Friday, 2 January 2015

VYAMA 10 VILISIVYO NA UWAKILISHI BUNGENI VYAWATAKA VIONGOZI WA DINI KUTOJIHUSISHA NA SIASA

 Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kwa niaba ya vyama 10 visivyo na uwakilishi wa wabunge Bungeni wakati wakitoa tamko kuhusu viongozi wa dini kutojihusisha na masuala ya siasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu 2015 . Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa Chama cha Sauti ya Umma (Sau), Ali Kaniki na Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima Tanzania (AFP), Rashid Rai.
 Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima Tanzania (AFP), Rashid Rai (katikati), akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Naibu  Katibu Mkuu wa Chama cha UMD, Moshi Kigundula na Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi.
 Katibu Mkuu wa Chama cha Sauti ya Umma (Sau), Ali Kaniki (kulia), akizungumza katika mkutano huo kuhusu suala zima la Nishati ya umeme nchini na sakata la Escrow. Kushoto Kiongozi wa chama cha Jahazi Asilia Mbwana Kibande na Amina Mcheka kutoka chama cha Chausta.
 Naibu Katibu Mkuu wa wa Chama cha UPDP, Felix Makuwa (kulia), akichangia jambo kwenye mkutano huo.
 Mwakilishi kutoka chama cha Chausta, Amina Mcheka akitoa ufafanuzi wa masuala kadhaa katika mkutano huo.
 Mwakilishi kutoka chama cha Jahazi Asilia, Mbwana Kibande (kushoto) naye akichangia jambo kwenye mkutano huo.
 viongozi wa vyama hivyo wakiwa kwenye mkutano huo.
Wanahabari wakichukua taarifa hizo.
…………………………………………………………………………….
 
Dotto Mwaibale
 
VYAMA kumi visivyokuwa na uwakilishi bungeni vimewaonya  viongozi wa dini nchini katika kipindi cha mwaka huu ambako kutafanyika uchaguzi mkuu kutojihusisha na masuala ya siasa kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na katiba ya nchi.
 
Aidha, vyama hivyo vimeitaka serikali kupitia upya mikataba ya makampuni yanayozalisha umeme nchini kwa kuwa baadhi yanauza nishati hiyo kwa gharama kubwa licha ya kwamba baadhi yanazalisha umeme kwa kutumia gesi na kusababisha wananchi kuingia gharama kubwa.
 
Tamko hilo limetolewa na makatibu wakuu wa vyama vya AFP, CCK, SAU, UMD, Chausta, UPDP, NRA, Jahazi, Chauma na DP ikiwa ni salamu za kukaribisha mwaka mpya wa 2015.
 
Katibu Mkuu wa AFP, Rashid Rai, akisoma tamko hilo jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya wenzake, alisema katika miaka ya hivi karibuni kumejitokeza tabia ya viongozi wa dini kujihusisha na masuala ya siasa hususani kipindi cha uchaguzi mkuu na hivyo kuwachanganya wananchi.
 
Rai alisema viongozi hao wamekuwa wakitoa matamko kwenye vyombo vya habari kupendekeza au kutoa sifa ya kiongozi anayefaa kuongoza nchi au asiyefaa kupewa nafasi ya uongozi wa umma katika Taifa.
 
Alisema viongozi wa dini lazima watambue kuwa sheria inazuia viongozi wa dini kujihusisha na masuala ya siasa kwani hali hiyo inawachanganya wananchi kushindwa kujua kama viongozi hao wamebadilisha majukumu yao.
 
“Unakuta kiongozi wa dini anasema Rais ajaye awe ni mwadilifu na mcha Mungu, au anasema  kiongozi huyu ni chaguo la Mungu, maana yake ni nini,kila dini au dhehebu lina vigezo vyake vya uadilifu na ucha  Mungu,”alisema.
 
Rai alisema kama viongozi wa dini wanaona watu waliopo kwenye siasa wanafaidi sana ni bora wakaachana na masuala ya kuhubiri dini badala yake waanzishe vyama vya siasa au wajiunge na vyama vya siasa ili waendelee kupata neema wanayohisi inapatikana huko.
 
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha SAU, Ali Kaniki, alisema sakata la akaunti ya Tegeta Escrow limetoa fundisho kwa serikali kuona umuhimu wa kupitia upya mikata ya makapuni yote ya makampuni yanayozalisha umeme.
 
Alisema baadhi ya makampuni yanayozalisha umeme na kuliuzia Shirika la Umeme nchini (Tanesco) yanatoza tozo kubwa hali ambayo imekuwa ikisababisha gharama za umeme kuwa kubwa hapa nchini.
 
“Tunayo makampuni yanayozalisha umeme hapa nchini ambayo ni Songas, IPTL Aggreko na Symbion, ukiangalia yote IPTL ndiyo inayouza umeme kwa bei ndogo ukilinganisha na mengi, tunataka serikali ipitie mikataba ya makampuni haya,”alisema.
 
Naye Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi, alisema katika hali ya kushangaza baadhi ya makampuni licha ya kwamba yanatumia nishati ya gesi kuzalisha umeme lakini yamekuwa yakiuza umeme kwa bei ya juu.
 (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com)

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!