Mashine ya mionzi ya kutolea huduma ya matibabu ya saratani katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, inatarajia kuanza kufungwa wiki hii ikiwa ni sehemu ya ukarabati wake hivyo kuendelea kukabiliana na ukosefu mitambo hiyo katika hospitali nyingi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid (pichani), alisema mashine hiyo ni moja ya zilizoharibika na kwamba ufungaji wake unaanza ndani ya wiki hii baada ya wataalamu na vifaa vyake kutarajia kuwasili kutoka Canada.
Aliongeza kuwa serikali pia ipo katika mkakati wa kuleta mtambo mwingine mpya wa mionzi ambao utagharimu Dola za Marekani milioni moja.
Kwa mujibu wa Dk. Rashid, gharama hizo zitachangiwa na serikali kwa asilimia 50 na asilimia 50 zitatolewa na Shirika la Kimataifa la Atomi ‘International Atomic Agency.’
Kuhusu hali ya saratani nchini, alisema, hali bado ni mbaya kwani hadi sasa idadi ya wagonjwa inaendelea kuongezeka.
Kwa mujibu wa Waziri Rashid, hadi sasa kuna wagonjwa 33, 834 ambao wanaugua ugonjwa huo nchini kote.
Kati ya idadi hiyo, 7, 304 wanasumbuliwa na saratani ya shingo ya kizazi na iliyobaki ni kwa aina nyingine ikiwamo ya ngozi na matiti.
Alisema kwa sasa chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi imeanza kutolewa katika mkoa ya Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa Waziri Rashid, walengwa wakubwa wa chanjo hiyo ni pamoja na wasichana kwani katika umri huo kuna uwezekano wa kupatwa na ugonjwa huo.
Aliongeza kuwa, matibabu ya saratani kwa kutumia Maxine hine hizo pia huweza kutolewa katika hospitali za kanda na ile ya Bugando, jijini Mwanza.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment