Saturday, 24 January 2015

KIVUKO CHA MV MAGOGONI CHAOGOPESHA


BAADHI ya wakazi wa Kigamboni wanaotumia kivuko cha Mv Magogoni wameiomba serikali kukifanyia marekebisho kivuko hicho ambacho kimekuwa kikipata hitilafu mara kwa mara na kutishia maisha ya abiria wake.


Wakizungumza na gazeti hili wananchi hao walisema kivuko hicho kimekuwa na hitilafu kwa muda mrefu kabla hata ya kivuko cha Mv Kigamboni kwenda kufanyiwa matengenezo.
Walisema kwa sasa ni jambo la kawaida mtu kupanda kivuko hicho na baada ya muda kupoteza uelekeo, hali ambayo inawafanya wakazi wengi wa Kigamboni kukikwepa na kusubiria kivuko kidogo.
Akizungumzia tatizo hilo Mwanamisi Juma, mkazi wa Kigamboni alisema:“Kivuko hiki kimekuwa na hitilafu ya mara kwa mara hivyo mimi nikifika hapa nikikuta kivuko kidogo hakipo hata kama nina haraka kiasi gani sipandi hicho kikubwa hadi kidogo kitakaporudi kupakia kwa sababu naogopa kuhatarisha maisha yangu na pia sijui kuogelea hatari itakapotokea,” alisema.
Naye Salim Hamad, mkazi wa Kigamboni alisema anaogopa kivuko hicho na haamini kwamba kina usalama kwa sababu hata vifaa vya uokoaji ni vya muda mrefu na haamini kama ni vizima na vina uwezo wa kufanya kazi endapo hitilafu itatokea.
Gazeti hili lilimtafuta Dk Magufuli jana kuzungumzia suala hilo, lakini hakupatikana. Hata hivyo, Septemba mwaka jana wakati alipotembelea eneo kilipofanyiwa matengenezo kivuko cha Mv Kigamboni, yaliyokuwa yanafanywa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) Kamandi ya Maji, Dk Magufuli alisema “Nawaahidi kivuko cha Mv Kigamboni kikirudi mjipange tena kwa sababu tutawaletea Kivuko cha Mv Magogoni nacho mkifanyie matengenezo.”

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!