo baada ya kupoteza watu sita kwa mara moja, kitu ambacho kimewafanya kuchanganyikiwa.
 
“Tuliposikia kila mtu hakuamini jambo hili, hadi tulipofika hapa ndipo tulipoamini kweli hatuna ndugu tena, ni hali ya kushtua hasa kwa watu ambao hawakuwa wanaumwa unaposikia wamekufa pamoja,” alisema kwa majonzi.
 
Baadhi ya marafiki wa marehemu, Lucas Mpila (30), walisema enzi za uhai wake alikuwa na uwezo mkubwa wa kumbukumbu na kuchambua mambo mbalimbali kiasi cha kumpa jina la ‘Google.’
 
Mmoja wa rafiki yake mkubwa, Gerald Mkasoya, alisema Lucas alikuwa na msaada mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na tabia yake ya kusaidia na kuelimisha jamii katika masuala mbalimbali.
 
Alisema kutokana na kipaji chake, walimchagua kuwa mweka hazina wa kundi lao la kijamii la SOG, ambapo aliongoza kwa uadilifu hadi kifo.
 
“Kabla ya tukio hili, tulitumiana ujumbe kupitia simu zetu za mikononi kwa ajili ya vikao vyetu, lakini asubuhi nilishtuka nilipoambiwa Lucas na familia yake wamekufa kwa moto, ni jambo ambalo hatuliamini kabisa,” alisema Mkasoya.
 
Rafiki yake mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema siku moja kabla ya tukio hilo alimfuata na kumuomba ushauri juu ya ugonjwa wa ndugu yake Emmanuel, ambaye alinusurika katika tukio hilo.
 
Alisema anaona uchungu kumuona mdogo wake anapata shida kwa kuugua, hivyo anafikiria kumpeleka hospitali kesho yake.
 
Katika hatua nyingine, marehemu Lucas alijaribu kuwaokoa watoto na aliposhindwa aliwakumbatia na kisha kufa pamoja.
 
Kwa mujibu wa Justine Faustine, ambaye ni rafiki wa familia na kiongozi wa Jumuia ya Kikatoliki eneo hilo, alisema mwili wa marehemu ulikutwa chumba cha watoto huku akiwa amewakumbatia.
 
“Tunaamini kabisa Lucas alifanya juhudi ya kujikoa yeye na watoto, kwani mwili wake tuliukuta chumba cha watoto akiwa amewakumbatia, ni jambo la kusikitisha sana,” alisema Faustine.
 
MAZIKO 
Kwa mujibu wa Mwandosya, maziko ya marehemu hao yatafanyika kesho katika makaburi ya Airwing Ukonga na kwamba misa ya kuwaombea marehemu na shughuli ya kuaga itaanza saa 7:30 mchana hadi 9:00 alasiri.
 

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!