Tuesday, 6 January 2015

BOMBA LA GESI MTWARA -DAR KUKABIDHIWA JUNI



Makabidhiano ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia, likiwamo bomba la kuisafirisha kutoka Mtwara kwenda jijini Dar es Salaam, kati ya mkandarasi na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) yanatarajiwa kufanyika Juni, mwaka huu, baada ya kukamilika kwa asilimia 100.



Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Michael Mwanda na Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Usambazaji wa Gesi (Gasco), Mhandisi Kapuulya Musomba, mradi huo ulioanzishwa mwaka 2010, mpaka sasa umefikia asilimia 94.

Akielezea utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya gesi hiyo katika mkutano kati ya waandishi wa habari na bodi na menejimenti ya shirika hilo, jijini Dar es Salaam jana, Musomba alisema mradi huo umegharimu dola za Marekani 1.225 (zaidi ya Sh. trilioni 1.8), ambazo ni za mkopo.

Alisema Benki ya Exim ya nchini China imechangia asilimia 95, huku Serikali ya Tanzania ikiwa imechangia asilimia tano katika fedha hizo.

Musomba alisema fedha hizo zinatumika kugharimia maeneo mtambo wa kusafisha gesi asilia wa Songo Songo, ambao umegharimu dola za Marekani 151,735,000.

Pia mtambo wa kusafisha gesi hiyo wa Mnazi Bay umegharimu dola za Marekani 197,877,000 wakati bomba la kuisafirisha likigharimu dola za Marekani 875,715,000.

Musomba alisema upande wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi wamefika asilimia 97 na mitambo aslimia 87.

“Hizo asilimia zinahesabika; kuna sehemu ya matayarisho, usanifu, manunuzi na ujenzi,” alisema Musomba.

Aliongeza: “Manufaa makubwa namba moja ya mradi huo ni kusaidia uchumi wa nchi. Tunaamini tukipata umeme wa kufaa na wa kutosha tutapata nafasi ya kutoka hapa tulipo sasa na sisi tukaingia kati ya nchi chenye uchumi wa kati.”

Alisema mbali na hilo, muda wote wa mradi kumekuwapo na ajira za watu 1,000 kila siku na kwamba, manufaa mengine yataendelea kuwapo zaidi.
“Mradi uko katika viwango, mradi uko on ‘sheju’, tunategemea kukabidhiana mwezi Juni, mwaka huu,” alisema Musomba.

Alisema mradi huo unatokea Mnazibay, ambako kuna mtambo wa kuchakata gesi na kwamba, kuna matoleo ya Mtwara, Lindi, Kilwa, Mkuranga, Kinyerezi, Ubungo na Tegeta.

Alisema mpaka Agosti, mwaka jana, serikali ilikuwa imeshatumia Sh bilioni 20 kwa kazi ya uthamini.

Naye Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mafuta na Gesi wa TPDC, Anna Kidirifa, alisema usalama katika ujenzi wa miundombinu ya gesi umeimarishwa na kwamba, kutakuwa na vifaa maalumu vya kupeleka taarifa juu ya kila kitakachokuwa kikifanyika kwenye bomba.

Alisema pia kutakuwa na kamera za kurekodi matukio na doria za kutumia helikopta na pikipiki kuangalia nini kitakachokuwa kinafanyika kwenye bomba pamoja na vibao vya kuelekeza.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!