Tanzania ina kila aina ya vituko. Muuza nguo anakuletea shati, badala ya kutaja bei anakuuliza “unataka kununua shilingi ngapi?” Una dhahabu mkononi, unapotaka kuiuza mnunuzi haangalii ina ubora au daraja gani. Anakuuliza “dhahabu hii imefanana na ya nani?” Kama inafanana na ile ya Juma utalipwa kama alivyolipwa Juma. Kama imefanana na aliyouza Mr. Smith basi nawe utalipwa kama alivyolipwa Mr. Smith.
Ukitaka kununua tai mtaa wa Samora, utauziwa kwa bei ya mtaa huo. Lakini kama utabahatika kukutana na mchuuzi huyo mtaa wa Kongo, basi tai hiyo itauzwa kwa bei ya mtaa wa Kongo. Unapoenda kuomba tenda ya kulisha kampuni unaangaliwa ubora wa kitambi chako na siyo elimu au uzoefu wako katika ugavi.
Hili linawakuta sana vijana wanaochipukia kwenye sanaa. Anapoenda kwa mfadhili kwa mara ya kwanza inaangaliwa sauti yake imefanana na ya nani na hata sura yake imefanana na mwimbaji gani. Kama hana hali ya kufanana na nguli, ni lazima awe bingwa wa kupesti ndipo afadhiliwe.
Kabla sijalielewa hili vizuri, nilifikiri huo ni mfumo wa dunia nzima. Niliitazama Marekani na marais wake, nikaona wapo waliofanana kupita maelezo. Hata wewe nikikueleza jinsi Abraham Lincoln na JFK (John F, Kennedy) walivyooana (sorry, walivyofanana) huwezi kuniamini. Lakini ndiyo ukweli kamili; Ebu tazama:
Abraham Lincoln alichaguliwa Congress mwaka 1846 wakati John F. Kennedy alichaguliwa Congress mwaka 1946. Lincoln akachaguliwa kuwa Rais wa Marekani mwaka 1860 na Kennedy akachaguliwa kuwa Rais wa Taifa hilo mwaka 1960. Wote walijihusisha zaidi na haki za binadamu wakati wa uongozi wao.
Wake zao wote wawili walipoteza watoto wakiwa Ikulu ya Marekani. Kila mmoja wa marais hawa alipigwa risasi ya kichwa Ijumaa. Msaidizi wa Rais Lincoln aliitwa Kennedy na wa Rais Kennedy aliitwa Lincoln. Mrithi wa Lincoln aliitwa Johnson, kadhalika wa Kennedy aliitwa Johnson.
Johnson wa Lincoln alizaliwa mwaka 1808, na wa Kennedy alizaliwa mwaka 1908. Muuaji wa Lincoln alizaliwa mwaka 1839 na wa Kennedy alizaliwa mwaka 1939. Wauaji hawa walijulikana kwa majina yao matatu matatu yenye herufi kumi na tano.
Lincoln alipigwa risasi kwenye jumba la sinema lililoitwa Ford na muuaji akakimbilia kujificha kwenye ghala. Muuaji wa Kennedy alipiga risasi kutoka ghalani na kujificha kwenye jumba la sinema lililoitwa Lincoln na lililojengwa na Ford. Tena basi wauaji wao nao waliuawa kabla ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Unaona kufanana huko? Basi nikajua Kennedy alisafiria nyota ya Lincoln. Lakini kichwa kiliniuma sana kwa kujiuliza: kama sote tungefanana, ni nani angemwongoza mwenzake? Au kumwimbia mwenzake? Ni wazi kuwa binadamu wote ni sawa, lakini hata kama unaandika kama Shaaban Robert, utakuwa na mashairi yake?
Ni wazi pia kwamba kila mtu ana akipendacho tofauti na wengine. Kama wewe unapenda nyimbo za hip-hop, kuna wanaopenda nyimbo laini. Hao wanaopenda nyimbo laini pia wana vituko vyao. Huyu anapenda sauti nyororo kama za akina Dolly Paton, yule anataka sauti nzito zenye mikwaruzo kama ya Barry White. Kumbe ndiyo maana vipaji tofauti vinapaswa kuheshimiwa. “Half of the story has never been told” (nusu ya hadithi bado haijatolewa hadharani). Kila kipaji kipya kinapoibuka kinakuja na asilimia sufuri nukta sufuri sufuri kama mia, mwisho moja ya jambo jipya.
Pengine tofauti na wenzetu, wasanii wetu wachanga wanalazimika kuvaa kama fulani, kutembea kama fulani na kuigiza kama fulani ili wafanikiwe. Pia ndiyo maana sanaa yetu inaporomoka kadiri ya muda unavyokwenda. Hakuna kipya. Laiti tungelijua dada Halle Berry (mwigizaji mshindi wa Tuzo za Oscar na Emmy) alihamia New York akiwa hana pa kulala pale. Alikesha na yatima na baadaye akahamia kwenye makazi ya wasio na makazi yaliyomilikiwa na kituo cha YMCA. Wadau walimuibulia hapo.
Hakuna mtu asiyemjua Charlie Chaplin (usipomjua kwa jina hilo utamjua kwa “Chale Mwembamba”). Huyu naye ni mshindi wa tuzo za Oscar kwa uandishi, uigizaji, uongozaji na uzalishaji wa sanaa. Alikuwa mzururaji jijini London baada ya baba yake kufa na mama yake kupata uchizi. Lakini baada ya kugunduliwa kipaji chake cha kipekee, aliifundisha dunia kuwa komedi nazo ni mali
Hata James Bond yule wa picha za 007 aliyeitwa Daniel Craig hakuwa na kwao. Alilala kwenye vibaraza vya watu jijini London hadi “alipotoka”. Yupo KRS-One, Lil’ Kim (mshindi wa tuzo za Grammy), Tupac Shakur, Sylvester Stallone (mshindi wa Oscar) na hata Shania Twain. Mashabiki wa Shania wa leo ni masista du na mabrazameni, lakini yeye alikuwa peperu peperu tu kabla hajaibuliwa.
Kuna umuhimu wa kusaka vipaji vipya majalalani. Dhahabu haiokotwi mchangani. Kama tunasubiri mwenye suti kama ya King Yellowman tumpe kidaka sauti, yatupasa kwanza kujua kuwa King aliokotwa baada ya kutupwa na wazazi wake kwa vile alikuwa na ulemavu wa ngozi.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment