Friday, 23 January 2015

WALIOMCHINJA KATIBU WA CCM KAHAMA WAKAMATWA

Mwili wa marehemu  Daudi Lusalula Mbatiro(56) baada ya kuchinjwa Desemba 5,2014-Picha kutoka maktaba ya malunde1 blog




 Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha
 
Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kunasa mtandao wa watu wanaojihusisha na vitendo vya mauaji ya watu kwa kuchinja kwa visu,ikiwemo tukio la mauaji ya Katibu  wa Chama Chama Mapinduzi kata ya Mwalugulu wilayani Kahama mkoani Shinyanga Daudi Lusalula Mbatiro(56) aliyeuawa kwa kuchinjwa kama kuku mwaka jana kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa

Tukio la kuuawa kwa katibu huyo wa CCM lilitokea Desemba 5,2014 saa mbili usiku wakati katibu huyo wa CCM kata ya Mwaluguru ambaye pia alikuwa ni katibu wa elimu,malezi na mazingira baraza la wazazi wa CCM wilaya ya Kahama akitokea kata ya Kagongwa kwenda nyumbani kwake  Sungamile baada ya  kutoka kwenye mkutano wa chama chake uliokuwa unafanyika mjini Kahama.

Waliotajwa na jeshi la polisi kuhusika katika mtandao huo ni pamoja na diwani wa kata ya Mwalugulu wilayani Kahama Bundala Kadilanha(CCM),mfanyabiashara wa Kagongwa Tobo Mwanasana,pamoja na Emmanuel Maziku,Masanja Shepa,Samwel Seni Budugu na Shija Shepa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha alisema katika uchunguzi wa mauaji ya katibu wa CCM kata ya Mwalugulu Daudi Mbatiro jeshi la polisi limewakamata watuhumiwa Emmanuel Maziku na Masanja Shepa na baada ya kuhojiwa walikiri kuhusika na mauaji hayo.

Alisema baada ya kuwahoji watuhumiwa hao wawili,waliwataja wahusika wengine ambao ni Bundala Kadilanha(diwani wa Mwalugulu),Tobo Mwanasana(mfanyabiashara,Samweli Seni Budugu  mkazi wa Mwakitolyo na Shija Shepa mkazi wa Mwalumba Kahama.

Alisema awali jeshi la polisi baada ya kupata taarifa za watu hao liliweka mtego kwa kuwapigia simu ili kuwakodi kufanya mauaji katika kijiji cha Nyindu  na kufanikisha kuwakamata watu hao ambao hujihusisha na matukio mbalimbali ya mauaji.

Alisema baada ya kuwafanyia mahojiano watu hao wawili walikiri kuhusika na matukio ya mauaji katika mkoa wa Shinyanga na Tabora kwa kukodiwa ili kuchinja watu kwa kisu na wao sio wakata mapanga ingawa wanaua vikongwe na kulipiza kisasi.

Kamanda Kamugisha alisema watuhumiwa walisema kiongozi wao ni Samweli Seni Budugu na wenzake ni Tobo Mwanasana,Bundala Kadila na Shija Shepa na kabla ya mauaji hayo wanaenda kupakwa dawa kwa waganga wao wa jadi ambao ni John Shija mkazi wa kijiji cha Lyabukande na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Tabu mkazi wa Kizungu.

Kamanda Kamugisha alisema watuhumiwa wote wamekiri kuhusika na matukio ya mauaji ya marehemu Ngolo Sakumi(69) mkazi wa Mwalugulu na walikodiwa kwa shilingi 1,000,000/= aliyewakodi ni Jikuba Kajile na Lukuba Nangi.

Tukio jingine walilokiri kuhusika ni mauaji ya Mary Seleman Masenya(45) mkazi wa kijiji cha Matinje na walikodiwa kwa shilingi 800,000/= na wanawake watatu ambao ni wake wenza wa marehemu.

Alitaja tuko jingine walilohusika ni lile la mauaji ya Mboje Seni(70) mkazi wa kijiji cha Butondo na walikodiwa kwa shilingi 800,000/= walikodiwa na Mwanabundi mkazi wa Butondo na tukio jingine ni mauaji ya Kwigema Lubinza(60) mkazi wa kijiji cha Kakulu kata ya Nyahanga.

Kamanda huyo alisem jeshi la polisi linaendelea na msako wa kuwakamata wahusika wengine wa matukio hayo ikiwa ni pamoja na waganga wa kienyeji waliohusika huku akiwataka wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika wote wa mauaji ya kukodiwa na mauaji ya vikongwe ili kukomesha kabisa mauaji hayo.
Na Kadama Malunde-Shinyanga

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!