Thursday, 29 January 2015
VITALU VYA UWINDAJI WA KITALII MWISHO 2018
MAMLAKA ya wanyamapori nchini inatarajia kusitisha umiliki wa vitalu vya uwindaji wa kitalii nchini, ifikapo mwaka 2018, jambo litakalosaidia mamlaka hiyo kumiliki mapori yote ya akiba na kuwa na uwezo wa kubadilisha sera ya matumizi ya mapori hayo.
Aidha, mamlaka hiyo inayotarajiwa kuanza kufanya kazi mwezi ujao nchi nzima itabadilisha maeneo yote ya hifadhi kama ilivyofanywa katika pori la Selou kwa kilometa za mraba 4,000 kutengwa kwa ajili ya utalii wa picha.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema hayo bungeni jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mbogwe, Manyanda Maselle (CCM) aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kubadilisha maeneo ya mapori kuwa na matumizi mengine yenye kuleta faida zaidi.
Akijibu swali hilo, Nyalandu alisema mamlaka hiyo inayoanza kazi Februari 12 mwaka huu, itasaidia kupanga upya matumizi ya mapori ya akiba kama vile inavyopaswa.
Katika swali lake la msingi, Maselle aliuliza Serikali ina mpango gani wa kulitenga Pori la Akiba la Moyowosi kuwa kivutio cha utalii na kwa kuwa halmashauri zenye mapori ya akiba zinapaswa kulipwa asilimia 25 ya mapato ya uwindaji, ni lini wilaya ya Mbogwe itaanza kulipwa fedha hizo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa alisema pori hilo la akiba linatumika kwa shughuli za uwindaji wa kitalii na kuna vitalu nane.
Alisema umiliki wa vitalu vya uwindaji wa kitalii utakoma nchini kote ifikapo mwaka 2018 na baada ya hapo itafanyika tathmini ya vitalu vyote itakayosaidia Serikali kutenga vitalu vinavyofaa kwa utalii wa picha na uwindaji wa kitalii.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment