Saturday, 24 January 2015

JINSI BENDI YA WALEMAVU INAVYOKUBALIKA NCHINI

Nimekutana na watu wengi wakidai kuwa wana tatizo fulani linalowafanya washindwe kuonyesha uwezo wao kwenye kazi fulani, wengine wakikimbia kuomba, kuwa tegemezi kwa madai kuwa ni walemavu.

Ulemavu siyo kikwazo cha kushindwa kutekeleza majukumu ya msingi ya kila binadamu ingawa wakati mwingine ni changamoto.
Changamoto hiyo na nyingine nyingi wanakutana nazo watu wenye walemavu zimefanyiwa kazi na wanamuziki wa Bendi ya Tunaweza ambao kwa ujumla wao ni walemavu wa viungo, lakini kila mmoja anaonyesha kipaji chake kadri awezavyo.
Wanamuziki wa bendi hii walikutana mwaka 2008, wakikusanywa na Masudi Wanani na kuanzisha bendi hiyo iliyokuwa na wanamuziki 10 na walikuwa wanafanyia mazoezi eneo la Mkwizu kwa mafundi magari, Magomeni jijini Dar es Salaam.
Mtayarishaji wa muziki wa bendi hiyo, Kudra Mazongela anawataja wanamuziki waanzilishi wa bendi hii, kiongozi wao Idd Tembo, Salehe Abdallah akiwa ndiye dansa, Mwakatobe Peter analikung’uta gitaa la solo na Emannuel Mpesa anapiga kinanda.
Mazongela anasema kuwa yeye mwenyewe pamoja na kuimba pia ni mpiga gitaa la bezi, wanamuziki wengine walioanzisha bendi hiyo ni Irene Malekela na Latifa Abdallah ambao ni waimbaji.
Anasema waliendelea kujifunza kwa kuhama hama kutokana na kukosa eneo maalumu la kufanyia mazoezi hadi walipofanikiwa kurekodi albamu yao ya kwanza yenye jina la ‘Raha Duniani’.
Anazitaja nyimbo zilizokuwamo kwenye albamu hiyo kuwa ni ‘Raha Duniani’, ‘Tutenge’, ‘Mbilimbi’, ‘Kokolido’, ‘Walemavu Tuungane’ na ’Tunamshukuru Mungu’.
Mazongela anafafanua kuwa nyimbo zote za albamu hiyo zinawagusa watu wenye matatizo ambao wanahitaji kupewa moyo au kujitambua na kukataa kubweteka kwa kujichanganya kutafuta maisha.
Anatolea mfano wimbo wa ‘Walemavu Tuungane’ lengo lake ni kuwakumbusha kwamba wanatakiwa kuwa kitu kimoja ili iwe rahisi kuwezeshwa kwani kwa umoja wao wanaweza kufanya vitu vya ajabu kuliko wakigawanyika.
Mazongela anafafanua kuwa wimbo wa ‘Tunamshukuru Mungu’, lengo lake ni kuwakumbusha waja wote kuwa wanatakiwa kushukuru kwa hali yoyote waliyokuwa nayo cha msingi bado roho inadunda.
“Tumeungana na hadi sasa tupo pamoja, tukiwezeshwa tunaweza kwa sababu kila mmoja anakubali hali aliyokuwa nayo, kumshukuru Mungu katika hili ni lazima kwani ukiwa unalia huna miguu kuna mwingine hana hata mdomo wa kuonyesha kuwa analia hivyo hata akilia hakuna anayejua,” anasema Mazongela.
Anasema mbali ya kuwa na vipaji, umoja ndiyo umesababisha wawe pamoja hadi leo kwa sababu wana changamoto nyingi ikiwamo kukosa vyombo vya kufanyia shoo na hata mazoezi.
Mazongela anasema kuwa kwa sasa wamepewa eneo la kufanyia mazoezi na mwimbaji wa Bendi ya Segere, Siza Mazongela ambaye ni dada yake hivyo kwa sasa wanafanyia mazoezi hapo.
Anaeleza kuwa walibahatika kuagiziwa vyombo na marehemu Isihaka Kibene, ambapo hadi anakutwa na umauti vilikuwa havijafika na vilipofika hawakuwa na fedha za kuvigomboa na mfadhili wao huyo alikuwa amekwishatangulia mbele ya haki.
Anafafanua kuwa ili waweze kuvipata vyombo hivyo ambavyo vipo mikononi mwa mtu ambaye hakutaka kumtaja wanahitaji kuwa na kiasi cha Sh3 milioni.
“Hatuna fedha ya kugomboa vyombo vyetu, uwezo wa kupata milioni tatu hatuna kwa sababu hatufanyi shoo,” anasema Mazongela. Anasisitiza kuwa kama watapata mfadhili wa kuwagombolea vyombo vya atakuwa amewasaidia kwani kwa sasa wanashindwa kufanikisha malengo yao kutokana na kukosa vyombo vitakavyowawezesha kufanya mazoezi kwa kujiachia na kufanya shoo zitakazokuwa zinawaingizia fedha na kujikimu kimaisha.
“Licha ya kupata eneo na kuazimwa vyombo vya kufanyia mazoezi hatuna uhakika wala kauli ya kujivunia kuwa kwa sasa Bendi ya Tunaweza inafanya hiki na hiki, kwa sababu hatujafanikiwa,” anasema Mazongela.
Mazongela aliwaomba wafadhili ambao watakuwa na nia ya kuwasaidia wafikirie na suala la kuwapatia gari kwa sababu inawawia vigumu kukutana kutokana na wengi wao kushindwa kumudu changamoto za usafiri kutokana na maumbile yao.
Anasema iwapo watapata vyombo, usafiri wa uhakika watafanya makubwa zaidi kuliko sasa, ingawa hawajakata tamaa bado wanapambana.
Kalunde Jama

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!