Thursday, 5 February 2015

BOBBY CHRISTINA YALE YALE YA WHITNEY


Los Angeles, Marekani. “Maji hufuata mkondo,” walisema Waswahili. Ndivyo unavyoweza kumwelezea Bobby Kristina, mtoto wa aliyekuwa nguli wa miondoko ya muziki wa Pop Whitney Huston aliyepoteza maisha kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Binti huyo naye sasa amelazwa hospitali baada ya kukutwa amepoteza fahamu ndani ya jakuzi, huku habari zikieleza kuwa alikuwa ametumia dawa za kulevya.
Kifo cha mama wa binti huyo, Whitney kilitokea katika mazingira kama aliyokutwa nayo.
Tofauti kati ya matukio hayo ya mama na mwana ni kwamba Whitney alikutwa ameinamisha kichwa ndani ya maji akiwa ameshafariki, lakini Bobby alikutwa amezirai akiwa katika mazingira kama hayo.Siku 10 baada ya kifo cha Whitney, tovuti ya TMZ ilitoa habari kuwa binti yake Bobby Kristina naye anatumia dawa za kulevya na kwamba hawezi kujitokeza mbele za watu bila kuzitumia.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa ndugu wa familia ya Houston wanasubiri mazishi Whitney ili wampeleke Bobby kwenye kituo maalumu cha kupambana na matumizi ya dawa za kulevya.
Kwa tukio la juzi, tovuti ya CNN iliarifu kuwa binti huyo wa mwanamuziki Bobby Brown alifikwa na hali hiyo mwishoni mwa wiki huku ndugu yake wa karibu akimweleza mwandishi wa tovuti hiyo, Sunny Hostin kwamba baada ya kugonga mlango mara kadhaa bila majibu, alipata shaka na kuingia ndani na kumkuta Bobby katika hali hiyo na kupiga simu polisi, ambao walifika na kumkuta akiwa na hali mbaya kisha kumpeleka katika Hospitali ya North Fulton.
Msemaji wa Polisi, Lisa Holland aliiambia tovuti hiyo kuwa walipofika walimkuta Bobby hapumui, lakini baada ya kufikishwa hospitali na kupatiwa huduma ya kwanza alianza kupumua, ingawa alikuwa hajitambui.
Tovuti ya TMZ imeripoti kuwa baada ya Polisi kufanya ukaguzi walikuta dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa TMZ, siku moja kabla ya tukio Bobbi Kristina alikuwa na rafiki yake Maxwell Byron Lomas, ambaye mwezi mmoja uliopita alikamatwa kwa kusambaza dawa za kulevya na kuwekwa chini ya ulinzi na baadaye aliachiwa kwa dhamana.
Taarifa kutoka Polisi zinazoandikwa katika jarida la Fulton County Jail records zinasema Lomas amekuwa akihusishwa na kashfa ya dawa za kulevya kwa muda mrefu na siku moja kabla ya tukio hilo alikuwa na Kristina pamoja na mumewe Gordon.
Ilivyokuwa kifo cha Whitney
Whitney Huston alifariki dunia Februari 11, 2012 katika Hoteli ya Beverly Hilton jijini Los Angeles, saa chache kabla ya kufanya onyesho kwenye sherehe za maandalizi ya Tuzo za Grammy.
Mkuu wa Polisi wa Beverly Hills, Luteni Mark Rosen alithibitisha kukutwa kwa aina fulani ya vidonge vya kutuliza maumivu katika chumba alichofia mwanamuziki huyo, huku kukiwa na ushahidi kuwa alikuwa akitumia dawa za kulevya baada ya kushindwa kutumbuiza jukwaani mara kadhaa na kukaa kimya ‘akisikilizia’ kama wafanyavyo mateja.
Whitney ambaye alikuwa gumzo miaka ya 1980 na 1990 kutokana na sauti yake ya kumtoa nyoka pangoni na baadaye kwenye ushiriki wake katika filamu za ‘The Body Guard’ na ‘Waiting to Exhale’ aliwahi kukaririwa akisema baada ya kuanza kuyumba kwa afya yake: “Nina shetani mkubwa ananiandama, kama siyo marafiki zangu, basi ni maadui zangu au ni akili yangu inayonituma kufanya vitu ambavyo vitagharimu maisha yangu.”

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!