Thursday, 29 January 2015

LIPUMBA AUGUA GHAFLA, ATINGA KORTINI


MWENYEKITI wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka ya kuwashawishi wafuasi wake watende kosa la jinai.
Lipumba alifikishwa mahakamani hapo jana saa 8 mchana na kusomewa mashitaka saa 9:10 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Isaya Arufani.


Wakili wa Serikali, Joseph Maugo akisaidiwa na Hellen Moshi alidai katika tarehe tofauti kati ya Januari 22 na 27 mwaka huu, akiwa Mwenyekiti wa CUF, aliwashawishi wafuasi wake watende kosa la jinai. Baada ya kusomewa mashitaka, Prof Lipumba alikana na kudai “si kweli, ni uongo mtupu”.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo, haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Prof Lipumba aliachiwa kwa dhamana baada ya kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni mbili na kuwa na wadhamini wawili, ambao kila mmoja alisaini hati ya Sh milioni mbili. Kesi itatajwa tena Februari 26 mwaka huu.
Akizungumza nje ya Mahakama, Lipumba alisema nchi haitendi haki, pia aliwashukuru wanasheria, wanachama na wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) waliopo bungeni kwa ushirikiano wao mpaka amepata dhamana.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya makao ya polisi, Dar es Salaam, Profesa Lipumba alikamatwa na polisi bila kosa, kwani wao walishaahirisha maandamano na kilichokuwa kinaendelea ni wao kwenda kuwapa taarifa wenzao wa Mbagala na sio kuandamana.
“Mimi nipo nje kwa dhamana na tumefunguliwa kesi ya kuandamana bila kibali,” alisema Profesa Lipumba.
Akieleza chanzo kilichosababisha yeye na wafuasi wake kukamatwa, alisema wakati wakielekea Mbagala Zakhem kuwapa wenzao taarifa za kuahirishwa kwa maandamano, polisi waliwavamia na kuanza kuwapiga na kuwakamata kwa nguvu kisha kuwapandisha kwenye magari.
“Polisi walituvamia wakati tupo njiani kuelekea Mbagala Zakhem kuwataarifu wenzetu kuwa tumeahirisha maandamano ya maadhimisho ya kuwakumbuka mashujaa waliopoteza maisha Januari 27 mwaka 2001,” alisema Profesa Lipumba Baada ya hapo, Profesa Lipumba aliingia kituoni ambapo waandishi wa habari walizuiliwa kuingia na kubakia nje, kusubiria kujua nini kitaendelea.
Mara baada ya kuingizwa polisi, saa saba mchana, kwa siri polisi walimpandisha Profesa Lipumba kwenye gari lenye namba za usajili PT 2566 na kuwadanganya waandishi wa habari kuwa waendelee kusubiri, watajulishwa ni gari gani atapanda na wapi ataelekea.
Taarifa iliyotolewa na Mwanasheria anayesimamia kesi hiyo, John Mallya alisema Profesa Lipumba anaumwa na anasumbuliwa na presha ya kushuka, hivyo wanampeleka katika hospitali ya UN Clinic iliyopo Kinondoni kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Alisema baada ya kupatiwa matibabu, ndio itajulikana ni hatua gani itafuata. Lakini, licha ya kuwepo kwa taarifa ya kumpeleka mwanasiasa huyo hospitalini, badala yake walimpeleka mahakamani moja kwa moja ambako alisomewa mashitaka ya kuandamana bila kibali cha polisi.
Akizungumzia afya yake, Prof Lipumba alisema anaendelea vizuri, na kwamba alikuwa anasumbuliwa na malaria pamoja na presha, lakini ameambiwa apate mapumziko na kufanya mazoezi.
Imeandikwa na Flora Mwakasala na Emmannuel Ghula.

HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!