Wednesday, 7 January 2015

UMEME WA GESI KUANZA MWEZI UJAO

Watanzania waliokuwa wakisubiri kwa hamu kuanza kutumia umeme utokanao na mradi wa gesi asilia wa Kinyerezi, sasa watahitajika kuvuta subira kidogo kutokana na uzalishaji wa nishati hiyo kusogezwa hadi katikati ya mwezi ujao.

Awali, maofisa wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na makandarasi wa mradi kwa nyakati tofauti, walinukuliwa kuwa ujenzi ungekamilika Desemba mwaka jana na uzalishaji wa majaribio ungeanza mapema mwezi huu.
Hata hivyo, ripoti ya maendeleo ya mradi huo iliyotolewa jana na TPDC inaonyesha kuwa baadhi ya masuala ya ujenzi na ununuzi yanatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu na Februari.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa ujenzi wa mradi mzima wa bomba hilo la gesi linalotokea Mtwara hadi Kinyerezi, ulikuwa umekamilika kwa asilimia 94.8 wakati ununuzi ulikuwa ni asilimia 99 mwishoni mwa Novemba.
Akielezea kilichochelewesha, Meneja wa mradi huo kutoka TPDC, Kapuulya Musomba alisema kuwa uzalishaji wa majaribio umesogezwa kutokana na tatizo la usafirishaji wa vifaa lililoathiri ratiba ya awali. Uzalishaji rasmi unatarajiwa kuanza Juni mwaka huu.
“Kuna wakati tulikuwa tukitegemea mitambo iliyoingia bandarini ingetolewa ndani ya wiki moja, lakini haikuwa hivyo,” alisema Musomba.
Kuhusu uwapo wa uchakachuaji wa kuongeza bei mara mbili ya mradi huo, Musomba alisema kiasi cha Sh2 trilioni walizoomba kukamilisha ujenzi huo ndizo zilizomo kwenye mkataba. Novemba, 2014 akiwa mjini Nzega, mkoani Tabora, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwatuhumu vigogo wa Serikali kwa ufisadi wa kuongeza Dola 600 milioni za Marekani (Sh1.02 trilioni) katika ujenzi wa mradi huo hali iliyofanya gharama ziongezeke mara mbili na kufikia Sh2.4 trilioni.
Alisema kuwa awali kampuni inayojenga bomba hilo, ilisema gharama halisi za mradi huo ilikuwa Sh1.20 trilioni, lakini wao wakaongeza mara mbili ya fedha hizo kwa manufaa yao binafsi.
Msomba alibainisha kuwa TPDC haishiriki kumlipa moja kwa moja Mkandarasi zaidi ya kukagua madai ya mkandarasi huyo, kuishauri serikali iidhinishe na hatimaye mkopeshaji wa mradi, Exim Bank ndiye ambaye hulipa fedha hizo moja kwa moja.
“Hata ukiangalia kwenye riba bado mkopo wetu una malipo ya chini sana kuwahi kutokea. Asilimia 75 ya mkopo huo ina riba ya asilimia mbili wakati zilizobakia zina riba ya asilimia 4.3 hivi ni benki gani ulimwenguni inaweza kukopesha kwa kiasi hicho?,” alihoji Mhandisi huyo.
Alisema hana nguvu ya kubishana majukwani na wanasiasa juu ya gharama halisi za mradi huo lakini anayetaka kujiridhisha afanye uchunguzi na kufanananisha na uhalisia wa gharama za ripoti hiyo.
Sehemu hiyo ya kwanza ya mradi wa megawati 150 inajengwa na Shirika la Teknolojia ya Petroli na Maendeleo la China (CPTDC) kwa ushirika na kampuni ya Jacobsen Elektro AS ya Norway

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!