Wednesday, 18 February 2015

AJIRA 41,000 KUZALISHWA NDANI YA MIEZI MITATU INATIA MOYO



HABARI kwamba ajira 40,735 zilizalishwa ndani ya miezi mitatu kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka jana na kufanya jumla ya ajira 173,787 kupatikana kwa kipindi cha nusu mwaka kuanzia Julai hadi Desemba kwa kweli zinatia moyo.


Tunasema zinatia moyo kwa sababu, kilio kikubwa kwa Tanzania hasa vijana, ni suala la ajira. Suala la ajira limekuwa ni tatizo sugu ikizingatiwa kwamba vijana wengi wanapomaliza elimu katika ngazi zote kuanzia msingi, sekondari hadi vyuo vikuu wapo mitaani wakisaka kazi.
Kabla ya kuruhusu sekta binafsi katika kutoa ajira, Serikali ilikuwa ikilemewa na mzigo katika kuandaa vijana wake kuhakikisha wanasoma, na wakimaliza, kutafuta nafasi chache za kazi, lakini kuwepo kwa sekta binafsi katika mfumo wa ajira, umeipunguzia kazi Serikali, hivyo kuwezesha kupatikana kwa nafasi hizo zilizotajwa na nyingine nyingi.
Katika kufafanua suala hili, Wizara ya Kazi na Ajira inasema ongezeko hilo la ajira limejitokeza katika maeneo makuu mawili; ikiwemo ajira serikalini ambazo ni 2,652 sawa na asilimia 6.5 na ajira kupitia sekta binafsi ambazo ni 38,083 sawa na asilimia 93.5.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi Dar es Salaam, Msemaji wa Wizara hiyo, Ridhiwan Wema alisema takwimu hizo zinaonesha kwamba sekta binafsi imeendelea kuwa mhimili wa uzalishaji wa ajira nchini kutokana na serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya waajiri kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.
Akasema katika kipindi cha nusu mwaka, sekta binafsi rasmi ambayo ndiyo mwajiri mkuu ilizalisha ajira 173,787 kupitia uwekezaji binafsi ambapo uwekezaji kupitia ujenzi zilizalishwa ajira 107,527, uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) ajira 34,184 na Sekta ya Mawasiliano ajira 342.
Pia akasema hatua zinazochukuliwa kwa sasa ni pamoja na kufanya marekebisho ya Sera ya Ajira ya 2008, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6,2004, Sheria ya Taasisi za Kazi namba 7,2004 pamoja na kutunga sheria Mpya ya Ajira za Wageni ambayo imelenga kulinda ajira za Watanzania, kuboresha mazingira ya biashara na kuhamasisha uwekezaji.
Akasema taarifa hizi zimelenga kuiwezesha Serikali kujua hali ya ajira nchini na kuchukua hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kuwezesha Serikali kupanga matumizi sahihi ya nguvu kazi nchini.
Akasema taarifa hizo ni miongoni mwa vigezo vikuu vinavyotoa picha halisi ya mafanikio ya kiuchumi na kimaendeleo kwa nchi au mahali husika na zinasaidia kupanga, kutekeleza na kupima ufanisi wa mipango ya kiuchumi nchini pamoja na kupima uwezo wa kiuchumi katika wakati husika.
Tunaamini, makusudi ya Serikali yataiwezesha nchi kutatua tatizo hili la ajira ambalo limekuwa likiimbwa kila kukicha na Mungu bariki, Watanzania walio wengi watafikiwa.

HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!