Tuesday, 20 January 2015

MICHEZO: TUNASUBIRI MUDAUFIKE TUIUE AZAM-KAGERA


Jackson Mayanja, kocha mkuu wa Kagera Sugar, amesema kikosi chake kiko vizuri na wanasubiri muda ufike ili 'wawaue' wapinzani wao Azam FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza leo.



Baada ya kuifunga Stand United 1-0 usukumani mjini Shinyanga Jumamosi, Azam FC, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), wanashuka kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kuwakabili Kagera Sugar katika mechi yao ya kiporo ya raundi ya 10 ya ligi hiyo.

Mechi hiyo Na. 67 ilipaswa kuchezwa Januari 10 mjini Bukoba, Kagera lakini ikapigwa kalenda kutokana na timu nne za Tanzania Bara, Azam, Mtibwa Sugar, Simba na Yanga kualikwa kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar Januari 1-13.

Akiwa jijini Mwanza jana mchana, Mayanja aliiambia NIPASHE kuwa wamefanyia kazi upungufu uliojitokeza katika mechi yao iliyopita waliyolala 1-0 dhidi ya Mbeya City jijini humo Jumamosi, na sasa wako vizuri kupambana na kikosi cha Mcameroon Joseph Omog cha Azam FC.

"Tunachokisubiri kwa sasa ni muda tu, tunangoja muda ufike ili tufanye la maana hapa Mwanza. Tumejipanga, tumezungumza na vijana na tumewajenga kiakili," alisema Mganda huyo.

Azam FC waliotua jijini humo juzi wakitokea Shinyanga, walifanya mazoezi kwenye Uwanja CCM Kirumba jana asubuhi kuweka miili sawa kabla ya mechi hiyo.

Meneja wa Azam FC, Jemedari Said alisema jana kuwa wamekusudia kuchukua pointi sita Kanda ya Ziwa na kumalizia kwa Simba Jumamosi kabla ya kwenda Lubumbashi, DR Congo kushiriki mashindano maalum ya kimataifa ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika mwezi ujao.

Azam iko nafasi ya pili katika msimamo wa VPL ikiwa na pointi 17 sawa na vinara Mtibwa Sugar, tatu mbele ya Kagera Sugar iliyoko nafasi ya sita.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!